Header Ads

ad

Breaking News

MIAKA MITATU YA DKT SAMIA, TFS YAKUSANYA SHILINGI 371,956,374,658.38

Kamishna wa Uhifadhi, Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Profesa Dos Santos Silayo, akielezea mipango yao kwa wahariri na waandishi wa habari wakati wa kikao kazi kilichoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina jijini Dar es Salaam leo Jumanne Machi 19,2024.


Na Mwandishi Wetu

KAMISHNA wa Uhifadhi, Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Profesa Dos Santos Silayo, ubunifu mkubwa uliofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan katika kipindi cha uongozi wake wa miaka mitatu, umewezesha Wakala huo kuongeza idadi kubwa ya watalii wanaotembelea

vituo vya utalii ikolojia kutoka watalii 59,606 kwa mwaka 202/2021 hadi kufikia watalii 242,824 kwa mwaka 2022/2023.

Profesa Silayo ameyasema hayo wakati wa kikao kazi kati ya TFS, wahariri na waandishi wa habari kilichofanyika leo Jumanne Machi 19,jijini Dar es Salaam, huku akiweka wazi kuwa, katika kipindi cha miaka mitatu, Wakala umekusanya jumla ya shilingi 371,956,374,658.38 na kuwasilisha Mfuko Mkuu wa Serikali shilingi 62,900,000,000, ikiwa ni asilimia 15 ya makusanyo.

Amesema kabla ya ongezeko hilo la watalii, walikuwa wakikusanya mapato kiasi cha shilingi 154,965,050, lakini baada ya watalii kuongezeka mapato nayo yaliongezeka na kufikia shilingi 1,5018,940,965.Kikao kazi hicho kimeratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina.

"Wakala tumefaidika sana na juhudi za makusudi zilizochukuliwa na zinazochuliwa na Serikali ikiwemo ubunifu wa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan wa kuandaa filamu ya “Tanzania the Royal Tour” ambayo imetangaza nchi yetu ndani na nje ya nchi," amesema.

Profesa Silayo amesema hayo ni mafanikio makubwa kupatikana na Wakala katika sekta ya utalii eneo la utalii ikolojia kuliko wakati mwingine wowote, huku wakijiwekea malengo ya kuweka rekodi mpya kwa kufikisha watalii 500,000 na kukusanya shilingi bilioni tatu ifikapo mwaka 2025.

Mbali na mapato hayo, Profesa Silayo amesema wamejenga hosteli tatu, ambazo mbili zimejengwa katika shamba miti la la Wino wilayani Songea Vijijini mkoani Ruvuma na moja katika msitu wa Sao Hill Wilayani Mafinga mkoani Iringa, ujenzi ambao umekamilika.

Kamishna wa Uhifadhi TFS, amesema pamoja na kujenga nyumba tatu, pia wamejenga hosteli moja na nyumba za kupumzika wageni mbili zimekarabatiwa katika hifadhi ya Mazingira Asilia Amani wilayani Muheza mkoani Tanga, ukarabati wake umekamilika.

"Tumejenga hosteli moja ambayo imekamilika, tumekarabati nyumba mbili za kupumzikia wageni wetu, zote hizo ziko katika Hifadhi ya Mazingira Asilia Amani wilayani Muheza mkoani Tanga, haya yote ni matunda ya uongozi wa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan, kwa jitihada kubwa anazofanya kwenye sekta ya utalii," amesema Profesa Silayo.

Kamishna huyo amesema kuwa, TFS imetekeleza miradi ya makambi 43 ya watalii katika hifadhi za misitu 9, ujenzi wa banda moja la kupumzika watalii, mageti matatu na mabango nane, benchi nane na meza tatu, vyote hivyo vimefanyika katika misitu minne.

Amesema katika kipindi cha mwaka 2022/23,TFS ilipewa fedha kiasi cha shilingi bilioni 4 kutoka sehemu ya fedha alizotoa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan za kupunguza athari za UVIKO–19 kwa kuboresha uhifadhi na shughuli za utalii katika misitu yetu.

Mhifadhi mkuu huyo amesema miradi hiyo imekamilika kwa ufanisi ambayo ni ujenzi wa malango matano katika hifadhi tano, ujenzi wa barabara yenye urefu km 97 na njia za kutembea kwa miguu km 190.5 katika hifadhi 11.


"Wakala tumeendelea kutangaza vivutio vya utalii kupitia maonesho mbalimbali ya ndani na nje ya nchi ikiwemo Sabasaba, Nanenane, Tanga Trade Fair, International Tourism Expo Japan 2022, East Africa International Tourism Expo,S!TE na kwenye Kombe la Dunia 2022.

Profesa Silayo amesema ubunifu wa mazao mapya ya utalii kama mashindano  maarufu ya West Kili Forest Tour Challenge, Bata Msituni Festival, Magamba Walkathon, Swahili Marathon, Meru Forest trail Run, Rubare Marathon, Mkeka na Khanga Festival na Sao Hill Forest Rally, kutangaza utalii.

 

Baadhi ya wahariri na waandishi wa habari wakifuatilia maelezo ya Kamishna wa Uhifadhi, Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Profesa Dos Santos Silayo kuhusu mafanikio ya Wakala kwa kipindi cha miaka mitatu tangu kuingia madarakani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan.

No comments