Header Ads

ad

Breaking News

NEEC, WANAWAKE 5,000 KUMPONGEZA RAIS SAMIA

Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), BengI Issa

Na Mwandishi Wetu

BARAZA la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC) kwa kushirikiana na Taasisi mbalimbali za wanawake hapa nchini kesho wameandaa hafla maalumu ya kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan ikiwepo pia kutambua umahiri wake wa kuwa mwanamke kinara kwa masuala ya nishati safi ya kupikia na utunzaji wa mazingira.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mtendaji wa NEEC, BengI Issa hafla hiyo ambayo itahudhuriwa pia na Rais Samia itafanyika kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee sambamba na kumpongeza kwa ujasiri na uthubutu wake.

“Hii ni fursa ya kipekee kwa wanawake wa mkoa wa Dar es Salaam kujitokeza kwa wingi kwenye hafla hiyo maalumu ya kutambua kuwa Rais Samia Suluhu kuwa ni mwanamke kinara wa masuala ya nishati safi ya kupikia na utunzaji wa mazingira,” amesema.

Issa amesema Rais Samia kwa ujasiri wake mbali ya kuwa mwanamke kinara kwenye masuala nishati safi ya kupikia na utunzaji wa mazingira hapa nchini, amefanikiwa kuifungua nchi katika nyanja za kiuchumi, kijamii na kisiasa pia.

“NEEC inatambua na kuheshimu mchango wa Rais Samia katika kuwawezesha wanawake kutoka kwenye mazingira magumu ya nishati ya kupikia ikiwemo mkaa na kuni ambavyo vimekuwa vikileta madhara kwa afya ya binadamu na mazingira hivyo kupitia mpango huo utaleta matokeo chanya kwa Tanzania na Afrika kwa ujumla wake,” alisema Bi. Issa.

Amesema kupitia mpango huo Rais Samia anatarajia kwenda Ufarasa kuongoza kikao ambacho kitawakutanisha marais wa dunia wakilenga kumuunga mkono sambamba na kuja na mikakati itakayowezesha kukamilisha mpango utakaokuwa mwarobaini wa nishati safi ya kupikia na rafiki kwa mazingira.

Aidha, alibainisha kuwa Baraza linajumla ya majukwaa ya uwezeshaji 3,500 katika ngazi ya mtaa, vijiji, kata, wilaya, mikoa mpaka ngazi ya kitaifa lengo likiwa kuwaleta wanawake wote pamoja na kujadili na kuibua fursa mbalimbali za kiuchumi na kutoa mchango kwa maendeleo ya taifa.

“Majukwaa yote hapa nchini yaende na kasi ya mheshimimiwa Rais Samia ya kujielekeza kwenye matumizi ya nishati safi na tuone kwamba hii ni fursa ambayo kila mwanamke wa kitanzania anatakiwa kuichangamkia sambamba kuandaa miradi pamoja na kubuni rasilimali ambazo zinaendana na utunzaji wa mazingira,” amesema.

Hafla hiyo inatarajiwa kuwakutanisha wanawake zaidi ya 5,000 kutoka makundi mbalimbali ya wanawake nchini kama majukwaa ya uwezeshaji wanawake kiuchumi, wanawake kutoka vyama vya utafiti , wanawake kutoka vyama vya makandarasi Tanzania, wanawake waandishi wa habari wanawake, wanawake kutoka kwenye vikoba, wanawake kutoka vyama vya kilimo na vyama vya utafiti.

No comments