Header Ads

ad

Breaking News

MIAKA MITATU YA DKT.SAMIA SULUHU HASSAN, TAWA YAWANEEMESHA WAVUVI NA WAFUGAJI

Kamishna wa Uhifadhi na Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Mabula Misungwi Nyanda akifafanua jambo wakati wa kikao kazi kati ya mamlaka hiyo, wahariri na waandishi wahabari kilichofanyika Jumatatu Machi 18,2024 jijini Dar es Salaam.


Na Frank Balile

MAMLAKA ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), imeweka utaratibu wa kuiwezesha jamii kunufaika na shughuli za uvuvi na ufugaji nyuki katika maeneo ya mapori ya akiba na tengefu katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan.

Akizungumza katika kikao kazi kilichowakutanisha wahariri, waandishi wa habari na TAWA, Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Mabula Misungwi Nyanda, amesema kuwa,kuimarika kwa uhusiano huo kumewezesha kupatikana ajira kwa wavuvi 7,511 na warina asali 2,046.

 Nyanda amesema jumla ya shilingi bilioni 3.98 zilizotokana na shughuli za uvuvi na ufugaji nyuki katika Mapori ya Akiba ya Rukwa, Ugalla, Uwanda, Moyowosi Kilombero na Inyonga, zilipatikana.

"Wananchi wamekuwa wakinufaika kwa kuvua wastani wa tani 15 kwa siku katika pori la akiba uwanda pekee, kupitia uvuvi Halmashauri ya Sumbawanga imekusanya shilingi milioni 303 kupitia leseni na ushuru kutokana na uvuvi kwenye hifadhi katika kipindi cha Julai hadi Desemba 2023.

Kamishna Nyanda ameongeza kuwa, TAWA imeendelea kushirikiana na jamii katika shughuli za uhifadhi kwa kuchangia miradi ya maendeleo inayoibuliwa na jamii kwenye maeneo mbalimbali hususan yanayozunguka Mapori ya Akiba. 

Amesema kuwa, kati ya mwaka 2021 na 2024, TAWA imechangia miradi ya jamii yenye thamani ya shilingi milioni  193.3 ikiwemo ujenzi wa soko la samaki katika mji mdogo wa Ifakara–Kilombero (shilingi milioni 66), ujenzi wa darasa, ofisi ya walimu na ununuzi wa madawati katika Shule ya Msingi Usinge iliyopo Kaliua mkoani Tabora iliyotumia kiasi cha shilingi milioni 50.

Kamishna mkuu huyo amesema TAWA imechangia madawati 100 katika Wilaya ya Bunda, ununuzi wa mashine mbili za kusaga mkoani wa Mara, kuchangia shilingi milioni 10 kwa ajili ya ujenzi wa zahanati na darasa huko Mwibara, huku ikichangia shilingi milioni 20 kwa ajili ya ujenzi wa Zahanati ya Bungo wilayani Korogwe mkoani Tanga.

"Ongezeko la matukio ya wanayapori wakali na waharibifu kati ya mwaka 2021-2024, TAWA imefanya doria siku watu 58,818 kukabiliana na matukio 8,001 yaliyotokea katika Wilaya 73 nchini," amesema Kamishna wa Uhifadhi, Nyanda.

Nyanda amesema jitihada nyingine zilizofanyika ili kupunguza madhara kwa maisha ya watu na mali zao ni pamoja na kujenga vituo vituo 16 vya askari katika Wilaya 16 ili kuitikia kwa haraka matukio ya wanyamapori wakali na waharibifu.

"Tumenunua pikipiki 50, tumetoa mafunzo kwa kuwashirikisha askari wa wanyamapori wa vijiji - na jeshi la akiba 184, askari waliopata mafunzo ya kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu wanafanya kazi kwenye maeneo sugu ya matukio  ambayo ni Bunda, Busega, Meatu, Same, Lindi, Korogwe,Itilima, Liwale, Nachingwea, Mwanga, na Tunduru.

Amesema wameweza kuongeza vituo vya muda vya askari kutoka 46 hadi 55, wameongeza idadi ya askari wa kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu kutoka 139 hadi 237 na ujenzi wa mabwawa 10 katika mapori ya akiba Kizigo tisa lililopo Manyoni na Mkungunero moja lililopo Wilaya ya Kondoa.

"Kutoa elimu ya uhifadhi na mbinu rafiki za kujikinga na madhara ya wanayapori wakali na waharibifu kwa wananchi 764,438 katika vijiji 1,319 nchini, ambapo wameviimarisha vikundi 179 vya wananchi vya kufukuza tembo na kutoa vifaa vya kufukuza tembo ikiwemo Roman candles 1,320, thunder flashes 1,310, vuvuzela 548, filimbi 288, tochi 524, mbegu za pilipili na mabomu ya pilipili.

Amesema kuwa, kufunga visukuma mawimbi kwa viongozi wa makundi ya tembo nane katika Wilaya za Same, Tunduru, Liwale na Nachingwe kumesaidia kuimarisha mawasiliano kwa kutoa namba ya kupiga simu bure ili wananchi watoa taarifa mapema.

Mjumbe wa Kamati Utendaji ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Neville Meena amesema kikao kazi hicho kimekuwa na manufaa kwa wahariri na waandishi wa habari kujifunza na kufahamu kazi mbalimbali za mamlaka hiyo, huku akiwashauri waandishi kuendelea kujifunza kwa kusoma taarifa mbalimbali za mamlaka hiyo ili kuwa na wigo mpana wa kuifahamu taasisi hiyo.

Maafisa wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), wakisikiliza

Wahariri na waandishi wa habari wakifuatilia taarifa ya Kamishna wa Uhifadhi na Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Mabula  Misungwi Nyanda (hayupi pichani)
Baadhi ya wahariri wakiwa makini kusikiliza
Baadhi ya wahariri na waandishi wa habari wakisikiliza
Afisa Mwandamizi wa Habari na Mawasiliano Ofisi ya Msajili wa Hazina, Sabato Kosuri akieleza jambo wakati wa kikao kazi.
Afisa Habari wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Beatus Maganja akieleza jambo

No comments