Header Ads

ad

Breaking News

SERIKALI YATUA RUFIJI, KIBITI KUZUNGUMZA NA WAATHIRIKA WA MAFURIKO

Na Mwandishi Wetu, Maelezo

MAWAZIRI na makatibu wakuu wa kisekta wakiongozwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu,  Jensta Mhagama na Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi, Aprili 10, 2024 wametembelea Wilaya za Rufiji katika kijiji cha Muhoro na Kibiti kijiji cha Mtunda mkoani Pwani kujionea hali halisi ya mafuriko yaliyoikumba wilaya hiyo na kuzungumza na wahanga ambao wamekusanyika kwenye vituo mbalimbali baada ya kukosa makazi.

Akizungumza kwa niaba ya Serikali, Mhagama aliwasilisha salamu za pole kutoka Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa wahanga, ambapo pamoja na salam hizo alisema Serikali imelipa uzito suala hilo na ipo kazini kuhakikisha huduma zote muhumu ikiwemo chakula, makazi na madawa vinapatikana katika kipindi hiki ambacho familia hizo zimepoteza makazi.

“Uhai wa wananchi ni jambo la kwanza, tumekuja hapa kuhakikisha tunawapatia huduma zote muhimu katika kipindi hiki ambacho mnakabiliwa na janga la mafuriko, nimeongozana na viongozi mbalimbali wakiwemo Mawaziri wa kisekta ambao kila mmoja ana timu ya wataalamu tayari wameshaanza kazi, kuna mahitaji muhimu yameshafika na mengine yapo njiani kikiwemo chakula, naomba chakula hicho kitumiwe na wahanga tu, tutafatilia,”alisema  Mhagama.

Aidha, alitoa rai kwa watendaji kuhakikisha misaada inayopelekwa hususan chakula inawafikia walengwa na kwamba Serikali itafanya ufuatiliaji wa karibu kuhakikisha pasiwepo watu wasio walengwa kujinufaisha na misaada hiyo ambapo alionya hatua kali zitachukuliwa kwa atakayebainika.

Akizungumza katika Kituo cha Televisheni ya Taifa (TBC) baada ya ziara hiyo, Msemaji Mkuu wa Serikali, Matinyi, alitolea ufafanuzi wa chanzo cha mafuriko hayo kuwa, Serikali ilipokea utabiri kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), wa kwamba nchi itegemee mvua kubwa za El Nino ambazo zitaungana na mvua za vuli pamoja na masika. 

Mvua hizo zilianza Oktoba, 2023 na kwamba, taarifa ilitolewa kwa wananchi ili kuchukua taadhari.

“Serikali imetoa maelekezo kadhaa kwa wahanga wa janga hili ikiwemo kuhamia maeneo salama ambapo tayari viwanya 6,000 vimepimwa na vitatolewa bure, wakazi wa vijiji hivyo wametakiwa kuendelea kuchukua tahadhari ili kuepuka matatizo yanayoweza kuambatana na janga la mafuriko ikiwemo kujilinda na mamba wanaotoka mtoni pamoja na kutumia dawa ili kuepuka magonjwa ya mlipuko,” alisema Matinyi.

Alisema kwa upande wa chakula, hadi sasa tayari mahindi tani 40 yamepelekwa na unga kiasi cha tani 150 kitatolewa, vitu vingine ni maharagwe tani 50 na mafuta ya kupikia lita 5,000 vitafikiswa katika maeneo hayo ambayo wahanga wameweka kambi ili kuhakikisha wanapata mahitaji muhimu.

No comments