Header Ads

ad

Breaking News

TANAPA: ROYAL TOUR IMEFUNGUA MILANGO YA UTALII, FURSA ZA UWEKEZAJI

Kamishna wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Mussa Juma Kuji akieleza mafanikio ya shirika hilo katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Awamu ya Sita wa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan, jana Alhamisi Machi 21,2024.

Na Frank Balile

SHIRIKA la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), limesema filamu ya The Royal Tour imefungua milango ya utalii na fursa za uwekezaji katika Hifadhi za Taifa baada ya nchi kutoka kwenye athari za janga la UVIKO-19.

Hayo yamesemwa na  Kamishina wa Uhifadhi TANAPA, Mussa Juma Kuji, katika kikao kazi kilichowakutanisha pamoja na wahariri na waandishi wa habari leo Alhamisi Machi 21,2024 jijini Dar es Salaam.

Kamishina Kuji amesema kuwa, kwa sasa katika Hifadhi za Taifa kumekuwa na ongezeko la watalii wanaotembelea Hifadhi za Taifa mwaka hadi mwaka, ambapo kwa mwaka mwaka 2018/2019, jumla ya Watalii waliotembelea Hifadhi za Taifa walikuwa 1,452,345 ikihusisha watalii wa ndani 719,172 na nje 733,173.

Amesema idadi hiyo ilianza kupungua mwanzoni mwa mwaka 2020 kutokana na janga ya UVIKO-19 na kusababisha idadi ya wageni kupungua hadi kufikia watalii 485,827 katika mwaka 2020/2021. 

Kamishna Kuji amesema kutokana na anguko hilo la utalii, Serikali ya awamu ya sita  ilichukua hatua mbalimbali katika kurejesha hali ya utalii kama ilivyokuwa hapo awali ikiwemo kutengenezwa kwa miongozo maalum ya kupokea na kuhudumia watalii na upatikanaji wa chanjo ya UVIKO-19.

Amesema kuwa, suala hilo lilikwenda sambamba na utangazaji mahiri wa vivutio vyetu kupitia filamu ya “Tanzania: The Royal Tour” iliyofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan na kuzinduliwa 2022.

"Jitihada za Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan, mwaka 2021/2022 idadi ya watalii ilianza kupanda na kufikia watalii 997,873, hali ya kuimarika kwa utalii nchini iliendelea kupanda, mwaka 2022/2023 idadi ya watalii waliongezeka na kufikia 1,670,437,Aidha, kwa mwaka huu wa fedha 2023/2024. 

Amesema katika kipindi cha kuanzia Julai 2023–Machi 19,2024, idadi ya watalii 1,514,726 wa ndani wakiwa 721,543 na wa nje 793,183), wametembelea Hifadhi za Taifa, sawa na ongezeko la asilimia 5, ikiwa ni zaidi ya lengo la kupokea watalii 1,387,987 wa nje 827,713 na watalii wa ndani 726,676, katika kipindi husika. 

Kamishna wa Uhifadhi huyo amesema kuwa, idadi ya watalii wanaotarajiwa kutembelea Hifadhi za Taifa kwa mwaka wa fedha 2023/2024 ni 1,830,081 ambapo watalii wa nje 963,413 na watalii wa ndani 866,667.

Ameongeza kuwa, katika kipindi cha miaka mitatu kumekuwa na ongezeko la siku za kukaa wageni kutoka wastani wa siku 1,749,194 katika mwaka wa fedha 2021/2022 hadi kufikia wastani wa siku 2,669,586 kufikia Februari 2024, ongezeko ambalo limechangia kuongezeka kwa mapato.

"Kumekuwepo na kuchipuka kwa masoko mapya ya utalii yenye idadi kubwa ya watalii, hali hiyo inatoa uhakika wa kuendelea kupokea watalii wengi kufika nchini kutembelea Hifadhi za Taifa, masoko hayo mapya ni China, Urusi, Ukraine, Poland, Jamhuri ya Czech na Israeli.

Kamishna wa Uhifadhi amesema kuwa, TANAPA imefanikiwa kupata tuzo ijulikanayo kama Best Practice Award ambayo hutolewa kila mwaka na taasisi ya European Society for Quality Research - ESQR, ambayo ni kwa ajili ya utoaji wa huduma bora kimataifa hutolewa na taasisi hiyo baada ya kutambua taasisi za Serikali na zisizo za Kiserikali pamoja na watu binafsi wanaotoa huduma za ubora wa viwango vya hali ya juu kimataifa.

Amesema wameendelea kupata tuzo zinazotolewa na taasisi ya ESQR kwa kipindi cha miaka minne mfululizo ambazo kati ya hizo, tuzo za miaka mitatu mfululizo zimepatikana katika kipindi cha uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita kwa kiwango cha Platinum category mwaka 2021, Gold category mwaka 2022 na Diamond category mwaka 2023.

"Hifadhi ya Taifa Serengeti imepata tuzo itolewayo na shirika la World Travel Awards (WTA) ya kuwa hifadhi bora barani Afrika kwa miaka mitano mfululizo 2019 hadi 2023, tuzo tatu kati ya hizo tano zimepatikana chini ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita za mwaka 2021 hadi 2023. 

Amezitaja Hifadhi ya Taifa Tarangire na Kilimanjaro kila moja ilipata tuzo mara mbili mfululizo kwa mwaka 2021 na 2022 ya kuwa vituo vyenye mvuto katika utalii, ambapo tuzo hizo hutolewa na jukwaa la kimataifa la Trip Advisor.

Kamishna wa Uhifadhi amesema kuwa, kampuni ya Explore Worldwide yenye makao yake makuu nchini Uingereza, mwaka huu wa 2024 imeutambua Mlima Kilimanjaro kuwa namba moja ya alama za asili za kudumu na zinazokumbukwa zaidi ulimwenguni.

"Tuzo hizi zimeliongezea Shirika kuaminiwa na wateja mbalimbali na kutoa uhakika kwao kuhusu aina ya huduma zitolewazo, kutambulika zaidi na kuongeza idadi ya watalii na kutoa uhakika kwa watalii na wadau wa utalii kuhusu ubora wa hifadhi," amesema.

Kuji amesema kwamba, kumekuwa na ongezeko la maeneo ya malazi na wawekezaji katika Hifadhi za Taifa, uwekezaji ambao umelenga kuboresha huduma za malazi katika Loji, Kambi za Kudumu, Kambi za Muda, Kambi za Jumuiya, Mabanda na Hosteli.

Amesema uwekezaji huo umeongeza idadi ya vitanda kutoka vitanda 5,755 mwaka 2021 hadi vitanda 10,094 mwaka 2024, hata hivyo, ujenzi wa malazi unaendelea wenye uwezo wa vitanda 1,148, ukikamilika kutakuwa na vitanda 11,242.

Ameongeza kwamba, kumekuwa na ongezeko la wawekezaji kwenye maeneo ambayo yalikuwa hayana mvuto kwa wawekezaji zikiwemo Hifadhi za Ruaha, Saadani na Mikumi, huku maeneo mapya ya uwekezaji yakiwa 176, wakati 34 ni loji na 142 ni kambi ambayo yameainishwa katika Hifadhi zote kwa kuzingatia mipango ya uendeshaji wa kila Hifadhi na yametangazwa kwenye tovuti ya Shirika.

Afisa Mwandamizi wa Habari na Mawasiliano Ofisi ya Msajili wa Hazina, Sabato Kosuri akieleza umuhimu wa kikao kazi.

Maofisa wa TANAPA
Wahariri na waandishi wa habari wakisikiliza taarifa iliyowasilishwa na Kamishna wa Uhifadhi TANAPA, Mussa Juma Kuji (hayupo pichani)


Wahariri na waandishi wa habari wakisikiliza taarifa iliyowasilishwa na Kamishna wa Uhifadhi TANAPA, Mussa Juma Kuji (hayupo pichani)

Afisa Uhifadhi Mkuu TANAPA, Mohamed Kiganja, akieleza jambo


Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, akitoa neno la shukrani baada ya kumalizika kwa kikao kazi

No comments