Header Ads

ad

Breaking News

KIKWETE AMWELEZEA MWINYI, ASEMA ALIKUWA SI MTU WA KUJIKWEZA

Rais Mstaafu Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete akisaini kitabu cha maombolezo ya Rais mstaafu wa awamu ya pili, hayati Ali Hassan Mwinyi , Mikocheni jijini Dar es Salaam.

Na mwandishi wetu

RAIS Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa Awamu ya Nne, Dkt.Jakaya Kikwete amesema kwamba, hayati Alhaji Ali Hassan Mwinyi alikuwa kiongozi asiyejikweza, alikuwa mwenye mapenzi na watu wote.

Kikwete amesema hayo leo Machi 1, 2024 alipozungumza mbele ya waombolezaji waliohudhuria hafla ya kumuaga kitaifa hayati Mwinyi kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

"Mwinyi aliishi maisha ya kawaida ya uungwana, alikuwa msikivu, mtu wa kupokea maoni na zaidi alinifundisha kuwa na maamuzi hasa kwenye vitu vyenye maslahi ya taifa, yeye ndiye baba wa mageuzi ya uchumi na kisiasa hapa nchini,"  amesema Rais mstaafu Kikwete.

Naye, Waziri Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Awamu ya Pili, Mstaafu Joseph Warioba amesema, "Leo ni siku ya majonzi ya kuondokewa na mzee Mwinyi, lakini pia ni siku ya furaha ya kusherehekea maisha yake kwa mengi aliyoyafanya wakati alipolitumikia taifa letu, amekuwa na juhudi nyingi za kuleta maendeleo hasa kwenye nyanja ya kiuchumi na kisiasa," amesema Jaji Warioba. 

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM),  Abdulrahman Kinana amemwelezea hayati Mwinyi kwa kusema kuwa, "Sote ni mashahidi kwamba, hayati Ali Mwinyi alifanya jitihada za kuitoa nchi ya Tanzania kwenye mfumo wa chama kimoja kwenda kwenye mfumo wa vyama vingi," amesema Kinana.

Ameongeza kuwa, haikuwa rahisi alitupeleka kwenye uchumi huria,  alifanya yote haya na mengine mengi, huku akimshirikisha hayati baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa lengo la kuhakikisha kwamba, mabadiliko yanafanyika kwa utulivu na kulinda amani ya nchi.

Kabla ya kupelekwa Uwanja wa Uhuru, mwili wa Alhaji Mwinyi umeswaliwa katika msikiti wa BAKWATA na maziko yatafanyika kesho Zanzibar.
Rais Mstaafu Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete (kulia), akimpa pole Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi,  Mikocheni nyumbani kwao kufuatia kifo cha baba yake Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi kilichotokea februari 29, 2024.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila 
(kulia), akimpa pole Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi,  Mikocheni nyumbani kwao kufuatia kifo cha baba yake Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi kilichotokea Februari 29, 2024.

No comments