Header Ads

ad

Breaking News

WATOTO MARUFUKU KUSHIRIKI MICHEZO YA KUBAHATISHA-MBALWE

Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha (GBT), James Mbalwe akizungumza katika kikao kazi na wahariri na waandishi wa habari, leo Machi 6,2024 jijini Dar es Salaam.


Na Mwandishi Wetu

BODI ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT), imesema katika kipindi cha mwaka 2022/2023 imechangia zaidi ya shilingi bilioni 170, katika pato la Taifa ilizotokana na kodi, huku akionya waendesha michezo hiyo kuwaruhusu watoto wenye umri chini ya miaka 18.

Akizungumza jijini Dar es Salaam leo Machi 6,2024, Mkurugenzi Mkuu wa GBT, James Mbalwe, amesema kuwa kodi hiyo imeongezeka kutoka shilingi bilioni 33.6 kwa mwaka 2016/17, hadi kufikia shilingi bilioni 170 kwa mwaka 2022/2023, kiasi hicho ni wastani wa ongezeko la asilimia 407 kwa mwaka katika kipindi hicho.

Mkurugenzi Mkuu huyo aliyazungumza hayo katika katika kikao kazi kati ya jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) na Bodi hiyo chini ya usimamizi wa Ofisi ya Msajili wa Hazina, ambapo vikao kazi hivyo ni mwendelezo wa taasisi na mashirika yaliyo chini ya ofisi hiyo kueleza shughuli mbalimbali wanazofanya.

Mbalwe amesema kuwa, sheria ya michezo hiyo inakataza watoto na vijana wenye umri chini ya miaka 18, kushiriki michezo ya kubahatisha, hivyo wanaoendesha michezo hiyo wakishindwa kuwadhibiti watachukuliwa hatua kazi za kisheria.

"Lengo la katazo hilo ni kuhakikisha tunawalinda watoto wadogo ili wasishiriki michezo hii ya kubahatisha, ukweli GBT tumesimamia katazo hili kikamilifu," amesema Mkurugenzi Mkuu wa GBT, ndugu Mbalwe.

Mkurugenzi Mkuu huyo amesema kuwa, baadhi ya waendeshaji wa michezo hiyo huwaruhusu watoto wenye umri chini ya miaka 18 kushiriki michezo hiyo kinyume na sheria na maadili ya jamii, hivyo hukiuka masharti ya leseni zao na taratibu zilizowekwa kisheria.

Hata hivyo, GBT katika kaguzi zake za mara kwa mara imekuwa ikiwabaini waendeshaji michezo hiyo, hasa wa mashine za sloti ambao wanaweka mashine zao kwenye maeneo yasiyosajiliwa na kuwachukulia hatua.

Mbalwe amesema jambo hilo ni kinyume cha sheria na linaharibu taswira ya michezo ya kubahatisha, huku akiweka wazi kwamba, kumekuwepo na mwingiliano wa mamlaka za serikali katika utoaji wa leseni/vibali vya kuendesha michezo ya kubahatisha kinyume na matakwa ya sheria inayosimamia michezo hiyo (Gaming Act,2003), ambayo imeipa jukumu hilo GBT pekee.

Akielezea michezo ya kubahatisha nchini, Mkurugenzi Mkuu huyo amesema ilikuwepo tangu enzi za mkoloni, kwenye miaka ya 1950 wakati huo ikitumika kama njia ya kukusanya pesa kwa ajili ya kuchangia huduma za kijamii kama ujenzi wa zahanati na shule.

Mbalwe amesema kabla ya kuanzishwa kwa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT), michezo hiyo ilikuwa ikisimamiwa na kuendeshwa na iliyokuwa Bahati Nasibu ya Taifa (BNT), ambayo ilikuwa ni msimamizi na mwendeshaji kwa wakati mmoja, hali iliyosababisha mgongano wa kimaslahi (Conflict of Interest).

Amesema wakati wa mageuzi ya kiuchumi yaliyotokea nchini kuanzia kwenye miaka ya 1980 hadi mwanzoni mwa miaka ya 2000, yaliweka uchumi huria ambao uliifanya sekta hiyo kupitia katika mabadiliko makubwa ambapo mwaka 2003,Sera ya Taifa ya Michezo ya Kubahatisha ilitungwa.

"Sera ilitaka kuwepo kwa Mamlaka ya kudhibiti michezo ya kubahatisha nchini kwa lengo la kuiwezesha sekta hii kuchangia pato la Taifa na kulinda maslahi na ustawi wa jamii, mageuzi hayo yakachangia kuanzishwa kwa GBT kwa lengo la kuiwezesha sekta ya michezo ya kubahatisha kuratibiwa vizuri na hivyo kuwa moja kati ya shughuli muhimu katika uchumi wa nchi na chanzo muhimu cha pato la Taifa." 

GBT ilianzishwa kwa Sheria ya Bunge Na. 4 ya 2003 (Gaming Act No. 4 of 2003) ambayo ilifuta Shirika la Bahati Nasibu ya Taifa (BNT) na kuanzisha Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT).



Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha (GBT), James Mbalwe akizungumza katika kikao kazi na wahariri na waandishi wa habari, leo Machi 6,2024 jijini Dar es Salaam.

Afisa Habari Mwandamizi wa Ofisi ya Msajili wa Hazina, Sabato Kosuri, akifafanua jambo wakati wa kikao kazi kati ya Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT) na wahariri chini ya usimamizi wa Ofisi ya Msajili wa Hazina  leo Machi 6,2024 jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodaus Balile, akitoa neno la shukrani

No comments