Header Ads

ad

Breaking News

OSHA, WAHARIRI KUSHIRIKIANA KUELIMISHA WAAJIRI, WAFANYAKAZI KANUNI ZA USALAMA KAZINI

MKuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambuke akizungumza katika semina iliyoandaliwa na Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSHA), kwa wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari

Mwandishi Wetu

WAKALA wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSHA), umewataka wahariri wa vyombo vya habari nchini kutumia nafasi zao kuwaelimisha waajiri na wafanyakazi kuzingatia kanuni bora za usalama na afya katika sehemu za kazi ili kupunguza ajali, magonjwa na vifo vinavyoweza kusababishwa na vihatarishi vya usalama na afya mahali pa kazi.

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule amayesame hayo alipofungua semina kuhusu usalama na afya kazini iliyoandaliwa na OSHA kwa wahariri wa vyombo mbali mbali vya habari nchini iliyifanyika Alhamisi Aprili 19,2024 jijini Dar es Salaam.

Amesema Serikali ya Awamu ya Sita imekuwa ikifanya jitihada kubwa kuhamasisha uwekezaji nchini, hivyo shughuli nyingi za kiuchumi zimekuwa zikianzishwa na wawekezaji wa ndani na nje ya nchi, hivyo wahusika katika uzalishaji wanatakiwa kuwa na uelewa wa kutosha wa masuala ya afya na usalama kazini.

Mkuu wa wilaya huyo amesema uchumi wa nchi unakua kwa kasi na uwekezaji unaongezeka kila kukicha, akitolea mfano Wilaya ya Kinondoni anayoiongoza kuwa na zaidi ya viwanda 150 pamoja na shughuli nyingine za kiuchumi zinazoajiri watanzania wengi.

"Uchumi wetu unazidi kukua kwa kasi sana, uwekezaji unaongezeka mfano wilaya ninayoiongoza ya Kinondoni tuna viwanda zaidi ya 150 na shughuli nyingine za kiuchumi zinafanyika, vyote hivyo vimetoa ajira kwa watanzania wengi sana," amesema Mkuu wa Wilaya, Saad Mtambule.

Hivyo, unaweza kuona ni kwa jinsi gani kuna umuhimu wa kuhakikisha sehemu za kazi zinakuwa na mifumo imara ya kulinda nguvukazi pamoja kuhakikisha kwamba waajiri na wafanyakazi wanakuwa na uelewa wa kutosha juu ya taratibu muhimu za usalama na afya mahali pa kazi,” ameeleza Mtambule na kuongeza:

Amesema OSHA inawahitaji wahariri kama wadau muhimu wa kufikisha elimu hiyo haraka zaidi kwa kuelimisha jamii ya waajiri na wafanyakazi, ndiyo maana wameandaa mafunzo hayo maalum huku akiwataka kuendelee kushirikiana na OSHA kuwaelimisha Watanzania masuala ya usalama na afya kazini.

Mkuu wa wilaya ameipongeza OSHA kwa kazi nzuri ya kusimamia utekelezaji wa Sheria Na. 5 ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi ya mwaka 2003 na kanuni zake, huku akiwataka watendaji wake kuendelea kufanya kazi kwa weledi na kuwachukulia hatua waajiri wote wanavunja sheria husika.

"Nawapongeza OSHA kwa kazi nzuri mnayoifanya, mnasimamia vizuri utekelezaji wa Sheria Na.5 na kanuni zake za Usalama na Afya Mahali pa Kazi ya mwaka 2003, nawaomba watendaji endeleeni kutekeleza majukumu yenu kwa weledi na kuhakikisha mnawabana waajiri wote wanaovunja sheria hizo," amesema Mkuu wa Wilaya, Mtambuke. 

Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda amesisitiza umuhimu wa kuzingatia masuala ya usalama na afya kwa wahariri wa vyombo vya habari wakati wa semina ya masuala ya usalama na Afya Mahali pa Kazi.

Mwenda amesema kuwa, mtu yeyote atakeyekiuka vifungu vya sheria hii au kanuni zake atakuwa ametenda kosa la jinai na ikibainika kutenda kosa hilo atawajibika kulipa faini au kifungo au vyote viwili.

Kwa upande wa watumishi, Mtendaji Mkuu huyo amesema wanatakiwa kutumia vifaa kinga wanavyopewa vya kulinda afya na usalama wake kazini na kutofanya mambo ambayo yanaweza kuhatarisha afya na usalama wake au wa wafanyakazi wengine kwenye eneo la kazi.

"Mwajili anatakiwa kuhakikisha afya, usalama na ustawi wa wafanyakazi kazini na urekebu wa wafanyakazi waliopata madhara, kufanya matengenezo ya mashine na mitambo ili iwe salama, kuhakikisha kutokuwepo kwa vihatarishi vya afya katika shughuli za uzalishaji, usindikaji, matumizi, utunzaji, uhifadhi na usafirishaji wa vitu hatarishi na kutoa maelekezo, mafunzo na usimamizi ili kuhakikisha afya na usalama wa wafanyakazi wake," amesema Mtendaji huyo.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSHA), Khadija Mwenda akifafanua jambo kwenye semina

Mkuu wa Kitengo cha Sheria Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSHA), Rehema Msekwa akitoa ufafanuzi wa masuala ya sheria
Mkuu wa Mafunzo wa Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSHA), Joshua  Matiko Mkurugenzi wa Mafunzo, Utafiti,Takwimu na Uhamasishaji

Wahariri wakiwa makini kusikiliza kwenye semina iliyoandaliwa na Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA)

Wakifuatilia 

Wakiwa makini kusikiliza

No comments