Header Ads

ad

Breaking News

SELF MICROFINANCE YATOA MIKOPO YA BILIONI 324.51, YAJIENDESHA KIFAIDA

Afisa Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa SELF Microfinance Fund (SELF MF), Mudith Cheyo, akizungumza kwenye kikao kazi hicho, Machi 11, 2024.


Na Mwandishi Wetu

AFISa Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa SELF (SELF MF), Mudith Cheyo amesema kuwa, hadi kufikia Desemba 31,2023 mfuko ulikuwa umetoa mikopo yenye thamani ya shilingi 324,506,402,014 ikiwa ni kiwango cha mikopo chechefu chini ya asilimia 10.

Akizungumza katika kikao kazi kilichowahusisha wahariri na waandishi wa habari na kuratibiwa na Ofisa ya Msajili wa Hazina, Cheyo amesema kuwa, mafanikio hayo yameuwezesha mfuko kujiendesha kwa kupata faida.

"Mafanikio tuliyopata mpaka kufikia Desemba 31,2023 yametuwezesha kupata faida na kujiendesha wenyewe, hii ni hatua nzuri kwetu," amesema.

Mfuko wa SELF ni taasisi ya Serikali chini ya Wizara ya Fedha inayojishughulisha na utoaji mikopo kwa wananchi wa kipato cha chini na kupunguza umaskini.

Afisa Mtendaji Mkuu amesema kuwa, mikopo hiyo iliwafiki wanufaika 314,055 ambapo wanawake walionuka ni 166,449 sawa na asilimia  53, huku wanaume wakiwa 147,606 sawa na asilimia 47, wakitoka katika mikoa 30 ya tanzania Bara na Visiwani Zanzibar.

Amesema Mfuko wa SELF ni mkopeshaji wa  jumla kwa taasisi ndogo ndogo za fedha, unazikopesha na kuzijengea uwezo taasisi ndogo ndogo, ambapo kwa sasa wanazikoipesha taasisi 200 nchi nzima.

Mafanikio mengine aliyoyaeleza ni pamoja na Mfuko wa SELF kusaidia kutengeneza ajira kwa wakopaji kwa wao wenyewe na wale wanaowaajiri, kwani kwa mwaka 2023 zimetengezwa ajira 37,024.

Afisa Mtendaji Mkuu amesema Mfuko wa SELF unafanya kazi nchi nzima kupitia matawi yake 12 ambayo ni Dar es Salaam inayohudumia Dar es Salaam yenyewe na Pwani, Morogoro (Morogoro, Katavi), Arusha (Arusha, Manyara, Kilimanjaro) na Mtwara (Mtwara, Lindi).

Mingine ni Tanga (Tanga, Ruvuma), Rukwa, Zanzibar (Unguja, Pemba), Kahama (Shinyanga,Tabora),Geita (Geita, Kagera, Kigoma), Mwanza (Mwanza, Simiyu) na Iringa (Iringa, Njombe).

Cheyo ametaja aina ya mikopo inayotolewa ni MFIs/SACCOS inayolenga wanufaika wanaofanya biashara au kilimo, ambapo riba ya mikopo hiyo ni kati ya asilimia 16-18 kwa mwaka.

Mikopo mingine ni ya moja kwa moja kwa wanufaika ambao ni wajasiriamali wadogo na wa kati-MSMEs,  wakulima wadogo/wafugaji kwa ajili ya kuboresha makazi, vikundi, nishati safi ya kupikia na mikopo kwa ajili ya watumishi wa umma, riba yake ni kati ya asilimia 15-22.

Afisa Mtendaji Mkuu ametoa mfano wa wanufaika ni Sta Natural Product Ltd, ambaye ni mjasiriamali kwenye sekta ya viwanda vidogo vidogo ambaye amekopa mara tatu kwenye mfuko huo.

Awali, mjasiriamali huyo alikuwa hakopesheki kwenye taasisi nyingine za fedha, lakini hadi sasa amejindeleza na kufikia mkopo mkubwa zaidi ya shilingi milioni 100, amekuza karakana yake ya kutengeneza mafuta na sabuni kutokana na zao la mchikichi.

Amesema mjasiriamali huyo amefungua vituo viwili vya kuchakata mafuta ya mchikichi, kimoja kiko Mkuranga na kingine Kibiti vyote vikiwa mkoani Pwani. Kila kituo kinasaidia wakulima 150 wa maeneo hayo kupata huduma ya kukamua mafuta.

Ameitaja taasisi nyingine iliyonufaika na Mfuko wa SELF ni Bright Future Academy inayojishughulisha na masuala ya elimu Zanzibar, ambapo amekopa mara tatu hadi sasa, alianza kukopa SELF kipindi ambacho alikuwa hana sifa ya kukopesheka kwenye taasisi nyingine za fedha, lakini sasa ana uwezo wa kukopa hadi shilingi milioni 300.

"Kutokana na uwezeshaji wa SELF, amefanikiwa kutoka kwenye nyumba ya kupanga yenye vyumba vinne hadi kununua kiwanja na kujenga shule yenye madarasa 32, bado anaendelea kupanua shule," amesema Cheyo.

Amesema shule hiyo ya Bright Future ilikuwa na wanafunzi 300, lakini hadi kufikia sasa ina jumla ya wanafunzi 1,470, na kuwa shule ya kwanza Zanzibar kufaulisha kwa miaka miwili katika matokeo ya darasa la saba.

Afisa Mtendaji Mkuu amesema kuwa, palipo na mafanikio hapakosi changamoto, katika kutekeleza majukumu yake ya kuongeza upatikanaji wa huduma za kifedha hasa kwa wananchi wa kipato cha chini, Mfuko unakumbana na chanagmoto nyingi.

Amezitaja changamoto hizo ni wananchi wengi kutokuwa na elimu ya fedha , jambo linalosababisha kukosa uelewa wa kutosha wakati wa kufanya maamuzi ya kukopa mikopo au kutumia mikopo nje ya malengo yaliyokusudiwa.

"Wananchi wengi hawana utamaduni wa kukopa na kurejesha, utamaduni wa kurejesha mikopo kwa hiari bado ni mdogo sana," amesema.

Mkurugenzi huyo amesema kuwa, Mfuko wa SELf umejiwekea malengo makuu matatu  katika mpango mkakati wake ambao ni pamoja na kuwafikia wateja wengi zaidi hasa wa kipato cha chini.

Amesema hatua hiyo itasaidia kuongeza utoaji wa mikopo, kusogeza huduma karibu na wananchi na kuwafikia walengwa wengi zaidi.

Mkakati mwingine ni kuongeza ufanisi ili kutoa huduma bora na kwa wakati, jambo ambalo litawezekana kwa kubadilisha mifumo na kutumia zaidi teknolojia.


Mkurugenzi Mkuu amesema kuwa, mpango mkakati mwingine ni kuhakikisha taasisi inajiendesha kwa faida na huduma zinazotolewa zinakuwa endelevu.

Mfuko wa SELF, ni taasisi ya Serikali chini ya Wizara ya Fedha inayoshughulika na utoaji wa mikopo hasa kwa wananchi wa kipato cha chini waweze kujishughulisha  na shughuli za uzalishaji mali ili kujiongezea kipato na kupunguza umaskini.

Amesema Mfuko huo ulianza kutekeleza majukumu yake Julai Mosi 2015, ukitrithi majukumu ya Mradi wa serikali iliojulikana kama Small Entrepreneurs Loan Facility (Self Project) (1999/2000-2014/2015).

Meneja wa Biashara na Uhamasishaji wa Mfuko SELF Microfinance Fund (SELF MF), Linda Mshana, akifafanua jambo katika kikao kazi.

Mkurugenzi wa Biashara na Masoko wa SELF Microfinance Fund (SELF MF), Petro Masaba akizungumza katika kikao kazi kilichofanyika leo Jumatatu Machi 11,2024, jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Mikopo, Santiel Yona, akifafanua jambo
Afisa Mwandamizi wa Habari na Mawasiliano Ofisi ya Msajili wa Hazina, Sabato Kosuri akieleza jambo wakati wa kikao kazi kati ya Mfuko wa SELF Microfinance  na wahariri kilichofanyika leo Jumatatu Machi 11,2024 jijini Dar es Salaam. 
Wahariri wakifuatilia wasilisho la Afisa Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa SELF Microfinance, Mudith Cheyo
Wahariri wakifuatilia wasilisho kwa makini
Afisa Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa SELF Microfinance Fund (SELF MF), Mudith Cheyo (katikati), Mkurugenzi wa Mikopo, Santiel Yona (kulia) na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Salim Said Salim, wakisikiliza maswali kutoka kwa wahariri na waandishi wa habari (hawapo pichani)
Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Salim Said Salim, akitoa neno la shukrani


No comments