Header Ads

ad

Breaking News

TANAPA: SERIKALI IMETATUA MIGOGORO MINNE YA MUDA MREFU

Kamishna wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Mussa Juma Kuji, akizungumza na wahariri na waandishi wakati wa kikao kazi kilichofanyika Alhamisi Machi 21,2024 jijini Dar es Salaam.


Na Frank Balile

KAMISHNA wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Mussa Juma Kuji amesema Serikali imekamilisha utatuzi wa migogoro minne iliyodumu kwa muda mrefu kati ya vijiji na Hifadhi za Taifa Serengeti (vijiji 7 wilaya ya Serengeti), Arusha (Farm 40/41 - Wilaya ya Arumeru), Tarangire (Kimotorok - Wilaya ya Simanjiro) na Manyara (Buger - Wilaya ya Karatu).

Ameyasema hayo wakati wa kikao kazi kati ya TANAPA, wahariri na waandishi wa habari kilichofanyika Machi 21,2024 jijini Dar es Salaam.

Amesema serikali inaendelea kutatua migogoro na kufanya uthamini katika Hifadhi za Taifa za Ruaha (Ihefu), Milima ya Mahale (Vitongoji vya Kabukuyungu na Mahasa Kijiji cha Kalilani), Saadani (Kitongoji cha Uvinje), Mkomazi (Kitongoji cha Kimuni), Arusha (Kijiji cha Nasula) na Kitulo (Wilaya ya Rungwe).

"Jumla ya vigingi 905 vimejengwa katika Hifadhi za Taifa za Serengeti (184), Ruaha 671, Ziwa Manyara 18 na Tarangire 32, pamoja na kulima Mkuza wenye urefu wa kilometa 609 Tarangire - 242, Ruaha - 344 na Mikumi - 23 na kufuatia utatuzi wa migogoro iliyokuwepo.

Amesema serikali iko katika hatua za mwisho za kukamilisha ulipaji wa fidia kwa wananchi wa vijiji vya Nyatwali, Serengeti na Tamau ili kutwaa eneo la Ghuba ya Speke kuwa sehemu ya Hifadhi ya Taifa Serengeti.

"Serikali iko katika hatua za mwisho za kukamilisha ulipaji fidia kwa wananchi wa vijiji vitatu ambavyo ni Nyatwali, Serengeti na Tamau ili kutwaa eneo la Ghuba ya Speke kuwa sehemu ya Hifadhi ya Taifa Serengeti," amesema Kamishna Kuji.

Kuhusu wanyama pori wakali na waharibifu, Kamishna Kuji amesema Shirika limeendelea kukabiliana na kudhibiti changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu, ambapo limeshughulikia kwa wakati matukio 4,954 yaliyoripotiwa. 

Amesema Shirika limefunga visimbuzi kwa makundi 12 ya tembo, makundi 12 ya simba na makundi 5 ya mbwa mwitu katika Hifadhi za Mkomazi, Serengeti, Mikumi, Nyerere na Ruaha, ambapo ufungaji huo wa visimbuzi umesaidia ufuatiliaji wa karibu kwa makundi husika na kufanikiwa kutambua mienendo yao ili kurahisisha udhibiti wanapotoka nje ya maeneo ya hifadhi.

Kamishna Kuji amesema kuwa, kupitia mradi wa REGROW, Shirika limewezesha mafunzo kwa askari wa vijiji (Village Game Scout – VGS) 354 kutoka vijiji 39 ili kusaidia kukabili kwa wakati matukio ya wanyamapori wakali na waharibifu.

Amesema Shirika linaendelea na ujenzi wa vituo vinane vya Askari Uhifadhi katika maeneo ya kimkakati yaliyopo katika vijiji vinavyoathirika zaidi katika wilaya za Mbarali, Kalambo, Kilwa, Namtumbo, Ruangwa, Serengeti, Bunda na Bariadi, kwani itasaidia askari kudhibiti kwa wakati wanyamapori wakali na waharibifu.

Mkuu wa Kitengo cha Maendeleo na Biashara TANAPA, Jully Bede Lyimo

Naibu Kamishna wa Uhifadhi na Maendeleo ya Biashara TANAPA, Herman Batiho
Maofisa TANAPA wakisikiliza

Afisa Mwandamizi wa Habari na Mawasiliano Ofisi ya Msajili wa Hazina, Sabato Kosuri, akizungumza katika kikao kazi kati ya TANAPA, wahariri na waandishi wa habari Alhamisi Machi 21.2024 jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, akitoa neno la shukrani kwa TANAPA na wasimamizi wa kikao kazi, Ofisi ya Msajili wa Hazina.

Wahariri wakifuatilia wasilisho

Wahariri wakisikiliza kwa makini

No comments