Header Ads

ad

Breaking News

DKT. BITEKO AZUNGUMZIA UWEZESHWAJI VYOMBO VYA HABARI


Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko akifungua mkutano wa kitaaluma ulioandaliwa na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Jumatatu Aprili 29,2024 jijini Dodoma.

Na Mwandishi Wetu

NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko, amesema suala la uwezeshaji wa vyombo vya habari kiuchumi ni jambo muhimu kwa ukuaji na ustawi wa vyombo vya habari na sekta nzima ya habari kwa ujumla wake.  

Kauli hiyo ameitoa wakati akifungua Mkutano wa Kitaaluma wa 13 wa Jukwaa la Wahariri  Tanzania (TEF), Jumatatu Aprili 29,2024 jijini Dodoma, ambapo amesema anafahamu kuwa, bila matangazo, redio, televisheni, magazeti na mitandao ya kijamii inakuwa na kazi ngumu kuendelea kutoa huduma ya habari.

"Bila ya matangazo kwenye vyombo vya habari, uendeshaji wake unakuwa mgumu sana, ndiyo maana vyombo vingine vimeshindwa kujiendesha, hivyo vimefungwa," amesema Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati.

Dkt.Biteko amesema atamwomba Mhe. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na viongozi wakuu wa Serikali wazisihi Wizara na Taasisi za Umma zitenge bajeti ya kutosha kulipia gharama za matangazo pindi wanapotumia huduma hiyo kwa vyombo vya habari.

Amesema habari ni huduma si biashara, hivyo hakuna uwezekano wa kutengeneza faida kupitia vyombo vya habari, inatakiwa vyombo vya habari viwezeshwe kwa njia ya matangazo navyo visaidie kufikisha ujumbe kwa wananchi kwani husaidia kujenga taifa imara.

Kuhusu matangazo, baada ya mabadiliko ya Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2023, iliondoa kikwazo kilichokuwa kikitaka kila tangazo la serikali kupitia Idara ya Habari Maelezo, hatua ambayo ilifikiwa kwa maelekezo mahsusi ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na hatua zitakazofuata ni za kimanunuzi.

Amesema kuwa, ukianza utaratibu huo wataona jinsi gani vyombo vya habari vingi kadri inavyowezekana vinapata matangazo, lakini kwa kuzingatia taratibu zilizopo kisheria. 

Kuhusu Akili mnemba (AI) na Uchaguzi, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati,Biteko amesema suala la Artificial Intelligence-AI, ameliona linakuja kwa kasi kubwa, hivyo Tanzania hatupaswi kuachwa kama Watazamaji. 

"Naamini mbali na faida inayo madhara yake pia. Naagiza wizara ifanye uratibu mzuri wa suala hili la AI na kuhakikisha halileti madhara katika nchi yetu. Upo umhimu wa nchi yetu kuwa na sheria inayoongoza masuala ya AI, kwani kutegemea sheria mbadala haina uhakika zaidi," amesema. 

Dkt.Biteko amesema lipo tishio la kompyuta kuchukua kazi za binadamu, lakini pia ndani yake kuna fursa, hivyo waandishi wa habari wajifunze kompyuta, wapate maarifa ya jinsi ya kutumia AI kwani inarahisisha kazi na wasipoitumia, mjue wenzenu tayari wanaitumia.

Kuhusu maandalizi ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt.Biteko amesema taasisi zinazohusika zinaendelea kufanya maandalizi na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan amekwisema bayana kuwa, nchi yetu itakuwa na uchaguzi huru na wa haki.

Amesema ombi lao kwa wahariri ni kuhakikisha wanaandika habari za kweli, bila kutia chumvi, kuwa na upendeleo au uonevu kwa mtu au chama chochote cha siasa, kwani Watanzania wanafahamu chama kilichowaletea maendeleo na wanaendelea kuwa na uaminifu mkubwa kwake, hivyo watashindana kwa haki kabisa.

Ameongeza kuwa, Serikali ina imani na wahariri na waandishi wa habari mtapima kwa haki utendaji wa serikali iliyopo madarakani, mtapima ahadi zinazotolewa na kila upande na uwezekano wa kuzitekeleza na kuziwasilisha kwa Watanzania ili wazipime na kufanya uchaguzi sahihi kwa maendeleo endelevu ya taifa.

Amesema bila shaka chama kilichofanya vizuri kinafahamika na kitaendelea kufahamika.

"Serikali hatuna hofu yoyote, tunajua Mama Samia analiongoza vyema jahazi letu, anaupiga mwingi, na atalifikisha salama mwaloni, hivyo kila Mtanzania awe na amani, uchaguzi utakwenda vizuri kuliko wakati wowote," amesema.

Dkt.Biteko amesema wanafahamu nyakati za uchaguzi baadhi ya watu huwa na tamaa ya kuchezea taarifa na kusukuma habari ‘feki’ kupitia mitandao ya kijamii, hivyo amewataka wahariri na waandishi wa habari nchini kushirikiana kwa karibu na serikali, kuwafundisha vijana na watu wanaoifanya kazi hiyo kupitia mitandao bila kufahamu maadili ya uandishi wa habari.

Amewataka wahariri kuutumia vizuri mkutano huo kuona kama taaluma iko sawa sawa au imekumbwa na wavamizi wanaoitwa ‘Makanjanja’, wanaojipachika uandishi wa habari, wanapiga simu kwa watu mbalimbali na kudai fedha kwa vitisho kwamba, wasipopewa wanawalipua. 

"Mmetaja mitandao ya kijamii kuwa, inatumika vibaya na kuna uwezekano wa kuwapa mafunzo wahusika wakawa watoa taarifa wazuri kwa kufuata misingi ya kitaaluma. Sisi tunasema leteni hayo mapendekezo jinsi mtakavyoifanya kazi hii, na pale tulipo na uwezo tutaona jinsi ya kusaidiana kwa nia ya kukuza taaluma hii muhimu," amesema.

Dkt.Biteko amesema jambo la msingi katika kikao hicho, mchekeche kwa makini misingi ya taaluma, matakwa ya kisheria, maadili yenu katika jamii kama nchi, misingi taifa letu, umoja wetu, kuulinda Muungano wetu, kuendeleza siasa za kistaarabu, rasilimali za umma - kumulika kama wahusika wanazisimamia vizuri, bila kusahau ninyi wenyewe kujimulika iwapo mnaifanya kazi ya uhariri na uandishi wa habari kama inavyostahili.

Kwa hali yoyote iwayo, kimsingi mimi nawapongeza kwa mkutano huu mzuri na natarajia kupitia maazimio mtakayoyafikia, basi mtatushirikisha kama Serikali tuone wapi tunaweza kuchangia nini kufanikisha taaluma yenu ya habari ikawa bora zaidi.

Amesema kwa pamoja wanamshukuru Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan aliyeboresha uhuru wa vyombo vya habari nchini na kuwapa mazingira bora ya kufanya kazi waandishi wa habari, akiwataka wahariri kuungana kwa pamoja kumpogeza Rais kwa kuweka mazingira bora ya waandishi wa habari kufanya kazi bila vikwazo.

"Nimefurahishwa na kaulimbiu ya mkutano huu ambayo inasema; “Uandishi wa Habari Kuhamasisha Matumizi ya Gesi Kulinda Misitu,” kauli mbiu hii inabeba ujumbe unalolenga kuhamasisha matumizi ya gesi kwa kupikia, kwa lengo la kuokoa misitu yetu nchini. Tanzania inayo gesi ya kutosha."

Amesema wote wanafahamu kuwa, dunia imemchagua Rais Samia kuwa Kinara wa uhamasishaji matumizi ya nishati safi ya kupikia, ambayo ni gesi kwa Bara la Afrika.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, amesema kwa mabara mengine kama Ulaya, Amerika ya Kusini na Kaskazini na Asia, kwa muda mrefu wamekuwa wakitumia nishati ya gesi kwa ajili ya kupikia majumbani. 

Amesema kutokana na kutumia gesi, ndiyo maana mabara hayo kukata mti kwa ajili ya kuni au mkaa huchukuliwa kuwa ni uhalifu usiokubalika.

Amesema nchi za wenzetu hutumia gesi kwa ajili ya kupikia, mfumo wa joto katika nyumba zao katika kipindi cha majira ya baridi, na hutumika pia kuendeshea magari, hivyo Wizara ya Nishati wameandaa mpango kabambe wa kuhamasisha matumizi ya gesi nchini.

Ameongeza kuwa, wakati Rais Dkt. Samia anakwenda katika nchi nyingine za Afrika kuhamasisha matumizi ya gesi, inatakiwa nchi hizo zije kujifunza nchini. 

"Tayari tunao mpango na tumeanza kusambaza mitungi ya gesi hadi vijijini, tunataka mama wa kijijini atumie gesi, aachane kabisa na mahangaiko ya kutafuta kuni," amesema.

Amesema baadhi ya mikoa, moshi unaotokana na kuni umekuwa chanzo cha mauaji kwa kina mama wazee wanaokuwa na macho mekundu kwa sababu ya moshi huo, wakituhumiwa uchawi, hivyo wanaamini wakimuunga mkono vyema Rais Samia kuhamasisha matumizi ya gesi vizuri, wananchi watapata faida kubwa.

Dkt. Biteko amesema kuwa, zipo faida nyingi ukitumia gesi, ambazo kati yake kubwa ni ulinzi wa misitu, hivyo kuliepusha taifa na dunia na hatari ya jangwa, kwani kukata misitu, kunaharibu ardhi na takwimu zinaonesha kuwa, asilimia 16 ya ardhi ya nchi yetu imeharibiwa kutokana na ukataji miti holela.




No comments