Header Ads

ad

Breaking News

MBUNGE DKT MABULA ‘ILEMELA TUMETENGA ZAIDI YA BILIONI 1.5 KWAAJILI YA MIKOPO’

 Dkt.Angeline Mabula, Mbunge wa Jimbo la Ilemela akizungumza na vikundi vya wanawake jimboni humo.

Na Mwandishi Wetu

ZAIDI shilingi bilioni 1.5 zimetengwa kwa ajili ya mikopo ya vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kutoka katika mapato ya ndani ya Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela jijini Mwanza.

Hayo yamesemwa na Mbunge wa Jimbo la Ilemela, Dkt.Angeline Mabula wakati akizungumza na kikundi cha Jumuiya ya Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT), tawi la Kigala, Buswelu katika ukumbi wa ofisi za CCM Kata ya Kirumba ikiwa ni mwendelezo wa ziara zake za kusikiliza kero za makundi mbalimbali ndani ya Jimbo lake, huku akiwataka kuchangamkia fursa ya uwepo wa mikopo hiyo kwa ajili ya kujikwamua kiuchumi.

"Nawapongeza kwa kuamua kujiunga katika kikundi , niwaombe mkisajili kikundi chenu ili muweze kunufaika na mikopo ya halmashauri, tumetenga fedha za kutosha kutoka kwenye mapato yetu ya ndani kwa ajili ya mikopo," amesema.

Dkt. Mabula mbali na kupokea pongezi za Rais Dkt. Samia Suluhu Hasan kwa kazi nzuri ya maendeleo anayoifanya kutoka kwa wanawake hao, ameahidi kuwachangia kiasi cha shilingi 700,000, lakini 500,000 kati ya hizo ni kwa ajili ya kutunisha mfuko wao wa kukopeshana kwa kuwaongezea mtaji.

Mbunge huyo amekagua uharibifu wa barabara ya kutoka Buswelu kupitia Kigala kufikia Buyombe.

Katibu wa kikundi hicho ambaye pia ni Katibu wa Jumuiya ya Wanawake Tanzania (CCM), tawi la Kigala, Janeth Sostenes Bida amewapongeza Dkt. Samia na Mbunge wa Jimbo la Ilemela Dkt. Angeline Mabula kwa kazi nzuri wanazozifanya.

Amesema kina mama hao watahakikisha wanamuunga mkono Dkt. Samia katika uchaguzi mkuu utakaofanyika mwakani, huku akimwomba mbunge huyo kuwafikishia salama zao kwa Rais Dkt. Samia kwa kazi kubwa anazozifanya, ikiwemo kutekeleza miradi inayogusa moja kwa moja wanawake kama miradi ya maji, zahanati, vituo vya afya na barabara za lami.

Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya CCM Kata ya Kirumba, Jackson Satta amesema anaridhishwa na kazi nzuri inayofanya na mbunge wao, huku akiwataka wananchi kumuunga mkono na kumwombea afya njema ili azidi kuwatumikia.

Naye, Katibu wa Ofisi ya Mbunge Jimbo la Ilemela, Charles Karoli David amewapongeza wanawake kwa kupata viongozi wanaotambua kero na changamoto za wanawake wenzao akiwemo Rais Dkt. Samia Suluhu Hasan na Mbunge Dkt. Angeline Mabula.

No comments