Header Ads

ad

Breaking News

MCHINJITA ATAKA SHERIA USIMAMIZI UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA

Mapokezi ya Makamu Mwenyekiti Bara wa Chama  cha ACT Wazalendo, Isihaka Mchinjita yaliyofanyika Lindi Mjini. #TaifaLaWote #MaslahiYaWote


Na Mwandishi Wetu

CHAMA cha ACT Wazalendo kimeitaka Serikali kutekeleza ahadi yake ya kutunga Sheria ya kuiwezesha Tume Huru ya Uchaguzi kusimamia Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Kauli hiyo imetolewa na Makamu Mwenyekiti Bara, Isihaka Mchinjita, leo Machi 17 L, 2024 kwenye mapokezi ya kumpongeza kwa kuchaguliwa na Mkutano Mkuu Taifa yaliyofanyika katika Ofisi ya Mkoa wa Lindi iliyopo Lindi Mjini.

"Februari 2, 2024 kwenye mchakato wa kutunga Sheria ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi Serikali ilileta Jedwali la Maboresho ili kuipa dhamana Tume ya Taifa ya Uchaguzi kusimamia na kuratibu uendeshaji wa uchaguzi wa Serikali za vijiji, mitaa na vitongoji kwa kuzingatia utaratibu utakaoainishwa na Sheria itakayotungwa na Bunge" alisema Mchinjita na kuongeza;

"Kwa bahati mbaya, Miswada ya Tume ya Uchaguzi na Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani bado haijasainiwa na Rais kuwa Sheria hadi sasa. Hatujui ni maboresho gani hasa yamepitishwa kuwa Sheria. Pili, hadi sasa, Serikali haijaanza mchakato wa Sheria iliyoahidiwa bungeni ya kuipa madaraka Tume ya Uchaguzi kusimamia Uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Tunaona dalili za Serikali kupata kigugumizi katika kutekeleza ahadi yake"

"Ni muhimu Bunge lisimame kidete kuhakikisha maboresho yaliyofanyika bungeni ya kuipa dhamana Tume ya Taifa ya Uchaguzi kusimamia uchaguzi wa serikali za mitaa yanazingatiwa. Ni muhimu mchakato wa kutunga sheria kwa suala hilo uanze sasa," amesema.

Mchinjita amesema ACT Wazalendo wameshaiagiza Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Chama kuainisha vipaumbele vya ACT Wazalendo wanavyotaka kuwepo kwenye Sheria hiyo.

Katika hatua nyingine, Mchinjita amesema kwa kushirikiana na viongozi wenzake na Baraza Kivuli la Mawaziri la ACT Wazalendo, atahakikisha kuwa ACT Wazalendo kinaendelea kuwa chama kinara katika kuzisemea kero za wananchi wa Tanzania.

Amesema kuwa Watanzania wana kero nyingi na ACT Wazalendo itazipa kipaumbele. "Mfano hapa Lindi, Mradi wa kuchakata gesi wa LNG ulishafikia hatua ya Serikali kusaini HGA wakati Waziri akiwa January Makamba.

"Amekuja Waziri mpya amerudisha nyuma mjadala kana kwamba tumekuwa na wataalam wapya wanaomshauri Waziri. Kuna habari kuwa kuna tishio la wawekezaji kutoka Marekani kujitoa na hivyo kurudisha nyuma jitihada zilizofanyika kwa muda mrefu," amesema.

Mchinjita amesema ACT Wazalendo wanaitaka Serikali iharakishe mazungumzo ili mradi uanze kwa maendeleo ya nchi yetu, Lindi na Kusini kwa ujumla.

Makamu Mwenyekiti huyo ameweka bayana kuwa kipaumbele chake kingine kitakuwa kushirikiana na viongozi wenzake katika ujenzi wa chama.

"Nitatumia sehemu ya muda wangu kuzunguka nchi nzima kuhakikisha kuwa mtandao wa matawi, kata, majimbo na mikoa ambao tumeujenga nchi nzima unaendelea kuimarishwa.

Mchinjita alichaguliwa na Mkutano Mkuu Taifa uliofanyika tarehe 5 na 6 Machi 2024 kuwa Makamu Mwenyekiti Bara wa Chama. Viongozi wakuu wengine waliochaguliwa ni Dorothy Semu aliyechaguliwa kuwa Kiongozi wa Chama, Othman Masoud Othman aliyechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Chama na Ismail Jussa aliyechaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti Zanzibar.







No comments