Header Ads

ad

Breaking News

KAMBI YA UPIMAJI NA MATIBABU YA MOYO YAFANYIKA JKCI DAR GROUP

Wananchi wa mkoa wa Dar es Salaam wakiwa katika foleni ya kupata huduma za upimaji na matibabu ya magonjwa ya moyo wakati wa kambi maalumu ya siku mbili inayofanywa na wataalamu wa afya wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete Hospitali ya JKCI Dar Group katika kuadhimisha siku ya wanawake duniani.

Na Mwandishi Maalumu, Dar es Salaam

TAASISI ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hospitali ya Dar Group inafanya kambi maalumu ya upimaji na matibabu ya magonjwa ya moyo kwa wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam na mikoa ya jirani.

Huduma hiyo ya upimaji imetolewa kwa siku mbili za Jumamosi na Jumapili kwa watoto na watu wazima, imemaliza leo.

Hayo yamesemwa jana jijini Dar es Salaam na Kaimu Mkurugenzi  wa JKCI Hospitali ya Dar Group, Iddi Lemmah wakati akizungumza na waandishi wa habari waliofika katika hospitali hiyo kwa ajili ya kuona huduma zinazotolewa katika kambi hiyo.

Lemmah alisema upimaji huo ulikuwa na lengo la kusogeza huduma za matibabu ya kibingwa ya moyo kwa wananchi na kuwahamasisha wananchi kujenga tabia ya kupima afya za mioyo yao mara kwa mara.

“Upimaji huu unajulikana kwa jina la Tiba Mkoba ya Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan, ambapo wataalamu wa taasisi yetu wanawafuata wananchi mahali walipo na kutoa huduma za ushauri, elimu, upimaji na matibabu ya moyo.”

“Huduma iliyotolewa ni ya kupima urefu na uzito, kiwango cha sukari kwenye damu, shinikizo la damu mwilini, tunaangalia uwiano baina ya urefu na uzito, tunatoa elimu ya lishe bora kwa wananchi na tunapima jinsi moyo unavyofanya kazi pamoja na mfumo wa umeme wa moyo,” alisema Lemmah.

Lemmah alisema katika upimaji huo walishirikiana na makampuni mbalimbali ya uagizaji na usambazaji wa dawa za binadamu, ambapo wananchi waliokutwa na matatizo ya moyo, kisukari na magonjwa mengine walipewa dawa za kwenda kutumia bila malipo yoyote.

Kwa upande wake daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto wa JKCI Hospitali ya Dar Group, Eva Wakuganda alisema wananchi wengi waliowapa huduma katika kambi hiyo wamewakuta na matatizo mbalimbali ya moyo ikiwemo shinikizo la juu la damu.

Dkt.Eva alisema baadhi ya wagonjwa waliowakuta na tatizo la shinikizo la juu la damu waliacha kutumia dawa, hiyo ni kutokana na kutopata elimu ya kutosha kuhusu ugonjwa huo, kwani baada ya kupata nafuu waliacha kutumia dawa hizo.

“Shinikizo la juu la damu lisipodhibitiwa linaleta madhara kwenye moyo ikiwa ni pamoja na kutanuka na vifo vya ghafla hivyo basi, tumewapa elimu wananchi ili waweze kutumia dawa kwa usahihi na wasikatishe dozi hata kama  watapata naafuu,” alisema Dkt. Eva.

Naye, Maria Samlongo ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Lishe wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), alisema wananchi wengi aliowahudumia aliwakuta na tatizo la kuwa na uzito mkubwa ambao unaweza kusababisha kupata magonjwa ya moyo na kisukari hivyo, waliwapa elimu ya jinsi ya kuepukana na magonjwa hayo kwa kufuata mtindo bora wa maisha.

“Nimewapa wananchi elimu ya kufuata mtindo bora wa maisha, hii ikiwa ni pamoja na kufanya mazoezi, kuepuka unywaji wa pombe uliopitiliza, kutotumia bidhaa aina ya tumbaku na kula vyakula bora zikiwemo mboga za majani na matunda,” alisema Maria.

Nao, wananchi waliopata huduma ya upimaji na matibabu ya moyo katika kambi hiyo walishukuru kwa huduma waliyoipata na kusema kuwa, imewasaidia vya kutosha kuweza kutambua afya zao.

“Nimefika mahali hapa na kupata huduma ya vipimo, matibabu na elimu ya lishe bora kwani nilikuwa sijua mengi kuhusu lishe, lakini leo hii nimefahamu ni aina gani ya vyakula ninavyotakiwa kula ili niwe na moyo wenye afya,” alisema Erick Urasa mkazi wa Chanika Dar es Salaam.

“Nimepata huduma ya kupimwa vipimo mbalimbali vya moyo na nimepewa dawa za presha na sukari bure bila kulipia chochote. Ninawaomba wananchi wenzangu changamkieni fursa hii nanyi mje kupima moyo msiiache huduma hii ikawapita,” alisema Mama Martha Kabelo mkazi wa Mbezi Dar es Salaam.

Daktari bingwa wa magonjwa ya ndani wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete Hospitali ya JKCI Dar Group Edwin Masue akimpima shinikizo la damu mwananchi wa Dar es Salaam aliyefika katika kambi maalumu ya siku mbili inayoendeshwa na wataalamu wa afya wa hospitali hiyo katika kuadhimisha siku ya wanawake duniani.

Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete Hospitali ya JKCI Dar Group Eva Wakuganda akimpima moyo mtoto wakati wa kambi maalumu ya siku mbili inayofanywa na wataalamu wa Taasisi hiyo katika kuadhimisha siku ya wanawake duniani.
Afisa Lishe wa Taasisi ya Moyo Jakaya ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Maria Samlongo akimpa elimu ya lishe mwananchi wa mkoa wa Dar es Salaam wakati wa kambi maalumu ya siku mbili inayofanywa na wataalamu wa Taasisi hiyo katika kuadhimisha siku ya wanawake duniani.
Mtaalamu wa Maabara wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete Hospitali ya JKCI Dar Group Noel Mingwe akimpima sukari kwenye damu mwananchi wa mkoa wa Dar es Salaam wakati wa kambi maalumu ya siku mbili inayofanywa na wataalamu wa Taasisi hiyo katika kuadhimisha siku ya wanawake duniani.Picha zote na Khamis Mussa

No comments