Header Ads

ad

Breaking News

CCM PWANI YANYAKUA VITI VYOTE VYA UDIWANI MKOANI WA PWANI

Mrisho Some aliyeshinda Udiwani Kata ya Fukayosi Jimbo la Bagamoyo, hapo akisalimia na mmoja wa viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wakati wa kufungwa kwa kampeni.

Na Omary Mngindo, Kibaha

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Pwani, kimefanikiwa kuchukua viti vyote vitatu vya Udiwani kwenye uchaguzi mdogo uliofanyika mkoani hapa.

Kata zilizofanya chaguzi zake baada ya madiwani wake kutangulia mbele za haki ni Fukayosi Jimbo la Bagamoyo, Kata ya Mlanzi Jimbo la Kibiti na Msangani Kibaha Mji, ambapo wagombea wake waliibuka na ushindi wa kishindo.

Taarifa ya Katibu wa Siasa, Uenezi na Mafunzo mkoani hapa David Mramba imeeleza kuwa, chama hicho kimewasha indiketa baada ya kupata ushindi mnono wa uchaguzi huo kwa kuwapiga vibaya wagombea kutoka vyama rafiki.

Mramba amesema kuwa wananchi mkoani Pwani wameonyesha upendo mkubwa kwa Dkt Samia Suluhu, kwa kumpatia zawadi nono ya kura za kutosha kwa wanaCCM ikiwa ni kukubaliana na kasi ya maendeleo inayoendelea nchini.

Aliongeza kwa kusema kuwa viko vyama vilivyoshiriki katika uchaguzi huo katika Kata ya Msangani vilivyopata mshangao mkubwa baada ya CCM kuvitupa mbali vyama vya ADA - TADEA, CCK, DEMOKRASIA Makini DP, N.R.A, UMD na UPDP.

"Kata ya Mlanzi vyama vilivyoisindikiza CCM ni ACT - Wazalendo, CUF, DEMOKRASIA Makini, N.R.A, UDP, UMD na UPDP ambavyo vimepigwa vibaya," imeeleza taarifa ya Mramba.

Imeongeza kwamba "Wakati huo vyama vilivyoshiriki katika Kata ya Fukayosi huku vikiangukia pua ni CCK, DEMOKRASIA Makini, UDP na UMD, ambapo mwanaCCM Mrisho Some amewaacha mbali kwa kujinyakulia kura 5,883, kati ya 5,960 sawa na asilimia 98.7," ilieleza taarifa hiyo.

"Katika Kata ya Mlanzi mwanaCCM Athumani Mketo amepata kura 1,592 Kati ya halali 1,732 sawa na asilimia 91.9, huku Kata ya Msangani inayopatikana Kibaha Mji Yohana Gunze amepata Kura 5,862 kati ya 5,909 sawa na asilimia 99.20," ilieleza taarifa ya Mwenezi huyo.

Mramba alimalizia kwa kusema kwamba ushidni huo ni ishara njema kuelekea chaguzi zijazo, kwani wananchi wana imani na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

David Mramba, Katibu wa Siasa, Uenezi na Mafunzo Mkoa wa Pwani akifafanua jambo katika moja ya matukio.


No comments