Header Ads

ad

Breaking News

WATU 447 WAPIMWA MOYO KAGERA

 Mtafiti wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Saadi Kamtoi akimwelekeza Afisa Uuguzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Bukoba (BRRH) Jenny Ndimuhela namna ya kujaza dodoso la kuwatambua wagonjwa wa moyo wakati wa kambi maalumu ya siku tano ya uchunguzi na matibabu ya moyo iliyomalizika hivi karibuni mkoani Kagera.   


Na Mwandishi Maalumu, Kagera

JUMLA ya watu 447 wakiwemo watu wazima 405 na watoto 42 wamepata huduma ya upimaji na matibabu ya moyo katika kambi maalumu ya matibabu iliyomalizika hivi karibuni mkoani Kagera.

Kambi hiyo ya siku tano ilifanywa na wataalamu wa magonjwa ya moyo kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Bukoba (BRRH).

Akizungumzia kuhusu kambi hiyo daktari bingwa wa magonjwa ya moyo wa JKCI, Yona Gandye alisema kwa upande wa watu wazima zaidi ya asilimia 95 ya watu waliowafanyiwa vipimo waliwakuta na tatizo la shinikizo la juu la damu.

“Baadhi ya hawa tuliowakuta na tatizo la shinikizo la damu walikuwa na matatizo mengine ya moyo ikiwemo moyo kutanuka, uwezo wa moyo kusukuma damu kuwa chini na wengine walikuwa na shida katika utengenezaji wa mapigo ya moyo na hivyo mapigo yao ya moyo kuwa chini kuliko kawaida.”

“Watoto tuliowapima baadhi yao tumewakuta na matatizo ya moyo ya kuzaliwa nayo ambayo ni matundu kwenye moyo na mishipa ya dam,” alisema Dkt. Gandye.

Dkt. Gandye alisema wagonjwa 55 wakiwemo watu wazima 50 na watoto watano ambao wamekutwa na matatizo ya moyo yaliyohitaji matibabu ya kibingwa wamepewa rufaa ya kwenda kutibiwa katika Taasisi hiyo.

“Tunashukuru kambi hii imeenda vizuri kwani uitikio kutoka kwa wananchi ulikuwa mkubwa na tumeweza kubadilishana ujuzi wa kazi na wenzetu wa BRRH ambao wataendelea kutoa huduma za matibabu ya moyo hata baada ya sisi kuondoka,” alisema Dkt. Gandye.

Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa - Bukoba Dkt.Museleta Nyakiroto aliishukuru JKCI kwa kufanya kambi hiyo na kusema kuwa licha ya wananchi kupata huduma ya kibingwa ya matibabu ya moyo lakini mewajengea uwezo wataalamu wa BRRH katika kutoa tiba ya magonjwa ya moyo.

Dkt. Nyakiroto alisema wananchi wataendelea kupata huduma za matibabu ya moyo katika hospitali hiyo kwani wataalamu wa BRRH wamejifunza kwa vitendo kutoka kwa wenzo wa JKCI na kama itatokea kuna mgonjwa ambaye atakuwa na tatizo litakalohitaji matibabu ya kibingwa watamtuma JKCI au Hospitali ya Kanda Bugando kwaajili ya kupata huduma zaidi.

“Tutaendeleza uhusiano uliopo baina ya JKCI na BRRH na ninatarajia upimaji wa aina hii ufanyike zaidi ya mara moja kwa mwaka kwani wagonjwa ni wengi wanaohitaji matibabu ya kibingwa ya moyo.”

“Nimejifunza wenzetu wa JKCI kila mgonjwa wanayemuona anapita kwa wataalamu wa lishe kupata ushauri nasi hapa tunawataalamu wa lishe, tutaboresha huduma na kuhakikisha wagonjwa wetu wanapita kwa wataalamu wa lishe ili kupata huduma ya ushauri wa lishe bora ambayo itawasaidia kuepukana na magonjwa yasiyoambukiza,” alisema Dkt. Nyakiroto.

Nao wataalamu wa afya kutoka BRRH ambao walikuwa wanafanya kazi pamoja na wenzao wa JKCI walisema kambi hiyo imewajengea uwezo wa jinsi ya kuwatambua na kuwatibu wagonjwa wa moyo na kufahamu mgonjwa ampe huduma ipi na kwa wakati gani.

“Nimejifunza mambo mengi ikiwemo jinsi ya kuwatambua wagonjwa wa moyo kabla hawajafika katika hatua mbaya na jinsi ya kuwatibu, kufanya vipimo vya kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi pamoja na mfumo wa umeme wa moyo na upimaji huu naweza kuufanya kwa mgonjwa yupi na kwa wakati gani,” alisema Dkt. Milton Kabiligi wa BRRH.

Wananchi waliopata huduma za uchunguzi na matibabu ya moyo katika kambi hiyo waliishukuru Serikali kwa huduma hiyo na kusema kuwa imewapunguzia gharama ya kusafiri na kuifuata jijini Dar es Salaam ambako ni mbali na mkoa wa Kagera. 

“Huduma ni nzuri na nimeridhika nayo, kwa muda mfupi niliofika hapa nimepata huduma zote zikiwemo za vipimo na ushauri ninawasihi wenzangu zinapotokea nafasi kama hizi wazitumie vizuri kwa kujitokeza kupima magonjwa mbalimbali,” alisema Erick Byabato mkazi wa Misenyi.

“Nimepima vipimo vyote vya moyo nimekutwa sina tatizo, shida niliyonayo ni uzito mkubwa nimeonana na mtaalamu wa lishe ambaye amenielekeza jinsi ya kula vyakula bora ambavyo vitanisaidia kutokupata magonjwa ya moyo pia amenisisitiza



umuhimu wa kufanya mazoezi ambayo yatanisaidia kupunguza uzito,” alisema Restituta Barungi mkazi wa Bukoba.

Afisa Uuguzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Bukoba (BRRH) Ernest Lengesela akimpima kipimo cha kuangalia shinikizo la damu mwilini mwananchi aliyefika katika hospitali hiyo kwa ajili ya kupata huduma za matibabu ya moyo wakati wa kambi maalumu ya upimaji iliyofanywa na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao wa BRRH.

Daktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Janeth Mmari na mwenzake wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Bukoba (BRRH) Martin Rwabilimbo wakimsikiliza mwananchi aliyefika BBRH kwaajili ya kupata huduma ya matibabu ya moyo wakati wa kambi maalumu ya siku tano ya uchunguzi na matibabu iliyomalizika hivi karibuni mkoani Kagera.
Wataalamu wa Taaasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na wenzao wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Bukoba (BRRH) wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kumalizkia kwa kambi maalum ya upimaji na matibabu ya moyo iliyofanyika mkoani Kagera. Jumla ya watu 447 wakiwemo watu wazima 405 na watoto 42 walifanyiwa uchunguzi wa moyo katika kambi hiyo. Picha zote na JKCI

No comments