Header Ads

ad

Breaking News

TANAPA YAANZA KUTANGAZA VIVUTIO VYA UTALII KIDIGITALI


Kamishna Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Mussa Juma Kuji,akizungumza katika kikao kazi na wahariri na waandishi wa habari kilichofanyika Machi 21, 2024 jijini Dar es Salaam. Kikao kazi hicho kimeratibiwa na Ofisa ya Msajili wa Hazina


Na Frank Balile

SHIRIKA la Hifadhi za Taifa (TANAPA), limeweka nguvu zake katika kuboresha mbinu za utangazaji wa vivutio vya utalii vilivyopo katika Hifadhi za Taifa kwa njia ya kidigitali ili kuwafikia walengwa wengi zaidi na kwa wakati mfupi. 

Kamishna Uhifadhi wa TANAPA, Mussa Juma Kuji, amesema miongoni mwa mikakati ya utangazaji wa vivutio kidigitali ni pamoja kuongeza idadi ya wafuatiliaji Katika mitandao ya kijamii.

Kauli hiyo ya Kamishna wa Uhifadhi, ameitoa ktika kikao kazi kilichowakutanisha wahariri na waandishi wa habari Machi 21,2024 jijini Dar es Salaam, kikiratibu na Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR), kwa lengo la kuhabarisha umma kazi zinazofanywa na taasisi mbalimbali za serikali.

TANAPA imefanikiwa kuongeza wafuatiliaji kwenye mitandao ya kijamii (facebook, Instagram, youtube, tiktok na twitter/X), kutoka watazamaji 1,327,000 kwa mwaka 2021 hadi kufikia watazamaji 8,960,000 katika mwaka 2024 na wafuatiliaji wa mitandao ya kijamii ya Shirika kutoka 62,000 mwaka 2021 hadi 1,014,000 mwaka 2024, hivyo inaonesha kufuatiliwa kwa shughuli zinazotekelezwa na Hifadhi za Taifa kila siku.

Amesema kuwa, usanifu wa taaarifa za majarida na vipeperushi katika mfumo wa 'Quick Reference' (QR Code)' umewezesha upatikanaji wa taarifa za Shirika na hifadhi kwa urahisi, kwa wakati, kwa lugha saba tofauti kwa wakati mmoja ambazo ni kiswahili, kingereza, kijerumani, kirusi, kichina, kifaransa na kispaniola, hivyo kupunguza matumizi ya karatasi.

Kamishna amesema kuwa, katika kipindi cha miaka mitatu, Shirika limeendelea kuboresha mahusiano na jamii zilizo jirani na hifadhi za Taifa katika shughuli za uhifadhi na utalii, ambapo ushirikiano huo umeleta faida mbalimbali ikiwemo kuibuliwa na kutekelezwa kwa miradi ya kijamii 'Support for Community Initiated Projects' (SCIPs).

Amesema kuwa, miradi 59 ya kijamii yenye thamani ya shilingi 30,785,819,981 ilitekelezwa katika kipindi cha miaka mitatu ambayo ni  ujenzi wa vyumba vya madarasa 20, mabweni 2, nyumba 7 pacha za walimu, zahanati 12, nyumba pacha za wauguzi 6, miradi ya maji 6, barabara 5 zenye urefu wa kilomita 76 na bwalo la chakula kwa wanafunzi 1 na ununuzi wa madawati 680. 

"Miradi hii imetekelezwa katika Wilaya za Ruangwa, Makete, Mbeya, Mbarali, Mpanda - Halmashauri ya Nsimbo, Uvinza, Kigoma, Muleba, Bariadi, Bunda, Serengeti, Mbulu, Arumeru, Rombo, Longido, Mwanga, Same, Korogwe, Lushoto, Pangani, Kilosa, Kilombero, Kilolo, Lindi na Ngorongoro (tarafa za Loliondo na Sale)," amesema Kamishna Kuji.

Ameongeza kuwa, ujenzi wa miradi hiyo umesaidia kupunguza kero kwa jamii na kuongeza usalama wa wanafunzi na kuwaboreshea mazingira ya kujifunzia na kuwapunguzia wananchi umbali wa kufuata huduma za kijamii ikiwemo huduma za afya na upatikanaji wa maji kwa matumizi ya binadamu na mifugo. 

Kamishna Kuji amesema kuwa, miradi hiyo imesaidia kuimarisha mahusiano mazuri kati ya jamii na hifadhi na kuifanya jamii kushiriki kikamilifu katika ulinzi wa Maliasili.

Amesema kuwa, jumla ya vikundi 138 vimewezeshwa katika miradi mbalimbali ya uzalishaji mali ikiwemo ufugaji wa nyuki, uchakataji wa viungo vya chakula na ufugaji, ambapo jumla ya shilingi billion 2.4 zilitumika kuwezesha miradi ya uzalishaji mali. 

Ameeleza kuwa, Benki za Kijamii za Uhifadhi 'Community Conservation Bank' (COCOBA) 159 zilianzishwa kupitia mradi wa REGROW na kupewa fedha mbegu kiasi cha shilingi 1,453,272,934, miradi hiyo imesaidia kuongeza wastani wa pato la wananchi katika maeneo husika na kupunguza utegemezi wa maliasili.

Kuhusu elimu, Kamishna Kuji amesema wanafunzi 1,051 kutoka vijiji 60 vinavyotekeleza mradi wa REGROW wamepatiwa ufadhili wa masomo wenye thamani ya shilingi 4,273,315,700 katika vyuo mbalimbali vya kitaaluma nchini, ufadhili ambao utaongeza kiwango cha uelewa kwenye jamii na kuongeza uwezo wa uzalishaji mali kwenye jamii husika.

"TANAPA kwa kushirikiana na Benki ya Ujerumani (KfW) na shirika lisilo la kiserikali la Frankfurt Zoological Society - FZS, imeendelea kuwezesha uandaaji wa mipango ya matumizi bora ya ardhi katika vijiji 57 vya wilaya za Serengeti, Morogoro, Kisarawe, Ulanga, Tunduru na Liwale na kutoa hati za kimila 16,243, kati ya hati hizo, hati 9,874 zilitolewa kwa jamii kwenye vijiji vinavyopakana na Hifadhi ya Taifa Nyerere na hati 6,612 zilitolewa kwa jamii ya vijiji vilivyopo wilayani Serengeti vinavyopakana na Hifadhi ya Taifa Serengeti," amesema.

Hata hivyo, Kamishna Kuji amesema wataendelea kuandaa hati za kimila kwenye wilaya za Bunda, Bariadi, Tarime, Meatu, Itilima na Busega, na kwamba uandaaji huu wa matumizi bora ya ardhi unasaidia kupunguza migogoro ya kimatumizi kati ya binadamu na wanyamapori kwenye maeneo husika na kuwajengea usalama katika umiliki wa ardhi kwa jamii zinazopakana na hifadhi.

Amesema kumekuwepo na ongezeko la idadi ya wananchi wanaofikiwa na elimu ya uhifadhi kutoka wananchi 169,245 kwa mwaka 2021/2022 hadi kufikia wananchi 211,986 katika mwaka wa fedha 2022/2023, wakati mwaka wa fedha 2023/2024 hadi kufikia Desemba 2023 wananchi 125,389 wamefikiwa na elimu ya uhifadhi. 

Kamishna Kuji amesema ongezeko hilo linatoa uhakika wa kuwa na wanajamii wanaoelewa masuala ya uhifadhi na hivyo, kuongeza uhakika wa ushiriki wa wananchi kwenye uhifadhi na ulinzi wa maliasili.

Katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia-nchi, Kamishna Kuji amesema TANAPA wamefungua vitalu na kugawa miche ya miti ya matunda, mbao na vivuli kwa wananchi, ambapo miche 209,690 imegawiwa kwa wananchi katika kipindi husika katika hifadhi za Kilimanjaro, Milima ya Udzungwa, Arusha, Serengeti na Burigi-Chato.

Afisa Uhifadhi Mkuu - TANAPA ambaye pia ni Mkuu wa Idara ya Mawasiliano, Catherine Mbena, akizungumza katika kikao kazi hicho.
Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Jully Lyimo akiwa kwenye kikao kazi hicho.

Naibu Kamishna wa Uhifadhi, Herman Batiho akiwa kwenye kikao kazi hicho.
Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Mhandisi Mshauri, Dkt. Richard John Matolo, akizungumza katika kikao kazi hicho.

Afisa Mwandamizi wa Habari na Mawasiliano Ofisi ya Msajili wa Hazina, Sabato Kosuri, akizungumza katika kikao kazi
Maofisa wa TANAPA wakifuatilia wasilisho
Baadhi ya wahariri wakisikiliza kwa makini wasilisho
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile akitoa neno la shukrani kwa viongozi wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) na waratibu wa kikao kazi hicho, Ofisi ya Msajili wa Hazina.

No comments