Header Ads

ad

Breaking News

JOWUTA YAANDAA MPANGO MKAKATI WA MIAKA MITATU

Kamati ya Utendaji ya Chama cha Wafanyakazi wa Vyombo vya Habari Tanzania (JOWUTA)


Mwandishi Wetu

CHAMA cha Wafanyakazi wa Vyombo vya Habari Tanzania (JOWUTA), kimekamilisha mpango mkakati wa kazi wa miaka mitatu ambao pamoja na mambo mengine unalenga kutetea haki za wafanyakazi kwenye vyombo vya habari nchini.

Wajumbe wa Kamati ya Utendaji wa JOWUTA wamekamilisha mpango kazi huo katika kikao ambacho kimefanyika Aprili 5,2024 katika Ofisi za JOWUTA jijini Dar es Salaam.

Katika kikao hicho kilichoongozwa na Mwenyekiti wa JOWUTA Taifa, Mussa Juma, JOWUTA kwa kushirikiana na mashirika ya kimataifa na taasisi za ndani, imejipanga kutoa elimu juu ya masuala ya haki za wafanyakazi, namna ya kusaini mikataba ya kazi na mikataba ya hali bora maeneo ya kazi kwa waandishi nchini.

Juma amesema mpango kazi huo unatarajiwa kuzinduliwa hivi karibuni na kwamba, wamejipanga kushirikiana na wadau wengine kutoa mafunzo kwa wanahabari juu ya kuandika habari za uchaguzi, Akili Bandia (Artificial Intelligence), ulinzi na usalama kwa wanahabari wakati wa kutekeleza majukumu yao.

"Tunaendelea kutafuta wadau ambao tutashirikiana nao kuhakikisha taaluma ya habari inaheshimika nchini, kwa wanahabari kulipwa vizuri, kuwa na mikataba ya kazi na kujua haki zao sehemu ya kazi," amesema

Awali, Katibu Mkuu wa JOWUTA, Suleiman Msuya amesema mpango kazi huo utasaidia kuonekana mchango wa wanahabari katika pato la Taifa kwani watakuwa wakilipa kodi mbalimbali baada ya kupata ajira ama mikataba bora.

"Kuna waandishi zaidi ya 10,000 nchini, wakipatiwa elimu ya masuala ya kazi na kuajiriwa ama kujiajiri serikali itanufaika kupitia makato ya mshahara, michango ya mifuko ya hifadhi ya jamii na kwingine,"amesema.

Naibu Katibu Mkuu wa JOWUTA, Said Mmanga na Mweka Hazina Lucy Ngowi wamewaomba wadau mbalimbali kuendelea kuiunga mkono JOWUTA, huku wakiwataka wanahabari na wafanyakazi katika vyombo vya habari kujiunga na chama hicho.

"Kwa mujibu wa sheria, JOWUTA ndiyo chama pekee chenye mamlaka ya kisheria kutetea na kupigania maslahi ya waandishi wa habari kwa njia ya mazungumzo hadi mahakamani, tunaomba waandishi wajiunge na chama hiki ili tuweze kusukuma mbele hili gurudumu kwa pamoja," amesema.

JOWUTA imesajiliwa na msajili wa vyama vya wafanyakazi nchini, hadi sasa ina zaidi ya wanachama 300 nchini nzima.

Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Vyombo vya Habari Tanzania (JOWUTA), Said Mmanga na Mweka Hazina Lucy Ngowi 

Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Vyombo vya Habari Tanzania (JOWUTA), Said Mmanga akifafanua jambo
Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Vyombo vya Habari Tanzania (JOWUTA), Mussa Juma (kulia), Katibu Mkuu wa chama hicho, Suleiman Msuya (katikati) na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Sophia Ngalapi
Wakiwa katika picha ya pamoja

No comments