Header Ads

ad

Breaking News

CSOs 44 ZAPEWA SHILINGI BILIONI 4

Mwakilishi mkaazi wa UNDP Shegeki Kamatsubara akimpongeza mkurugenzi wa MAIPAC Mussa Juma baada ya kisaini mkataba wa kupewa ruzuku


Mwandishi Wetu


MFUKO wa Mazingira Duniani (GEF) kupitia Programu ya Ruzuku Ndogo inayotekelezwa na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) limesaini makubaliano ya kutoa shilingi bilioni 4.04 kwa mashirika yasiyo ya kiserikali 44 nchini ili kutekeleza miradi ya uhifadhi wa mazingira, misitu, kuendeleza ufugaji nyuki, kutunza vyanzo vya maji na uwezeshaji jamii kiuchumi.

Utiaji saini wa makubaliano hayo umefanyika leo Aprili 4,2024, katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa (UN) nchini Tanzania na kuongozwa na Mwakilishi Mkaazi wa UNDP, Shigeki Komatsubara.

Miongoni mwa mashirika yaliyosaini mkataba kupatiwa fedha hizo ni Shirika la Wanahabari wa Jamii za Pembezoni (MAIPAC), Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (MJUMITA) ambao wamekuwa wakitekeleza miradi ya uhifadhi wa mazingira, misitu na vyanzo vya maji na kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

Akizungumza katika hafla hiyo, Komatsubara amesema mashirika zaidi ya 400 yalituma maombi kuomba fedha za kutekeleza miradi midogo midogo nchini Tanzania bara na Zanzibar lakini ni mashirika 44 tu ndio yamefanikiwa.

Komatsubara amesema anaimani kubwa mashirika ambayo yanapewa fedha hizo yatakwenda kutekeleza vyema miradi ambayo itagusa jamii hasa wanawake, vijana, walemavu wa jamii za pembezoni.

"Tunatarajia miradi mlioiandikia itakwenda kuchochea maendeleo katika jamii hasa kukabiliana na vichocheo vya uharibifu wa mazingira," amesema.

Naye, Mwakilishi wa Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Lilian Lukambuzi akizungumza katika hafla hiyo alitaka mashirika yaliyopewa fedha hizo kuzitumia kama ilivyokusudia.

Amesema serikali itafuatilia miradi ambayo inakwenda kutekelezwa ili kuhakikisha inakuwa na tija.

Awali, Mratibu wa Programu ya Ruzuku Ndogo za GEF nchini, Faustine Ninga amesema haikuwa kazi rahisi kupitisha mashirika hayo machache kupata ruzuku kutokana na uhitaji mkubwa kutoka katika maeneo mbalimbali nchini.

Amesema kamati ya uendeshaji ya programu hiyo ya ruzuku ndogo za GEF ambayo inaundwa na wataalam kutoka sekta mbalimbali na taasis zisizo za kiserikali kwa kushirikia na UNDP ilifanya kazi kubwa ya kuchambua maandiko ya miradi zaidi ya 400.

Hata hivyo, amesema kutokana na uhitaji kuwa mkubwa ni mashirika 44 tu ndiyo yalipitishwa, pamoja na mashirika mengine kuwa na madokezo mazuri ya miradi.

Hata hivyo ameyataka mashirika hayo kufuata kanuni, taratibu za nchi na miongozo ya uendeshaji wa taasisi zisizo za kiserikali katika utekelezaji wa miradi yao ili miradi iwe na matokeo mazuri.

Amesema kamati ya ufuatiliaji wa miradi itakagua na kufuatilia kwa karibu utekelezaji ili kuhakikisha jamii zinanufaika .

Wakizungumza baada ya kusaini mikataba baadhi ya watendaji wa mashirika hayo walipongeza UNDP kwa kuendelea kutoa fedha za kutekeleza miradi midogo katika jamii.

Mkurugenzi wa Shirika la MAIPAC, Mussa Juma amesema hii ni mara ya pili shirika hilo kupata fedha na kueleza katika miradi iliyopita kulikuwa na matokeo mazuri.

"Tulikusanya maarifa ya asili katika uhifadhi mazingira, misitu na vyanzo vya maji na kufanikiwa kutengeneza kitabu cha kwanza nchini cha umuhimu wa maarifa ya asili ambacho kilizinduliwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira na Muungano, Dkt. Seleman Jafo na kugawanywa bure katika shule, taasisi za serikali na binafsi,"alisema.

Amesema pia waliweza kushirikisha watungaji wa sera kutambu umuhimu wa kulinda na kuendeleza maarifa ya asili ikiwepo kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

"Safari hii maarifa ya asili yatakusanywa na kuhifadhiwa katoka kwenye vitabu na katika vyombo vya habari kwa jamii ya Wahdzabe na Waberbeig lakini pia vyanzo vya maji vitahifadhiwa," amesema.

Clara Chuwa, Mratibu Miradi wa Shirika la WODSTA amesema wanakwenda kutekeleza Mradi wa Kutunza Mazingira na Matumizi Endelevu ya Msitu na Chanzo Cha Maji kijiji cha Lemanda, Kata ya Oldonyosambu, Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la SECCA, Esaya Yusufu amesema wanakwenda kutekeleza mradi wa upandaji miti na kuchimba kisima katika eneo la ikolojia ya Serengeti.

Mfuko wa mazingira Duniani (GEF) ulianzishwa mwaka 1992 na umekuwa na miradi katika nchi 136 Duniani.

Mkurugenzi wa Shirika la MAIPAC, Mussa Juma

No comments