Header Ads

ad

Breaking News

ZPC, CRDB ZAJADILI CHANGAMOTO CHA KIUCHUMI NA KIFEDHA

Meneja wa Biashara benki ya CRDB Zanzibar, Abdalla Duchi, akifafanua jambo wakati wamazungumzo baina ya viongozi wa benki hiyo na wa Klabu ya Wandishi wa Habari Zanzibar (ZPC) yaliyofanyika katika ofisi za benki hiyo zilizomo katika jengo la Michezani Mall, Zanzibar


Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

VYOMBO vya habari vimetakiwa kuwa mstari wa mbele kuainisha changamoto za kiuchumi na kifedha zinazoikabili jamii ili zipatiwe ufumbuzi na taasisi za kifedha.

Akizungumza katika kikao maalum na uongozi wa Klabu ya Waandishi wa Habari Zanzibar (ZPC), Meneja wa Biashara wa Benki ya CRDB Zanzibar, Abdalla Duchi, alisema kuna changamoto ya uhaba wa elimu ya kifedha katika jamii, jambo linalosababisha kuzorota kwa shughuli za maendeleo.

Alieleza kuwa, pamoja na juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuhimiza ujasiriamali na uwezeshaji wa wananchi kiuchumi, bado elimu jumuishi ya kifedha inahitajika ili kuwe na matokeo chanya. 

Aidha, Duchi aliahidi kuendelea kutumia vyombo vya habari na waandishi wa habari kueleza shughuli zinazofanywa na benki hiyo, hivyo aliwataka wanahabari kuendelea kushirikiana nao kusambaza elimu kwa umma.

“Niwapongeze kwa kazi kubwa mnayoifanya ya kuelimisha  jamii juu ya masuala yanayohusu ustawi wao kiuchumi na kijamii, jambo linalopaswa kufanywa kwa kasi zaidi kwa ushirikiano tunayoyaanzisha leo,” alieleza Duchi.

Alifafanua kuwa, benki hiyo ina huduma mbalimbali zinazowagusa wananchi wa ngazi zote ikiwemo akaunti ya Kiislamu Al Barakah na bima mbalimbali zinazoweza kuwanufaisha wateja pindi wanapopatwa na majanga, misiba au ulemavu.

“Miongoni mwa bidhaa tulizonazo ni bima ya mtu mmoja mmoja na ya vikundi ambayo hutoa mafao yasiyopungua shilingi milioni moja kwa ajali, kifo, majanga, ulemavu wa kudumu, elimu na kadhalika kwa gharama inayoanzia shilingi 1,000,” alieeleza meneja huyo.

Awali, Mwenyekiti wa ZPC, Abdallah Mfaume, alieleza lengo la ziara hiyo inayofanyika kila mwanzo wa mwaka ni kuimarisha mahusiano baina ya klabu na wadau wake.

Alieleza kuwa, ZPC ni taasisi mwamvuli wa waandishi wa habari wanaoishi na kufanya kazi katika vyombo mbali vya habari vya ndani na nje ya Zanzibar ikiwa na jukumu la kuwaunganisha kitaaluma ili kujenga weledi wanachama wake kupitia shughuli mbalimbali.

Aliongeza kuwa, katika kutekeleza majukumu yake, ZPC hutoa mafunzo yanayowajengea uwezo wanachama wake na waandishi wa habari hivyo, kukua kwa mahusiano baina yake na benki hiyo kutaongeza uelewa wa jamii na wanachama wa klabu juu ya masuala ya kifedha na njia za kujiongezea kipato.

“Tumekuwa na utaratibu huu kila mwaka lengo ni kukumbushana juu ya namna bora ya kufanya kazi pamoja kwa malengo ya kukuza ufanisi wa malengo tuliyojiwekea kupitia shughuli za taasisi zetu,” alieleza Mfaume.

Kwa upande wake Meneja Biashara wa Benki ya Kiislamu wa CRDB Zanzibar, Anwar Said, alieleza kufurahishwa kwake na ziara ya viongozi hao na kuongeza kuwa, benki hiyo inaendelea kutoa huduma mbalimbali kupitia akaunti ya Al Barakah tangu ilipoanzishwa Novemba 2021.

“Katika benki ya Kiislamu kuna huduma na bidhaa nyingi sana ikilinganishwa na benki nyingine ambazo tutahitaji msaada wa vyombo vya habari kuujulisha umma,” alieleza Anwar.

Katika ziara hiyo, Mfaume aliambatana na Katibu Mkuu wa ZPC, Mwinyimvua Nzukwi, Mjumbe wa Kamati Tendaji, Zuhura Msabaha na Mratibu, Mgeni Hamad, mbali ya Duchi na Anwar, CRDB iliwakilishwa na Afisa Biashara na Mauzo, Lucy Mbuya na Afisa Ubora wa huduma, Zainab Ally.

Meneja wa Biashara benki ya CRDB Zanzibar, Abdalla Duchi (kushoto) akizungumza na viongozi wa Klabu ya Waandishi wa Habari Zanzibar (ZPC), walipofanya ziara ya kukuza mahusiano katika ofisi za benki hiyo zilizomo katika jengo la Michezani Mall, Zanzibar.
Mjumbe wa Kamati Tendaji wa Klabu ya Waandishi wa Habari Zanzibar (ZPC), zuhura msabah akizungumza jambo wakati viongozi wa klabu hiyo walipofanya mazungumzo ya kukuza mahusiano na uongozi wa benki ya CRDB katika ofisi za benki hiyo zilizomo katika jengo la Michezani Mall, Zanzibar. Kushoti ni katibu mkuu wa ZPC, Mwinyimvua Nzukwi.

No comments