Header Ads

ad

Breaking News

TBS YATENGA MILIONI 250 KUHUDUMIA WAJASIRIAMLI

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS ), Dkt. Athuman Ngenya, akizungumza wakati wa kikao kazi cha TBS, wahariri na waandishi wa habari kilichoratibiwa na Ofisa ya Msajili wa Hazina (TR) na kufanyika leo Aprili 15,2024 jijini Dar es Salaam.

Na Frank Balile

SERIKALI ya Awamu ya Sita inayoongozwa wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan kupitia Shirika la Viwango Tanzania (TBS), imekuwa ikitenga zaidi ya milioni 250 kwa lengo la kuhudumia wajasiriamali wadogo bila ya malipo yoyote.

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dkt.Athuman Ngenya, katika kikao kazi kilichowakutanisha  wahariri na waandishi wa habari leo Aprili 15,2024 jijini Dar es Salaam, kwa uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina.

Dkt.Ngenya amesema kuwa, kwa kipindi cha miaka mitatu, jumla ya leseni za ubora wa bidhaa 2,106 zilitolewa kwa wazalishaji mbalimbali wa bidhaa nchini sawa na asilimia 105.3 ya lengo la kutoa leseni 2,000.

Amesema kati ya leseni hizo, jumla ya leseni 1,051 zilitolewa bure kwa wajasiriamali wadogo.

"Katika kipindi cha miaka mitatu, tulitoa leseni za ubora wa bidhaa 2,106 kwa wazalishaji mbalimbali nchini sawa na asilimia 105.3 ya lengo la kutoa leseni 2,000," amesema Dkt.Ngenya.

Dkt.Ngenya amesema kuwa, katika kipindi cha miaka mitatu wadau 5,789 kutoka mikoa mbalimbali nchini walipewa mafunzo mbalimbali, huku TBS ikiendelea kutoa mafunzo kwa wajasiriamali wadogo (MSEs) na wazalishaji ili kuwawezesha kuzalisha bidhaa zinazokidhi matakwa ya viwango vya ubora na usalama na hatimaye kukidhi ushindani wa masoko ya ndani, kikanda na kimataifa.

Mkurugenzi mkuu huyo amesema katika kuhakikisha soko linakuwa bidhaa zenye ubora, TBS hufanya ukaguzi wa bidhaa zinazozalishwa nchini na kuweka utaratibu wa kukagua viwanda vyote nchini ili kuhakikisha kwamba, vinazalisha bidhaa zenye ubora unaotakiwa.

Dkt.Ngenya amesema kuwa, Shirika linahakikisha soko linakuwa bidhaa zenye ubora kwa kufanya ukaguzi wa bidhaa zinazotoka nje ya nchi na kudhibiti ubora wa bidhaa zinazoingizwa nchini kutoka nje kwa kutumia mfumo wa Pre- Shipment Verification of Conformity to Standards (PVoC) pamoja na kufanya ukaguzi pindi bidhaa zinapowasili nchini (Destination Inspection).

Ameongeza kwamba, katika kipindi cha miaka mitatu, jumla ya shehena 100,851 kabla hazijaingizwa nchini sawa na asilimia 99 ya lengo la kukagua shehena 102,083, wakati jumla ya bidhaa 151,570 kutoka nje ya nchi zilikaguliwa baada ya kufika nchini sawa na asilimia 77 ya lengo la kukagua bidhaa 197,417.

Amesema TBS hufanya kaguzi za mara kwa mara sokoni na viwandani kwa ajili ya kuhakikisha bidhaa zilizopo zinakidhi matakwa ya viwango husika, kwa kushirikiana na taasisi nyingine za Serikali kama Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Tume ya Ushindani (FCC), Ofisi ya Rais TAMISEMI, Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya usalama kufanya ukaguzi ili kubaini bidhaa zisizokidhi matakwa ya viwango na kuchukua hatua stahiki.

"Tunashirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Tume ya Ushindani (FCC), Ofisi ya Rais TAMISEMI, Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya usalama kufanya ukaguzi kwa lengo la kubaini bidhaa zisizokidhi matakwa ya viwango na kuchukua hatua stahiki," amesema Mkurugenzi Mkuu Dkt.Ngenya.

Amesema kuwa, TBS hutoa elimu kwa umma kupitia njia mbalimbali ili kukuza uelewa juu ya masuala ya viwango na udhibiti ubora ikiwemo kushiriki makongamano, maonesho, warsha na semina.

Dkt.Ngenya amesema kuwa, TBS huandaa  mikutano  na  wadau  wa  masuala  ya  viwango kwa kuendesha kampeni za elimu kwa umma katika ngazi za wilaya na mashuleni, kutumia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, kuandaa matangazo, majarida na vipeperushi na kutoa mafunzo mbalimbali kuhusu masuala ya ubora na usalama.

Meneja Udhibiti Ubora wa Bidhaa ziingiazo na zinazotoka nchiniwa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Gervas Kaisi, akielezea jambo wakati wa mkutano huo.

Mkurugenzi wa Udhibiti Ubora TBS, Lazaro Msasalaga, akijibu maswali ya wahariri na waandishi wa habari katika kikao kazi kilichoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina.
Mjumbe wa Kamati ya Utendaji Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Salim Said Salim akizungumza jambo wakati wa kikao kazi

Mkurugenzi wa TBS Dkt. Athuman Ngenya (kulia), akimsikiliza Mjumbe wa Kamati ya Utendaji Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Salim Said Salim (kushoto), wakati wa kikao kazi cha Shirika la Viwango Tanzania (TBS), wahariri na waandishi wa habari kilichoratibiwa na Ofisa ya Msajili wa Hazina (TR) na kufanyika jijini Dar es Salaam. Katikati ni Mkurugenzi wa Udhibiti Ubora TBS, Lazaro Msasalaga.

Afisa Mwandamizi wa Habari na Mawasiliano Ofisi ya Msajili wa Hazina, Sabato Kosuri akifafanua jambo wakati wa kikao kazi kati ya TBS, wahariri na waandishi wa habari leo Aprili 15,2024 jijini Dar es Salaam. Kikao kazi hicho kimeratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina.
Wahariri na waandishi wa habari wakifuatilia wasilisho
Wahariri wakisikiliza

No comments