Header Ads

ad

Breaking News

DKT.NCHIMBI AKUTANA NA BALOZI WA MAREKANI NCHINI, WATETA MENGI

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi akisalimiana na Balozi wa Marekani nchini, Michael Battle, Balozi huyo alipofika Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Lumumba jijini Dar es Salaam, leo, Machi 6, 2024.

Na Mwandishi Wetu

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi amesema dhamira ya Mwenyekiti wa CCM ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha nchi inaongozwa kwa kuzingatia misingi ya demokrasia na utawala bora na hivyo haipaswi kutiliwa shaka hata kidogo.


Balozi Dkt. Nchimbi amesema katika utekelezaji wa dhana ya utawala bora, chini ya uongozi wa Rais Samia, Tanzania imeendelea kushuhudia kuwapo kwa uhuru wa mihimili mitatu ya dola, ambayo ni Serikali, Bunge na Mahakama.


Amesema mihimili hiyo ya dola imeendelea kutimiza wajibu wake kwa kufanya kazi vizuri na hivyo kuaminiwa na wananchi.


Dkt.Nchimbi amesisitiza kuwa CCM chini ya Rais Samia, kitahakikisha dhamira hiyo pia inaendelezwa kwa vitendo kwa kuunga mkono uwapo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar kwa maslahi ya nchi na taifa kwani umoja huo ni zaidi ya vyama vya siasa.


Katibu Mkuu huyo wa CCM amesema hayo Jumanne Machi 5, 2024, alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Marekani nchini, Michael Battle, kwenye Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Lumumba, jijini Dar es Salaam, ambapo viongozi hao walijadiliana masuala anuai kuhusu ushirikiano na uhusiano wa muda mrefu kati ya nchi hizo mbili.


Katika mazungumzo yao, wamekubaliana nchi zote mbili kuangalia maeneo yanayoweza kuboreshwa kwa manufaa ya pande zote mbili hasa katika nyanja za biashara, uchumi na uwekezaji.


Vilevile, viongozi hao kwa pamoja wameelezea umuhimu wa kurahisishwa kwa upatikanaji viza.


“Ni wajibu wetu kuimarisha na kuuboresha uhusiano huu wa muda mrefu kama tulivyoupokea kutoka kwa waasisi na watangulizi wetu kama ulivyosema balozi. Tuuboreshe kwa ajili ya manufaa ya wananchi wetu wa pande zote mbili,'' anasema Balozi Nchimbi.


Naye Balozi Battle aliupongeza uongozi wa Rais Samia kwa jinsi ambavyo umekuwa wa wazi, imara na jasiri katika kusimamia misingi ya demokrasia na utawala bora.


“Kama unavyojua uhusiano huu ni wa muda mrefu, ukaboreshwa zaidi na urafiki uliokuwapo kati ya (Mwalimu) Julius Nyerere na (John) Kennedy. 


"Pia, kulikuwa na ukaribu kati ya (Jakaya) Kikwete na (George) Bush…na sasa tunaona ukaribu kati ya Rais Samia Suluhu Hassan na Makamu wa Rais (wa Marekani) Kamala Harris. Napenda kukuhakikishia na ujue kuwa uhusiano kati ya Tanzania na Marekani ni mkubwa na halisi,” amesema Balozi Battle.

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi akizungumza na Balozi wa Marekani nchini, Michael Battle, alipofika Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Lumumba jijini Dar es Salaam, leo, Machi 6, 2024

No comments