Header Ads

ad

Breaking News

TCB YAPATA FAIDA, WATEJA WAJAWA NA IMANI

Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Biashara Tanzania (TCB), Adam Charles Mihayo, akitoa wasilisho kwa wahariri na waandishi wa habari leo Jumanne Aprili 9,2024 jijini Dar es Salaam

Na Frank Balile

AFISA Mtendaji Mkuu wa Tanzania Commercial Bank (TCB), Adam Charles Mihayo, amesema benki hiyo imepata ongezeko la faida ya shilingi bilioni 10.7, baada ya makato ya kodi kwa kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka ambayo kilichoishia Machi 31, 2024. 

Akizungumza katika kikao kazi kilichowakutanisha wahariri na waandishi wa habari kwa usimamizi wa Ofisi ya Msajili wa Hazina, Mihayo amesema kuwa, benki hiyo inaamini ongezeko hili la asilimia 358 katika mapato yake kipindi cha robo ya kwanza yametokana na ukuaji mkubwa wa mapato katika aina zake zote za biashara na ongezeko kubwa la kitabu cha mizania katika kipindi hicho.

"Ongezeko hili la asilimia 358, katika mapato ya kipindi cha robo ya kwanza yametokana na ukuaji mkubwa wa mapato katika aina zote za biashara na ongezeko kubwa la kitabu cha mizania katika kipindi hicho," amesema Ofisa Mtendaji Mkuu huyo.

Mihayo amesema mapato hayo yaliongezeka kwa asilimia 30 hadi kufikia shilingi bilioni 56.8, yakiimarishwa na kitabu cha mizania na kasi kubwa ya ukuaji katika mapato yote.Mafanikio hayo yamepatikana chini ya uongozi wa Rais wa awamu ya Sita, Dkt.Samia Suluhu Hassan.

Amesema kuwa, amana za wateja zimeongezeka kwa asilimia 12 na kufikia shilingi trilioni 1.1 ikionesha imani kubwa ya wateja kwa benki hiyo, huku mikopo kwa wateja imepanda kwa asilimia 15.4 na kufikia shilingi bilioni 983.6 hadi Machi 31, 2024.

Ofisa Mtendaji huyo amesem hali hiyo inaonesha dhamira ya benki katika kuwezesha ukuaji wa uchumi na maendeleo ya watu wake.

“Ninajivunia kuwatangazia utendaji wetu wa kipekee katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka 2024, dhamira yetu kubwa ni kuleta ufanisi na kumridhisha mteja, hasa kwa kuwasikiliza wateja wetu na kuweka juhudi katika kuelewa mahitaji yao,” amesema Mihayo.

Ameongeza kuwa, ongezeko la mapato kwa asilimia 30 umeadhihirishia ujasiri wao na uwezo wa kulikabili soko linalokua kwa kasi.

Mihayo amesema kwamba, wateja wao wana imani kubwa na benki hiyo kama inavyothibitishwa na ongezeko la amana ya wateja, ambapo dhamira yao katika kuimarisha ukuaji wa uchumi inadhihirika wazi katika ongezeko la mikopo kwa wateja wetu. 

"Jumla ya gharama kulingana na kipato katika robo hii ya kwanza ni shilingi bilioni 43.2 ambazo ni sawa na ongezeko la asilimia 6.1 ukilinganisha shilingi bilioni 40.7 ya robo ya kwanza ya mwaka jana 2023," amesema Ofisa Mtendaji Mkuu huyo.

Mihayo ameongeza kuwa, jumla ya gharama za uendeshaji imepanda kutoka shilingi bilioni 26.5  mwishoni mwa robo ya kwanza ya mwaka 2023 hadi kufikia shilingi bilioni 26.8 mwishoni mwa robo ya kwanza ya mwaka 2024.

Amesema TCB hutumia njia ya kidijitali katika kufanya ufumbuzi wa kibenki, hivyo kuwapa wateja ufanisi, urahisi na uwezo wa kufanya shughuli za kimiamala. 

Ameongeza kuwa, mwelekeo huo unaimarishwa na mkakati wa kidijitali unaoendelea, ambao umeiwezesha benki hiyo kuwa karibu zaidi na wateja wake kuliko awali na kuwaruhusu kuendelea kujipatia huduma za kibenki katika sehemu zinazowapendeza wao na kuimarisha uhusiano wa kuaminiana kati ya benki na wateja wake.

Kuhusu mawakala, Mihayo amesema mtandao wa mawakala wa kibenki wa TCB Benki umekua mara nne katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, ambapo mwaka 2020 walikuwa mawakala 1,584, lakini kwa mwaka 2023 walikuwa mawakala zaidi ya 6,000.

"Mashine za UmojaSwitch za ATM zimeongezeka kutoka 250 kwa mwaka 2020 na kufikia mashine 281 kwa mwaka 2023, huku tukitoa kadi za VISA," amesema.

UmojaSwitch imeingia ubia na NMB Benki na katika robo ya kwanza ya mwaka 2024, tayari kuna mashine za ATM 750 za NMB ambazo zimeunganishwa na ATM za UmojaSwitch, na kuwa jumla ya mashine za ATM za UmojaSwitch kufikia 1,031 katika robo ya kwanza ya mwaka 2024.

Afisa Mtendaji Mkuu huyo amesema TCB imeanzisha M-Koba ambayo imeendelea kuaminika kwa wateja wao, huku akiwa na matumaini ya kuendelea kutoa bidhaa zitakazowalenga wateja na kuvunja rekodi kwa kipindi chote cha mwaka 2024 na kuendelea.

Tanzania Commercial Bank (TCB), ni taasisi ya kifedha ya Tanzania, ambayo imejikita katika kutoka suluhisho la kifedha. Ikiwa na historia pana na uwajibikaji katika kumridhisha mteja, TCB Benki imedhamiria kuwa benki pendwa zaidi na rafiki kwa wateja nchini Tanzania.

Matarajio yetu ni kusonga mbele na mikakati kusudiwa ili kupeleka mbele ukuaji wa Taasisi ya kifedha nchini Tanzania na kuwa taasisi inayoongoza nchini, kwa kutoa huduma ya viwango vya juu kwa wateja wetu na thamani isiyofikika. 

Tanzania Commercial Bank imeidhinishwa na inasimamamiwa na Benki Kuu ya Tanzania katika kutoa huduma za kifedha mbalimbali kwa kampuni, biashara ndogondogo na za kati, na kwa watu binafsi.

 Mkurugenzi wa Fedha wa Benki ya Biashara Tanzania (TCB), Regina Semakafu, akifafanua jambo kwenye kikao kazi hicho
Mkurugenzi wa Masoko na Maendeleo ya Biashara, Deo Kwiyuka akizungumza katika kikao kazi
Afisa Habari na Mawasiliano Mwandamizi Ofisi ya Msajili wa Hazina, Sabato Kusuri akifafanua jambo katika kikao kazi kilichowakutanisha Benki ya Biashara ya Tanzania (TCB), wahariri na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam chini ya usimamizi wa Ofisi ya Msajili wa Hazina
Maofisa wa Benki  ya Biashara Tanzania (TCB), wakifuatilia kwa makini
Wahariri na waandishi wa habari akisikiliza kwa makini
Wahariri na waandishi wa habari akisikiliza kwa makini
Wahariri na waandishi wa habari wakifuatilia wasilisho kutoka kwa Afisa Mtendaji Mkuu wa TCB, Adam Mihayo (hayupo pichani)


No comments