Header Ads

ad

Breaking News

TBS KUJENGA MAABARA ZA KISASA MWANZA, ARUSHA

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS ) Dkt. Athuman Ngenya,  akizungumza wakati wa kikao kazi kati ya TBS, wahariri na waandishi wa habari kilichoratibiwa na Ofisa ya Msajili wa Hazina leo Aprili 15,2024 jijini Dar es Salaam.

Na Frank Balile

SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS), linatarajia kuanza  ujenzi wa maabara ya kisasa mkoani Mwanza itakayohudumia kanda ya Ziwa na mkoani Arusha itakayohudumia kanda ya kaskazini, yakiwa ni mafanikio ndani ya miaka mitatu ya uongozi wa Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan.

Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dkt.Athuman Ngenya, amesema maabara ya kanda ya ziwa itahudumia mikoa sita ambayo ni Mwanza, Kagera, Mara, Geita, Shinyanga na Simiyu, wakati maabara ya kanda ya Kaskazini itaudumia mikoa minne ambayo ni Arusha, Kilimanjaro, Tanga na Manyara.

Kauli hiyo ameitoa katika kikao kazi kilichofanyika leo Aprili 15,2024 jijini Dar es Salaam kati ya TBS, wahariri na waandishi wa habari na kuratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina.

"Shirika linatarajia kuanza ujenzi wa maabara ya kisasa katika kanda ya Ziwa ambayo itakuwa Mwanza na kanda ya kaskazini itakuwa mkoani Arusha, ambapo maabara ya kanda ya ziwa itahudumia mikoa sita ambayo ni Mwanza, Kagera, Mara, Geita, Shinyanga na Simiyu," amesema Mkuriugenzi Mkuu Dkt.Ngenya.

"Maabara ya kanda ya Kaskazini hii itAhudumia mikoa minne ambayo ni Arusha, Kilimanjaro, Tanga na Manyara," amesema.

Dkt.Ngenya amesema kuwa, shirika limefanikiwa kusogeza huduma karibu na wananchi kupitia ofisi za kanda saba ambazo ni Kanda ya Kaskazini (Arusha), Kanda ya Kusini (Mtwara) ,Kanda ya Nyanda za Juu Kusini (Mbeya), Kanda ya Magharibi (Kigoma) ,Kanda ya ziwa (Mwanza) ,Kanda ya Kati (Dodoma) na Kanda ya Mashariki (Dar es Salaam).

Amesema kuwa, kanda hizo zina ofisi katika mipaka, bandari na viwanja vya ndege.

Ameongeza kuwa, Shirika limewekeza kwenye ununuzi wa vifaa vya maabara vya kisasa (state-of-the-art-equipment), kwa kutumia fedha za ndani na misaada kutoka kwa wadau mbalimbali wa maendeleo.

MKurugenzi Mkuu huyo amesema kuwa, Shirika lina maabara 12 pale Ubungo jijini Dar es Salaam ambazo zimehakikiwa na kupatiwa cheti cha ithibati ya umahiri wa kimataifa (accreditation).

"Hatua hii imesaidia majibu ya sampuli kutoka katika maabara zetu kuaminika duniani kote na hivyo kurahisisha biashara," amesema.

Dkt.Ngenya amesema Shirika limetengeneza mifumo ya kielektroniki inayotumika kutoa huduma zake ambayo imewezesha wateja kupata huduma za TBS popote walipo kwa wepesi na haraka hivyo kupunguza gharama kwa wateja.

Amesema kwa kipindi cha miaka mitatu, jumla ya viwango 1,721 vya kitaifa viliandaliwa sawa na asilimia 101.2 ya lengo la kuandaa viwango 1,700. Viwango hivyo viliandaliwa katika nyanja mbalimbali.

Amesema shirika hilo limeshiriki katika uandaaji wa viwango vya kibiashara vya Afrika Mashariki na Afrika nzima.

Dkt.Ngenya ametaja majukumu mengine kuchukua na kupima sampuli za bidhaa zinazokusanywa na wakaguzi wa TBS, kwa lengo la kutekeleza viwango au kwa kuzingatia maombi ya mzalishaji.

Amesema TBS itaendelea kutoa mafunzo kwa wenye viwanda na biashara juu ya uzalishaji na utoaji huduma bora kwa kuzingatia viwango na Kuvifanyia ugezi vipimo vya vifaa vya upimaji viwandani na vya kibiashara katika nyanja za uzito, urefu, ujazo, nishati na halijoto.

Majukumu ya Shirika la Viwango Tanzania yameainishwa katika Kifungu cha 4 (1) (a) – (v) cha Sheria ya Viwango Sura Na. 130. Majukumu hayo kwa ufupi ni kpamoja na kutayarisha na kutangaza Viwango vya ubora vya Tanzania kwenye sekta zote za uchumi. 

Kipaumbele kimewekwa katika viwango vya kitaifa katika nyanja za nguo, ngozi, kilimo na chakula, madawa (kemikali), uhandisi na mazingira.

Kutekeleza viwango vya ubora vilivyotangazwa kwa kutumia mifumo mbalimbali ya udhibiti ubora kama vile ukaguzi na upimaji wa bidhaa kabla ya kusafirishwa kuja nchini, upimaji wa bidhaa kwa kuzingatia matakwa ya kiwango au ya mzalishaji na usajili wa mifumo ya ubora.

Maofisa wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), wakijadiliana jambo wakati wa kikao kazi kilichowakutanisha na wahariri wa vyombo vya habari leo Jumatatu Aprili 15,2024 jijini Dar es Salaam
Afisa Mwandamizi wa Habari na Mawasiliano Ofisi ya Msajili wa Hazina, Sabato Kosuri, akizungumza katika mkutano huo.
Wahariri wakisikiliza wasilisho
Wakisikiliza kwa makini

Wakiwa makini kusikiliza wasilisho
Wahariri na waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali wakifuatilia wasilisho la Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Athuman Ngenya leo Jumatatu Aprili 15,2024 jijini Dar es Salaam.

No comments