Header Ads

ad

Breaking News

MIAKA MITATU YA RAIS DKT.SAMIA, TANAPA YAKUSANYA BILIONI 337.42

Kamishna wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Mussa Juma Kuji akifafanua jambo wakati wa kikao kazi na wahariri na waandishi wa habari kilichofanyika Alhamisi Machi 21,2024 jijini Dar es Salaam

Na Frank Balile

KAMISHNA wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Mussa Juma Kuji, amesema katika kipindi cha miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan, kumekuwa na ongezeko la mapato kutoka shilingi 174,715,158,494 za kipindi cha mwaka 2021/2022 hadi kufikia shilingi 337,424,076,896 katika kipindi cha mwaka 2022/2023, ikiwa ni sawa na ongezeko la shilingi 162,708,918,402 ambayo ni asilimia 94.

Hayo yamesemwa na Kamishna wa TANAPA, katika kikao kazi kilichowakutanisha shirika hilo, wahariri na waandishi wa habari Alhamisi Machi 21,2024 jijini Dar es Salaam.

Kuji amesema hayo ni mafanikio yaliyochagizwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan, baada ya kutoa filamu ya Royal Tour na kuonesha mataifa mbalimbali duniani, ambapo kwa mwaka wa fedha 2023/2024 kuanzia Julai 2023 hadi Machi 19, 2024, Shirika limekusanya shilingi 340,101,108,465 ukilinganisha na matarajio ya kukusanya shilingi 295,466,811,506 hadi Machi 2024. 

"Kiasi hiki chan fedha cha shilingi bilion 340 ni ongezeko la shilingi 44,634,296,959 ambayo ni sawa na asilimia 15, kwasasa shirika lina matarajio ya kukusanya kiasi cha shilingi 382,307,977,497 hadi Juni 2024." amesema Kamishna wa TANAPA, Kuji.

Kuji amesema mapato hayo yanazidi mapato ya shilingi 282,450,446,103 yaliyokusanywa mwaka 2018/2019, kabla kuzuka kwa janga la UVIKO–19, ambayo yalikuwa ndiyo kiwango cha juu cha mapato katika Shirika.

Amesema kuwa, 0ngezeko hilo la watalii na mapato linakwenda sambamba na malengo ya Ilani ya Chama Chama cha Mapinduzi 2020–2025 inayoelekeza idadi ya watalii nchini kufikia milioni 5 na mapato ya dola za Marekani bilioni 6 kwa mwaka ifikapo mwaka 2025.

Ameongeza kuwa, kumekuwepo na kuanzishwa kwa masoko mapya ya utalii yenye idadi kubwa ya watalii, jambo linalotoa uhakika wa kuendelea kupokea watalii wengi kutembelea Hifadhi za Taifa nchini.

Kamishna wa TANAPA, amebainisha masoko hayo mapya ni China, Urusi, Ukraine, Poland, Jamhuri ya Czech na Israeli, huku akiweka wazi ongezeko la maeneo ya malazi na wawekezaji katika Hifadhi za Taifa. 

Kuji amesema uwekezaji umelenga kuboresha huduma za malazi katika nyumba za kulala wageni (loji), kambi za Kudumu, kambi za muda, kambi za jumuiya, mabanda na hosteli, uwekezaji huo umeongeza idadi ya vitanda kutoka vitanda 5,755 vilivyokuwepo mwaka 2021 hadi vitanda 10,094 mwaka 2024. 

Amesema hata hivyo, ujenzi wa malazi unaendelea wenye uwezo wa vitanda 1,148 ambapo ukikamilika kutakuwa na jumla ya vitanda 11,242, pia kumekuwepo na ongezeko la wawekezaji kwenye maeneo ambayo yalikuwa hayana mvuto kwa wawekezaji zikiwemo Hifadhi za Ruaha, Saadani na Mikumi.

"Jumla ya maeneo mapya ya uwekezaji 176, loji zipo 34 na kambi 142 ni kambi yameainishwa katika hifadhi zote kwa kuzingatia mipango ya uendeshaji wa kila hifadhi na yametangazwa kwenye tovuti ya Shirika," amesema.

Kuhusu ongezeko la bidhaa za utalii, Kamishna wa TANAPA, amesema katika maeneo mengine ambayo awali hayakuwa na bidhaa husika, lakini sasa mabadiliko yanaonekana, ikiwemo shughuli za utalii wa puto (balloon), uliokuwa ukifanyika katika Hifadhi ya Taifa Serengeti kwenda Hifadhi za Tarangire, Ruaha na sasa maandalizi yanaendelea kwa Hifadhi ya Mikumi.

"Utalii wa faru katika Hifadhi ya Taifa Mkomazi, utalii wa baiskeli Hifadhi ya Taifa Kilimanjaro na Arusha, utalii wa michezo na burudani kwenye Hifadhi ya Taifa Serengeti hasa mchezo wa tennis na Hifadhi ya Taifa Mikumi kwa upande wa soka, pete na kikapu, hizi ni bidhaa zilizoongeza mvuto wa hifadhi hizo," amesema.

Amesema hata ongezeko kwa mbio za marathon katika maeneo ya ndani na pembezoni mwa Hifadhi za Taifa, zimekuwa zikivutia washiriki wengi, huku zikitangaza vivutio vya utalii katika maeneo ya hifadhi zilikoratibu mbio za marathoni ambazo ni Hifadhi ya Taifa Serengeti, Arusha, Mkomazi, Ruaha, Katavi, Mahale, Gombe, Burigi- Chato na Kilimanjaro.

Amesema kujiunga na mfumo wa utoaji wa huduma kwa kiwango cha Kimataifa (ISO), ambapo mwaka 2018 TANAPA iliingia katika mchakato wa kutambuliwa na Shirika la Viwango Duniani ili kujijengea kuaminiwa na wateja. 

"Kutambuliwa kwa TANAPA mwaka 2021 na ISO, kumewawezesha wateja kuamini na kuchagua huduma zinazotolewa na TANAPA na hifadhi zake hivyo, kuongeza idadi ya watalii na mapato."

Amesema katika kipindi cha miaka mitatu, Shirika limeendelea kutekeleza shughuli za utalii na uhifadhi kwa kuzingatia matakwa ya kiwango cha ubora cha ISO 9001:2015 kinachohusu utoaji wa huduma bora kwa wateja.

Katika kuimarishwa kwa miundombinu ya ukusanyaji wa mapato, TANAPA imeendele kuimarisha miundombinu ya ukusanyaji wa mapato ikiwemo kukamilisha ujenzi wa lango la kisasa la Naabi lenye uwezo wa kupokea zaidi ya magari 600 na wastani wa wageni zaidi ya 1,500 kwa siku.

Kamishna Kuji amesema katika kipindi cha miaka mitatu, TANAPA pia imeweza kujenga malango mapya 10 na ya kisasa katika Hifadhi za Taifa Tarangire mawili, Mkomazi matatu, Serengeti mawili na Nyerere matatu.

Amesema TANAPA imekuwa ikishinda tuzo za uandaaji bora wa taarifa za hesabu kwa kufuata viwango vya kimataifa kwa upande wa taasisi za umma zinazotolewa na Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA).

Ameongeza kuwa, Shirika limekuwa mshindi wa pili wa tuzo ya uandaaji bora wa taarifa za hesabu za mwaka 2022 katika kundi la taasisi za kiserikali zinazotumia mfumo wa IPSASs (2nd winner in the government agencies category (users of IPSASs) for the best presented financial statements award for the year 2022).

Kamishna Kuji amesema kuwa, serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo ikiwemo Benki ya Ujerumani (KfW), Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), imeendelea kuboresha, kujenga na kukarabati miundombinu ya barabara na viwanja vya ndege vilivyopo katika Hifadhi za Taifa.

Amesema Shirika lina mtandao wa barabara ambao umeongezeka kutoka urefu wa kilometa 7,638 mwaka 2021 na kufikia urefu wa kilometa 16,471 kwa mwaka 2024, kazi nyingine za miundombinu zilizofanyika ni kukarabati wastani wa kilometa 3,938 za barabara, kutengeneza njia za kutembea kwa miguu zenye urefu wa kilomita 334 pamoja na ujenzi wa madaraja 14 na vivuko 399.

Ameongeza kuwa, ukarabati viwanja vya ndege (Airstrips) 11 katika maeneo ya barabara za kuruka na kutua ndege (runway) na viungio vyake pamoja na maegesho ya ndege kwa kiwango cha changarawe katika hifadhi za Serengeti (1), Nyerere (3), Tarangire (1), Mkomazi (2), Saadani (1), Mikumi (1) na Ruaha (2), pamoja na viwanja vya kutua helikopta (helipads) vitano katika Mlima Kilimanjaro vilijengwa kwa kiwango cha zege kwa kuzingatia kanuni za TCAA na ICAO.

Amesema kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo Benki ya Dunia (Mradi wa REGROW) na IMF (Mradi wa TCRP), mitambo 59 ya aina mbalimbali ilinunuliwa kupitia mradi wa kuboresha usimamizi wa maliasili na kukuza utalii kusini mwa Tanzania (Resilient Natural Resources Management for Tourism and Growth - REGROW) ni motor grader 5, compactor 3, low loader 2, malori 17, excavator 2, bulldozers 2, concrete mixers 5, matrekta 7, malori ya kubebea maji 5, magari ya sinema (cinema vans) 4, magari ya kutolea elimu kwa wanafunzi na jamii “expedition trucks” 3 na malori ya kutengenezea magari (mobile workshop).

Kamishna wa TANAPA, amesema kjuwa, jumla ya shilingi 27,873,761,395.00 zilitumika kununua mitambo hiyo, huku akisema mitambo iliyonunuliwa kupitia fedha za mpango wa maendeleo kwa ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya UVIKO-19 (TCRP) ni motor grader 5, compactor 4, low loader 4, malori 15, excavator 4, magari madogo 7 (Landcruiser), concrete mixer 1, Back low loader 1 na malori ya kubebea maji 4, thamani ya shilingi 17,765,532,026 zilitumika kununua mitambo hiyo. 

"Mitambo hii imesaidia kwa kiasi kikubwa kuboresha miundombinu ya barabara katika Hifadhi zetu, wageni wetu hawapati usumbufu sana," amesema.

Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) ni Taasisi ya Umma lilianzishwa mwaka 1959 kwa Sheria ya Hifadhi za Taifa Sura ya 412 (National Parks Act Cap. 282) na marekebisho Na. 282 ya 2002 yenye dhamana ya kusimamia na kuendeleza maeneo yote yaliyotengwa kuwa Hifadhi za Taifa.

Maeneo ya Hifadhi za Taifa yanawakilisha kiwango cha juu kabisa cha uhifadhi wa wanyamapori nchini (highest conservation status of wildlife) ambapo hakuna shughuli zozote za kibinadamu zinazoruhusiwa kufanyika. Hadi sasa Shirika linasimamia Hifadhi za Taifa 21 zenye eneo la ukubwa wa kilomita za mraba 96,908.88 ambalo ni sawa na 10.2% ya eneo lote la nchi.

Maofisa wa TANAPA wakiwa makini kusikiliza
Wahariri wakiwa makini kusikiliza wasilisho kutoka kwa Kamishna wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Mussa Juma Kuji (hayupo pichani)
Afisa Mwandamizi wa Habari na Mawasiliano Ofisi ya Msajili wa Hazina, Sabato Kosuri, akifafanua jambo

No comments