Header Ads

ad

Breaking News

KARAFUU, PARACHICHI YAWA FURSA MOROGORO

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Kuendeleza Kilimo Nyanda za Juu Kusini mwa Tanzania (SAGCOT), Bw. Geoffrey Kirenga akizungumza katika moja ya mikutano ya wadau mbalimbali wa sekta za kilimo, mifugo na uvuvi uliofanyika jijini Dar es Salaam hivi karibuni.


Na Mwandishi Wetu, Morogoro

IMEELEZWA kuwa zao la karafuu ambalo kwa sasa linalimwa mkoani Morogoro limetajwa kuwa miongoni mwa zao la kimkakati linalotarajiwa kuongeza kipato cha mkulima sambamba na ajira kwa wakazi.

Akizungumza na mwandishi wa habari mkoani hapa, Meneja wa Kituo cha Kuendeleza Kilimo Nyanda ya Juu Kusini (SAGCOT),  Kongani ya Kilombero, John Banga amesema mbali na kuupaisha mkoa, kilimo cha karafuu pamoja parachichi ni mazao yanayowavutia wakulima wengi.

“Wakulima wa karafuu mkoani hapa wamekuwa wakilima kwa ustadi mkubwa sambamba na kupewa mafunzo na safari za mafunzo Zanzibar ambako ni chimbuko la zao hili la karafuu katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” amesema Banga.

Meneja huyo amesema kuwa, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro kwa kushirikiana SAGCOT imewapeleka wakulima Zanzibar kujifunza namna bora ya kuendeleza kilimo cha karafuu hapa nchini.

“Serikali imekuwa ikitoa msaada wa taarifa za masoko, pembejeo, upatikanaji wa kifedha kwa wakulima na utoaji wa mafunzo kupitia safari za visiwani Zanzibar ili kujifunza kwa wakulima wenzao na kuongeza tija katika uzalishaji,” amesema.

Kwa mujibu wa Banga, Mkoa wa Morogoro hususan katika wilaya zake za Gairo, Mvomero na Kilombero zimekuwa na hali ya hewa nzuri pamoja na ardhi nzuri inayofaa kwa kilimo cha karafuu.

Amesema SAGCOT kupitia wabia wake mbalimbali wakiwemo IUCN, AWF, WWF na wadau wengine wa maendeleo wamekuwa wakishirikiana kwa karibu na wakulima katika kuboresha kilimo cha karafuu.

“Mwaka 2023, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro kwa kushirikiana na SAGCOT waliwezesha ziara ya wakulima zaidi ya 50 na wataalam wa mikoa ya Morogoro na Tanga kujifunza Zanzibar namna ya kuongeza thamani kwenye mazao ya viungo ikiwemo karafuu,” amesema.

Amesema kufuatia ziara hiyo, wadau walielekeza nguvu kwenye uzalishaji wa miche bora ya karafuu hadi Februari 2024, zaidi ya miche 350,000 imezalishwa katika Wilaya ya Morogoro pekee, ambapo miche hiyo inatarajiwa kupandwa kwenye mashamba ya wakulima wadogo zaidi ya 5,000.

Banga amesema Wilaya ya Gairo pekee kuna zaidi ya wakulima 500 ambao wamehamasika kufanya kilimo cha karafuu na wakulima zaidi ya 40 wamepewa mafunzo maalum ya kilimo cha kisasa cha parachichi kutoka mkoani Njombe.

“Tunategemea kupitia zao la karafuu, mapinduzi makubwa ya kiuchumi na matokeo chanya katika kukuza pato la mkulima mmoja mmoja na taifa kwa ujumla wake,” amesema Banga na kuongeza kuwa, zao hilo jipya linaratibiwa na SAGCOT kupitia kongani yake Kilombero.



No comments