Header Ads

ad

Breaking News

BASHUNGWA ATOA SAA TATU KUREJESHWA MAWASILIANO BARABARA YA MTWARA – MASASI ILIYOKATIKA

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa akiwa na Naibu Waziri Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Deo Ndejembi na viongozi wengine wakikagua na kujionea daraja lililobomoka eneo la Maili Mbili katika barabara ya Mtwara-Mingoyo-Masasi mkoani Mtwara, tarehe 04 Machi 2024

Na Mwandishi Wetu

WAZIRI wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ameelekeza Wakala wa Barabara (TANROADS), kuhakikisha wanarejesha mawasiliano ya barabara iliyokatika eneo la Maili Mbili katika barabara ya Mtwara-Mingoyo-Masasi ndani ya masaa matatu mara baada ya Daraja kusombwa na maji katka eneo hilo.

Bashungwa ametoa agizo hilo tarehe 04 Machi, 2024 Wilayani Masasi akiwa na Naibu Waziri Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Deo Ndejembi, alipofika hapo kujionea adha ya watumiaji wa barabara hiyo waliokwama tangu majira ya asubuhi kutokana na kukatika kwa miundombinu hiyo iliyosababishwa na mvua kubwa zilizonyesha usiku wa jana.

“Nitoe pole kwa wananchi ambao mmepata changamoto kutokana na kukatika kwa mawasiliano ya barabara inayotoka mkoa wa Ruvuma kuelekea mkoa wa Mtwara na Lindi, Natoa saa tatu kwa TANROADS kuhakikisha inakamilisha kujenga barabara ya mbadala ili magari na wananchi waanze kupita,” amesisitiza Bashungwa.

Bashungwa ameeleza kuwa tayari Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshatoa fedha za kumtafuta Mkandarasi atakayeijenga upya barabara hiyo ya Mtwara-Mingoyo-Masasi (km 200) kwa kiwango cha lami kwa kuwa barabara hiyo imekwisha muda wake na imechakaa.

“Wizara ya Ujenzi tumeshapokea maelekezo ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan hadi kufikia mwezi wa sita mkandarasi awe amepatikana na kuanza kazi ya kuijenga upya barabara hii,” amefafanua Bashungwa.

Naye, Naibu Waziri Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Deo Ndejembi amesama kuwa, Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameshatoa kiasi cha Shilingi Bilioni 30 kwa ajili ya dharura za matengenezo ya barabara nchi nzima kupitia Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) na hivyo, wamejipanga vyema kutatua changamoto zozote za mawasiliano ya barabara pindi zinapotokea.

Kwa upande wake Mbunge wa Masasi, Geofrey Mwambe, ameishukuru Serikali na timu nzima ya watalaam wa TANROADS kwa kuchukua hatua za haraka za kuhakikisha wanaanza kazi ya kurejesha mawasiliano ya barabara hiyo na miundombinu mingine ambayo imeathiriwa na mvua katika Wilaya ya Masasi.

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa akizungumza na Wananchi wa Masasi Mara baada ya kukagua na kujionea daraja lililobomoka eneo la Maili Mbili katika barabara ya Mtwara-Mingoyo-Masasi mkoani Mtwara, tarehe 04 Machi 2024

Muonekano wa barabara ya Mtwara-Mingoyo-Masasi katika eneo la Maili Mbili ambapo Daraja lilosombwa na maji kutokana na Mvua za Elnino. 

No comments