Header Ads

ad

Breaking News

TEF YAOMBOLEZA KIFO CHA RAIS MSTAAFU MZEE MWINYI

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri (TEF), Deodatus Balile

 Na Mwandishi Wetu

JUKWAA la Wahariri Tanzania (TEF), limepokea kwa masikitiko taarifa ya kifo cha Rais mstaafu wa Awamu ya Pili wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi aliyefariki Dunia Februari 29, 2024 katika Hospitali ya Mzena iliyopo Kijitonyama jijini Dar es Salaam, alikokuwa akipatiwa matibabu.

Salamu hizo za rambirambi zimetolewa leo na Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri (TEF), Deodatus Balile, amesema mzee Mwinyi katika uongozi wake alianzisha demokrasia ya vyama vingi vya siasa Tanzania na kuondoa vikwazo kwa kampuni binafsi, akapunguza vikwazo vya uagizaji bidhaa kutoka nje na kupata jina la utani la Mzee Ruksa na kuwafanya watanzania wajue na kushika fedha katika uongozi wake.

Balile ameongeza kuwa, mzee Mwinyi alisisitiza uwajibikaji kazini na kukemea wazembe, kwa kuasisi maneno 'fagio la chuma' maana wazembe wote walikuwa wakiondolewa kazini au kupunguzwa kazi.

Mzee Mwinyi ndiye aliyeruhusu watumishi kujitafutia kipato cha ziada baada ya saa za kazi, ambapo madaktari wakaanza kufanya kazi kwenye vituo vingine na hata kufungua hospitali zao binafsi, huku akiamini katika ukuaji wa uchumi kwa mtu mmoja mmoja kwa maendeleo ya familia na taifa.

Mwenyekiti wa TEF amesema mzee Mwinyi wakati wa uhai wake alichagiza michezo, alikuwa mpenda michezo hasa jogging na mwandishi wa mashairi na vitabu.

Balile amesema kwa pamoja TEF wanaungana na familia ya mzee Ali Hassan Mwinyi na watanzania kuomboleza msiba huo mkubwa kwa taifa.

Mungu ailaze mahala pema peponi roho ya Mzee Mwinyi.



No comments