Header Ads

ad

Breaking News

MFUKO WA SELF WAWA NEEMA KWA WANANCHI

Afisa Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa SELF Microfinance Fund (SELF MF), Mudith Cheyo, akizungumza kwenye kikao kazi hicho, Machi 11, 2024.


Na Selemani Msuya

MFUKO wa Self umetoa mikopo ya zaidi ya sh. bilioni 324 kwa wananchi 314,055 wa mikoa 30 nchini huku ukijipanga kupanua wigo siku zijazo.

Mfuko pia umesema katika mikopo iliyotoa kiwango cha mikopo chechefu ni chini ya asilimia 10, huku wakijipanga kukabiliana na changamoto ya mikopo kaushadamu.

Hayo yamesemwa jana na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mfuko huo, Mudith Cheyo akizungumza kwenye mkutano wa 53 wa ya taasisi hiyo na wahariri wa vyombo vya habari Dar es Salaam, kupitia uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina.

Cheyo amesema hadi Desemba 31 mwaka jana, mfuko huo unaotarajia kuwezesha wananchi wengi kwa mikopo, ulifikia zaidi ya wananchi 300,000; wanawake 166,449 sawa na asilimia 53 na wanaume 147,606 sawa na asilimia 47.

Amesema pia umekopesha na kuzijengea uwezo taasisi ndogo 200 za fedha na kutengeneza ajira 37,024 kwa mwaka jana na kutoa elimu kwa wakopaji 1,519.

Ofisa Mtendaji huyo amesema katika kipindi cha miaka mitatu ya Rais Samia Suluhu Hassan, Mfuko wa Self umepata faida ya sh. bilioni 2 huku ikitoa gawio kwa serikali zaisdi ya shilingi milioni 240

“Tumekuwa tukikua mwaka hadi mwaka, na tumepata faida ya sh. bilioni mbili, tukatoa gawio la zaidi ya sh. milioni 240, huku mtaji ukiongezeka kutoka sh. bilioni 56 hadi 62,” amesema.

Cheyo amesema mikakati yao ni ifikapo mwaka 2026 Mfuko uwe na matawi 20 kutoka 12 ya sasa, huku akisisitiza kuwa wamejipanga kuondoa mikopo kaushadamu.

Amesema kupitia mkakati wa kuongeza matawi wanatarajia kwa siku za karibuni watafikia kundi kubwa la Watanzania hasa kwenye SMEs ambao wanakadiriwa kufikia milioni nne.

Mkurugenzi wa Biashara wa Self, Petro Mataba amesema Mfuko unafanya kazi kwa kuzingatia uadilifu, ushirikiano, ubunifu, mteja na uwajibikaji, hali imewawezesha kukua kwa kasi.

Amesema Mfuko umetoa mikopo kwa wananchi na taasisi kama Kampuni ya Star Natural Product iliyokopeshwa sh. milioni 100 na shule ya Bright Future Academy sh. milioni 400.

Ametaja changamoto zilizopo kuwa ni wananchi wengi kukosa elimu ya fedha, kujishughulisha na biashara zisizo rasmi na kukosa utamaduni wa kukopa na kurejesha, ingawa wanaendelea kutoa elimu ili wabadilike.

Mkurugenzi wa Masoko, Santiel Yona amesema mpango mkakati wao ni kufikia wateja wengi hasa wa kipato cha chini, kuongeza ufanisi na kuhakikisha taasisi inakuwa endelevu.

Mkurugenzi wa Biashara na Masoko wa SELF Microfinance Fund (SELF MF), Petro Masaba akifafanua jambo.

Meneja wa Biashara na Uhamasishaji wa Mfuko SELF Microfinance Fund (SELF MF), Linda Mshana, akifafanua jambo katika kikao kazi.
Mkurugenzi wa Mikopo wa Mfuko SELF Microfinance Fund (SELF MF), Santiel Yona akieleza mikopo inayotolewa na Mfuko huo.
Afisa Mwandamizi wa Habari na Mawasiliano Ofisi ya Msajili wa Hazina, Sabato Kosuri akifafanua jambo wakati wa kikao kazi kati ya Mfuko wa SELF Microfinance  na wahariri 
Wahariri na waandishi wakisikiliza kwa makini 
Afisa Mwandamizi wa Habari na Mawasiliano Ofisi ya Msajili wa Hazina, Sabato Kosuri (mwenye suti), wahariri na waandishi wakisikiliza kwa makini 

No comments