Header Ads

ad

Breaking News

SEKTA BINAFSI YASIFU UTEKELEZAJI WA MKUMBI

Katibu Mkuu Kiongozi Dkt. Moses Kusiluka

Na Mwandishi Wetu

SERIKAL imepongezwa kwa utekelezaji wa mapendekezo ya sekta binafsi kupitia vikao na mikutano ya Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) ambapo sekta binafsi imekiri kupatikana kwa mafanikio makubwa Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara (Mkumbi) ndani ya kipindi cha miaka mitatu ya utawala wa Rais Samia Suluhu Hassan.

Akizungumza mara baada ya kikao cha 37 cha Kamati Tendaji cha TNBC jana, Katibu Mkuu Kiongozi ambaye pia ni Mwenyekiti wa kamati hiyo, Dkt. Moses Kusiluka amesema sekta binafsi imeridhishwa na hatua mbalimbali zilizochukuliwa na serikali ya awamu ya sita katika kuboresha na kuweka mazingira na wezeshi ya uwezeshaji na ufanyaji biashara hapa nchini.

“Ni faraja kwetu kupata mrejesho chanya kutoka sekta binafsi kwani inaleta afya sambamba na kuonyesha dhamira ya kweli kuwa serikali ya awamu ya sita imedhamiria kuleta mageuzi ya kiuchumi sambamba na kuboresha mazingira ya kufanya biashara na kuvutia uwekezaji,” amesema Dkt. Kusiluka.

Mwenyekiti huyo amesema serikali imeshaondoa tozo mbalimbali ambazo zilikuwa kero kwa ustawi na ukuaji wa biashara hapa nchini kwa hayo yote ni matunda ya kazi ya Baraza la Taifa la Biashara.

Aidha, Dkt. Kusiluka amelipongeza Baraza kwa kazi nzuri wanayoifanya ikiwemo kusimamia na kuhakikisha vikundi kazi vyake ambavyo makatibu wakuu ndiyo wenyeviti wa vikundi kazi hivyo.

Amesema vikundi kazi vimefanya kazi nzuri ikiwemo kujadiliana na hatimaye kuja na mapendekezo yanayowasilishwa kwenye kikao cha kamati tendaji kabla ya kupelekwa kwenye mkutano wa Baraza mwishoni mwa mwezi mei au Juni mwanzoni ambapo Rais ndiye mwenyekiti wake.

“Miaka mitatu ya uongozi wa Awamu ya Sita chini ya Rais Samia imeweza kuboresha na kuimarisha mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji nchini ikiwemo kuchochea ukuaji wa sekta binafsi,” alisema Dkt. Kusiluka.

Naye, Mwenyekiti Mwenza ambaye pia ni Mwenyekiti wa Sekta Binafsi nchini (TPSF), Angelina Ngalula ameipongeza serikali kwa kufanya maboresho makubwa na kufanikishwa utekelezaji Mkumbi.

”Serikali inapaswa kuendelea kutoa elimu zaidi kwa umma na wadau mbalimbali ili waweze kuelewa namna Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara (Mkumbi) unavyofanya kazi kwani utasaidia kuondoa mkanganyiko baina ya wafanyabiashara na sekta ya umma,” alisisitiza Ngalula.

Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa TNBC, Dkt. Godwill Wanga amesema kuwa kikao hicho kimeangazia zaidi utekelezaji wa maazimio ya kikao cha 36 cha kamati tendaji ambapo jitihada kubwa zimechukuliwa katika utekelazaji wa maazimio hayo yenye lengo la kuboresha mazingira ya ufanyaji biashara nchini.

Aidha Dkt. Wanga amesema moja ya ajenda kubwa iliyojadiliwa ni pamoja na kuunganisha mifumo ya serikali ili weze kusomana na hivyo kujenga uchumi wa kidijiti utakao chochea na kuongeza tija katika uzalishaji na utoaji huduma nchini.

“Mapinduzi ya uchumi wa kidijiti utatoa mchango mkubwa katika kukuza pato la mwananchi mmoja mmoja na taifa kiujumla sambamba na kuchagiza maendeleo na ukuaji wa sekta nyingine za maendeleo na uchumi,” amesema Dkt. Wanga.

Dkt. Wanga amesema kikao hiko kimeelekeza maswala yote ya udhibiti yahakikishe yanadhibiti zaidi changamoto kuliko kuwadhibiti wazalishaji ili kutoathiri ukuaji wa uchumi sambamba na kufanya kazi kwa karibu na sekta binafsi ili iweze kuzalisha na kuchangia kikamilifu katika kukuza pato la Taifa.


No comments