Header Ads

ad

Breaking News

SERIKALI YAWAFUTA MACHOZI WALIOATHIRIWA NA TEMBO WILAYANI NACHINGWEA

Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea, Mohamed Hassan Moyo 
 Na Beatus Maganja

SERIKALI kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imetoa kifuta jasho na kifuta machozi cha zaidi ya shilingi millioni 399 kwa wananchi 1,658 walioathiriwa na wanyamapori wakali na waharibifu katika wilaya ya Nachingwea mkoani Lindi.

Kauli hiyo imetolewa Aprili 9, 2024 na Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea, Mohamed Hassan Moyo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika ziara ya kuelezea jitihada zinazofanywa na Serikali kupitia MAMLAKA ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), katika kukabiliana na wanyamapori wakali na waharibifu, ziara iliyofanywa na TAWA mkoani humo.

"Serikali kupitia utaratibu wake wa kifuta jasho na kifuta machozi, wahanga zaidi ya 1,658 wilayani Nachingwea walipatikana, lakini fedha ambazo Dkt. Samia Suluhu Hassan kazileta kwa ajili ya kifuta jasho mwaka jana ni shillingi 399, 405,000 na wale wote ambao walikuwa wanastahili kupata kifuta jasho walipata," alisema Moyo.

Moyo amesema wilaya yake imekuwa ikikabiliwa na changamoto kubwa ya wanyamapori wakali na waharibifu, hususan tembo wanaoathiri mali na maisha ya wananchi, lakini pamoja na changamoto hizo amekiri kuwepo na jitihada nyingi zinazofanywa na Serikali kupitia TAWA na Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI), katika kuelimisha wananchi mbinu mbalimbali za kukabiliana na wanyamapori pamoja na kuwadhibiti.

"Jitihada za TAWA zimefanyika mara nyingi na nimekuwa nikishiriki, jitihada moja ni kwa kutumia helikopta katika kuwaswaga au kuwafukuza wanyama wakali aina ya tembo," alisema mkuu huyo wa wilaya.

Akibainisha jitihada zilizofanywa na TAWA katika kukabiliana na changamoto za wanyamapori wakali na waharibifu Kanda ya Kusini, Mashariki, Mhifadhi Mkuu Kitengo cha Oparesheni, Linus Chuwa amesema TAWA imeanzisha vituo 10 vya askari wa kukabiliana na wanyamapori hao, ambapo vitano kati ya 10 ni vya kudumu na vingine vitano ni vya muda mfupi hasa yanapotokea matukio ya wanyamapori hao.

TAWA imefanikiwa kununua gari jipya kwa ajili ya kituo cha Malola ambalo hutumiwa na askari wa kituo hicho, pia imenunua ndege nyuki (drones), maalumu kwa ajili ya kufukuzia tembo ambazo zilitumika katika zoezi la kufukuza tembo mwaka jana (2023), zoezi ambalo linatajwa kufanikiwa kwa kiasi kikubwa.

Jitihada nyingine zilizofanywa na TAWA kwa kushirikiana na wadau ni pamoja na kuwafunga visukuma mawimbi tembo watatu ambao ni viongozi wa makundi na hivyo kufuatilia mienendo yao ili kuwadhibiti kabla hawajafika katika makazi ya binadamu.

Mhifadhi Mkuu Linus Chuwa ameongeza kusema kuwa, TAWA imepeleka askari wa wanyamapori wa vijiji 41 (VGS,) katika chuo cha Likuyu Sekamaganga kwa ajili ya kupatiwa elimu ya kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu, ambapo askari hao hutumiwa na TAWA katika matukio mbalimbali ya kudhibiti wanyamapori.

Kwa upande wake, Afisa Habari wa TAWA, Beatus Maganja amesema lengo kuu la ziara hiyo mkoani Lindi ni kuelezea jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali kupitia TAWA katika kukabiliana na wanyamapori wakali na waharibifu na kuwahakikishia wananchi kuwa, taasisi hiyo iko kazini kuhakikisha inafanya kila iwezalo kuwadhibiti wanyamapori hao kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo TAWIRI, GIZ na TANAPA.

Mhifadhi Mkuu Kitengo cha Oparesheni, Linus Chuwa

Afisa Habari wa TAWA, Beatus Maganja




No comments