Header Ads

ad

Breaking News

TAWA YATOA GAWIO KWA HALMASHAURI 32, VIJIJI 187

Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Mabula Misungwi Nyanda, akielezea mafanikio ya mamlaka hiyo katika kipindi cha miaka mitatu ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan. 

Na Frank Balile

MAMLAKA ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), imesema baada ya mafanikio makubwa waliyopata kutokana na shughuli za utalii hasa utalii wa picha na uwindaji, TAWA imefanikiwa kutoa gawio kwa halmashauri za wilaya 32 na vijiji 187 katika kipindi cha mwaka 2021/22-2023/24.

Kwa mujibu wa Mhifadhi Mkuu wa TAWA, Mabula Misungwi Nyanda, amesema jumla ya shilingi bilioni 8.95 zilitolewa kwa wanufaika na kuimarisha mahusiano na dhana ya uhifadhi kwa wananchi wanaozunguka maeneo ya hifadhi. Kikao kazi hicho kimeratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina.

Nyanda amesema fedha hizo hutumika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo inayoibuliwa na  wananchi ikiwemo kuimarika kwa utalii jumuiya za hifadhi za wanyamapori

Amesema kuwa, mamlaka imekuwa ikisimamia na kurejesha stahili zinazotokana na shughuli za utalii katika maeneo ya Jumuiya za Uhifadhi za Wanyamapori, wakati mwaka 2021-2024 jumla ya shilingi bilioni 11.91 zilirejeshwa kwa Jumuiya ya Hifadhi za Wanyamapori 13 kwa ajili ya kuendeleza uhifadhi na miradi ya maendeleo kwa vijiji vilivyotoa ardhi yao kuwa hifadhi za wanyapori. 

Nyanda amesema kuwa, mafanikio yanayopatikana kwa sasa ni juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan, kutangaza utalii kupitia filamu ya the Royal Tour, kutoa fedha za kuendeleza miundombinu ya utalii na fursa za kutangaza katika masoko ya Kitaifa na Kimataifa, mafanikio mengi yamepatikana kama kuongezeka kwa watalii.

Mhifadhi mkuu huyo amesema kuwa, idadi ya watalii wa picha na uwindaji imeendela  kuongezeka kwa idadi ya watalii  wa picha waliotembelea vivutio kutoka 37,684 mwaka 2020/21 hadi 166,964 mwaka 2022/23 na watalii 116,529 hadi Februari 2024.

Amesema kuwa, idadi ya wawindaji imeongezeka kutoka 355 mwaka 2020/21 hadi 787 mwaka 2022/23, ambapo wawindaji 481 hadi Februari mwaka 2024 watakuwa wameondoka.

"Kuongezeka kwa idadi ya meli za kimataifa za utalii kutembelea eneo la kihistoria Kilwa kutoka meli nne, watalii 400 mwaka 2020/21 hadi meli nane zilizokuwa na watalii 925, imechangia kuongeza kwa watalii," amesema.

Nyanda amesema miongoni mwa matunda ya Filamu ya Royal Tour, ni mwitikio wa mkubwa  wa wawekezaji katika mnada wa vitalu vya utalii, ambapo jumla ya vitalu 66 vimeuzwa na mapato ya jumla ya dola za Marekani 8,277,000 zilikusanywa ikilinganishwa na dola 2,405,000, endapo vitalu hivyo vingeuzwa kwa njia ya utawala ingakuwa ni ongezeko la dola 5,872,000. 

Amesema kuwa, serikali ilikamilisha taratibu za uwekezaji kwa ajili ya kusaini mikataba ya uwekezaji mahiri katika vVitalu vya Ikorongo, Grumeti, Maswa Mbono, Maswa Kimani, Maswa North, Mkungunero na Selous LL1.

Mhifadhi Mkuu wa TAWA, amesema mikataba saba ilisainiwa Januari 2024, kwani kupitia mikataba hiyo serikali itapata dola za Marekani  milioni 312.25 kwa kipindi cha miaka 20, sawa na wastani wa dola za Marekani milioni 15.5.

Amesema kuwa, kufuatia juhudi hizo idadi ya vitalu uwindaji vyenye wawekezaji imeongezeka kutoka kutoka 59 hadi 68, ambapo kusainiwa na kuanza utelelezaji wa mikataba ya uwekezaji mahiri –SWICA,jumla ya dola za Marekani 2,773, 000 sawa na shilingi bilioni 7.01 zilikusanywa tangu kusainiwa kwa mikataba ya SWICA Januari 3, 2024.

Ameongeza kuwa, kuimarika kwa ukusanyaji wa maduhuli ya jumla kupitia vyanzo mbalimbali na kuchangia katika Mfuko Mkuu wa Serikali, jumla ya shillingi bilioni 184.74  zilikusanywa kati ya mwaka 2020/21 hadi 2024 Machi 8,2024.

Nyanda amesema kuwa, kwa kutumia fedha zilizotolewa kwa Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO 19, wameboresha miundombinu wezeshi ya utalii katika maeneo yanayosimamiwa na mamlaka, pamoja na miradi ya kujenga km 431.4 za barabara katika mapori ya Wamimbiki, Mpanga Kipengere, Igombe, Swagaswaga, Mkungunero, Kijereshi, Rungwa na Pande.

Ameongeza kuwa, ukarabati wa viwanja vya ndege vitatu katika Pori Tengefu la Lake Natron (Engaresero) na Pori la Akiba Maswa (Buturi na Mbono),kujenga  miundombinu ya kupumzika wageni  na hosteli moja katika mapori ya Akiba Mpanga Kipengere, Mkungunero, Lukwika Lumesule, Pande Swagaswaga na Magofu ya Kilwa.

  Amesema kuwa, fedha hizo zimesaidia ujenzi wa malango matano na vituo vinne vya kukusanyia mapato katika mapori ya Akiba ya Wamimbiki, Mkungunero, Lukwika Lumesule, Swagaswaga, Mpanga Kipengere, Kijereshi na katika Pori Tengefu Lake Natron.

"Fedha zile zimejenga njia ya waenda kwa miguu zenye urefu wa kilometa 3.7 katika Pori Tengefu Ziwa Natron na mapori ya Akiba Swagaswaga, Kilwa Kisiwani na Mpanga Kipengere, pia zimetumika kukarabati mabanda sita ya utalii katika Pori la Akiba Wamimbiki."

Mhifadhi Mkuu wa TAWA, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwaamini na kuwapatia fedha za kuboresha miundombinu ya utalii pamoja na kuboresha miundombinu ya uhifadhi na utalii.

Amesema kupitia bajeti ya mamlaka ya maendeleo na fedha zilizotolewa kwa Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO 19, TAWA imefanikiwa kujenga  maghala ya silaha 25, nyumba za watumishi 26, vituo 28 vya askari, ofisi 10 na Karakana nne kwa lengo la kuboresha mazingira ya utendaji kazi.

Mhifadhi mkuu huyo ameongeza kuwa, mamlaka imenunua vitendea kazi yakiwemo magari 60, boti za doria 7 na za utalii 2 zenye uwezo wa kubeba abiria 30 na 60, mahema, sare za watumishi, mtambo wa kuchimba visima, gari la kubeba mitambo, mtambo wa barabara (Grader), silaha , kuweka mifumo ya mawasiliano, radio za upepo na mfumo wa kukusanya taarifa za doria.

Nyanda amesema kuwa, mamlaka imejiimarisha katika matumizi ya mifumo ya TEHAMA katika ukusanyaji wa mapato kupitia mfumo wa MNRT Portal, uandaaji wa bajeti (PlanRep), matumizi (MUSE), kushughulikia majadala e-office, huduma kwa wateja na mfumo wa kukusanya taarifa za uhifadhi na mfumo wa kukusanya taarifa za doria.

Mhifadhi Mkuu wa TAWA, amesema kuwa, palipo na mafanikio changamoto hazikosekani, ikiwemo ongezeko la matukio ya wanyamapori wakali na waharibifu, uvamizi wa maeneo yaliyohifadhiwa kwa shughuli za kilimo  na mifugo na kampeni za kupinga uwindaji wa kitalii zinazoongozwa na asasi za kiraia hususan katika nchi ambazo ni masoko makubwa ya uwindaji.

Amesema wataendelea kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, kanuni, miongozo na maelekezo ya viongozi mbalimbali wa wizara na kitaifa, wataongeza ubunifu na mbinu mbalimbali kukabiliana na matukio ya wanyamapori wakali na waharibifu.

Nyanda amesema wataendelea kulinda rasilimali za wanyamapori na kuongeza mapato kwa kushirikiana na wadau na majukwaa ya Kimataifa kuelezea faida za uwindaji wa kitalii ili kukabiliana na kampeni za kupinga uwindaji.  

Wahariri na waandishi wa habari wakifuatilia wasilisho
Wahariri na waandishi wa habari wakisikiliza kwa makini
Maafisa wa TAWA wakifuatilia wasilisho

Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Mjukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Neville Meena akitoa neno la shukrani

No comments