Header Ads

ad

Breaking News

THAMANI YA UWEKEZAJI YAONGEZEKA, YAFIKIA SHILINGI TRILIONI 76

 

Mkuu Idara ya Habari (Maelezo) na Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi, akizungumza na waandishi wa habari na wahariri Machi 24,jijini Dar es Salaam.

Na Mwandishi Wetu

MKURUGENZI Mkuu Idara ya Habari (Maelezo) na Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi amesema thamani ya uwekezaji  katika taasisi  zinazosimamiwa  na ofisi ya Msajili na Hazina imeongezeka kutoka shilingi trilioni 70 katika kipindi cha mwaka 2021 hadi kufikia shilingi trilioni 76 mwaka 2023, sawa na ongezeko la asilimia 8.6.

Matinyi ameyasemwa hayo Machi 24,2024 jijini Dar es Salaam, alipozungumza na wahariri na waandishi  wa habari, ambapo alisema Ofisi ya Msajili wa Hazina imeongeza makusanyo ya mapato yasiyo ya kodi  kutoka shilingi bilioni 637.66 hadi shilinghi trilioni 1.008 kwa mwaka 2023 sawa na ongezeko la asilimia 58.

Amesema sababu kubwa ya ongezeko hilo ni Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuongeza mitaji kwa kiasi cha shilingi trilioni 5.5 katika mashirika ya kimkakati kwa maslahi ya taifa. 

Matinyi amesema serikali imeongeza umiliki wa hisa katika Kampuni ya almasi ya Williamson Diamonds kutoka asilimia 25 hadi asilimia 37, huku ikisaini mikataba ya ubia wa asilimia 16 zisizohamishika katika Kampuni za madini. 

Amesema Wizara ya Madini katika kipindi cha kuanzia Machi 2024 hadi Februari 2024 imefanikiwa  kuiendeleza sekta kwa namna mbalimbali ikiwemo kukusanya maduhuli yatokanayo na ada mbalimbali, mirabaha, faini na penati na kufikisha kiasi cha shilingi trilioni 1.93. Awali, mwaka 2021/22 ilikuwa shilingi bilioni 591.5, lakini hadi kufikia mwaka 2023/24 imefikia shilingi bilioni 690.4.

Matinyi amesema kuwa, Tanzania imeendelea kuwa katika kundi la nchi zenye uchumi wa pato la kati ikimaanisha pato la wastani la kila mwanachi kwa mwaka (GNI per capital), ingawa mwaka 2019 ilikuwa kiasi cha dola 1,080 (sh. 2,743,813), lakini mwaka 2022 ni dola 1,200 (sh. 3,048,681). 

“Uchumi wa Tanzania umeendelea kukua licha ya athari kubwa za mripuko wa UVIKO-19 duniani pamoja na vita za Urusi na Ukraine na katika nchi za  Mashariki ya Kati, matatizo haya yaliutikisa uchumi wa dunia na Tanzania ambao ulikuwa umefikia wastani wa ukuaji wa zaidi ya asilimia 7 na kuushusha hadi asilimia 4.2 mwaka 2020," amesema.

"Hivi sasa ukuaji umefikia asilimia 5.2 kutokana na uongozi thabiti wa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt.Samia Sukuhu Hassan, Tanzania imeendelea kuwa katika kundi la nchi zenye uchumi wa pato la kati, ikimaanisha pato la wastani la kila mwanachi kwa mwaka (GNI per capital), ingawa mwaka 2019 ilikuwa kiasi cha dola 1,080 (sh. 2,743,813, lakini mwaka 2022 ni dola 1,200 (sh. 3,048,681)," amesema Matinyi.

Amesema serikali imeendelea kudhibiti mfumuko wa bei, ambapo kwa sasa ni chini ya asilimia 4, kiwango ambacho ni miongoni mwa viwango bora katika nchi za jumuiya za kikanda ambazo Tanzania ni mwanachama, kama Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Kuhusu kilimo, Msemaji Mkuu wa Serikali amesema kuwa, bajeti imeongezeka kutoka shilingi bilioni 294.16 mwaka 2021/2022 hadi kufikia shilingi bilioni shilingi bilioni 970.78 mwaka wa fedha 2023/2024," amesema Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi.

Amsema matumizi ya mbolea yameongezeka kutoka tani 320,233 kwa mwaka wa fedha 2020/21 hadi kufikia tani 580,628 kwa mwaka wa fedha 2022/23, ambapo bajeti ya maendeleo ya umwagiliaji imeongezeka kutoka shilingi bilioni 46.5 mwaka 2021/22 hadi shilingi bilioni 361.5 mwaka 2023/24.

"Wataalam wa kilimo 320 wameajiriwa na kusambazwa katika ofisi za umwagiliaji zilizopo katika wilaya 139, mitambo 15 na magari 53 vimenunuliwa kwa ajili ya shughuli za umwagiliaji," amesema.

Ameongeza kuwa, eneo la umwagiliaji limeongezeka kutoka hekta 694,715 mwaka 2020/2021 hadi hekta 727,280.6 mwaka 2022/2023, na kwamba serikali inaendelea kukamilisha ujenzi wa skimu za umwagiliaji zenye hekta 95,000 zilizoanza mwaka 2022/2023 pamoja na kuanza skimu mpya zenye ukubwa hekta 95,000 kwa mwaka 2023/2024, zikikamilika zitaongeza eneo la umwagiliaji kufikia hekta 917,280. 

Amesema programu ya Vijana ya Jenga Kesho Iliyo Bora (Build Better Tomorrow-BBT), mradi huo unashirikisha vijana 688, ambao wameanza kilimo biashara katika shamba la Chinangali II.

Mbali na kilimo, amezungumzia ufugaji na uvuvi katika kipindi cha miaka mitatu 2021/22 hadi mwaka 2023/24, amesema bajeti ya sekta ya mifugo imekuwa ikiongezeka kwa kasi kutoka shilingi 47,844,950,000/-mwaka 2021/22 hadi shilingi 112,046,777,000/- mwaka 2023/24.

Amesema katika kipindi cha miaka mitatu, 2021/22 hadi mwaka 2023/24, bajeti ya sekta ya uvuvi imepanda kutoka shilingi 121,350,046,999/- mwaka 2021/22 hadi shilingi 183,874,156,000 mwaka 2023/24.

Ameongeza kuwa, ili kuhakikisha serikali inarasimisha shughuli za uvuvi, kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Januari 30, 2024, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan, alizindua zoezi la ugawaji wa boti 160 na vizimba 222, kwa ajili ya makampuni, watu binafsi na vikundi vya wavuvi kupata vitendea kazi hivyo kwa njia ya mkopo usio na riba na kwasasa bandari ya uvuvi inajengwa Kilwa Masoko.

Wahariri wakifuatilia kwa makini
Wahariri wakifuatilia taarifa ya Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) na Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi (hayupo pichani), Machi 24, 2024 jijini Dar es Salaam
Mkuu Idara ya Habari (Maelezo) na Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi(aliyesimama mbele) , akizungumza na waandishi wa habari na wahariri Machi 24,jijini Dar es Salaam.

Mkuu Idara ya Habari (Maelezo) na Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi, akizungumza na waandishi wa habari na wahariri (hawapo pichani), Machi 24,jijini Dar es Salaam.

No comments