Header Ads

ad

Breaking News

WAZIRI MKUU MGENI RASMI BONANZA LA WAANDISHI WA HABARI JUMAMOSI FEBRUARI 10,2024

Waziri Mkuu Kassima Majaliwa
Na Mwandishi Wetu

WAZIRI Mkuu Kassima Majaliwa ameridhia kuwa mgeni rasmi katika Bonanza la Waandishi wa Habari Tanzania linaloandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA).

Bonanza hilo limepangwa kufanyika kesho Jumamosi Februari 10, 2024, eneo la Msasani Beach Club jijini Dar es Salaam kuanzia saa 2:00 asubuhi.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa TASWA, Alfred Lucas Mapunda, amesema kwa muda mrefu mabonanza ya waandishi wa habari yalisimama, lakini walipoingia madarakani, waliahidi kuyarejesha.

Amesema baada ya kazi nyingi za kuhabarisha watanzania, wanatakiwa kupata siku moja ya kukutana na kubadilishana mawazo na kufurahi pamoja.

Mapunda amesema kuwa, Waziri Mkuu Majaliwa atawasili eneo la Msasani Beach Club kuanzia saa nane mchana, katika bonanza hilo litakalowahusisha waandishi wa habari pamoja na wafanyakazi wa kada mbalimbali kwenye vyombo vya habari.

Ametaja michezo itakayoshindaniwa ni mpira wa miguu, pete, pool table, riadha, kukimbia na magunia, kurusha tufe, kuruka kamba, draft, bao, karata na rede.

Katibu Mkuu huyo amesema kuwa, TASWA watatumia bonanza hilo kuzindua tuzo za mwanamichezo bora, ambapo mwanamichezo bora wa Januari atatangaza.

Amesema kuwa, kamati ya tuzo chini ya Mwenyekiti Jemedari Said Kazumari iliundwa na tayari ilianza kazi hiyo. Jemedari ni mchambuzi wa michezo wa Kituo cha redio cha EFM, pia ni mchezaji wa zamani wa mpira wa miguu.

Ameongeza kuwa, TASWA itatumia bonanza hilo kuzindua kamati zake ilizoteua kwa lengo la kusaidia masuala mbalimbali ya kiutendaji ambazo ni Kamati ya Mafunzo na Maadili itakayoongozwa na Dkt.Egbert Mkoko, Kamati ya Fedha na Mipango itakuwa chini ya CPA Shija Richard na Kamati ya Ukaguzi wa Hesabu chini ya Baraka Katemba.

Kamati nyingine ni ya Katiba itakayokuwa chini ya Boniface Wambura na Kamati ya Wanawake na Michezo itaongozwa na Timzoo Kalugira.

Mapunda amesema kuwa, wanatarajia kuwa na wageni zaidi ya 2,000 watakaoshiriki bonanza na uzinduzi wa kamati hizo, miongoni mwao ni viongozi mbalimbali wa vyama vya michezo, wachezaji nguli wa zamani na wadau wa masuala ya habari nchini. 

Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Tanzania (TASWA), Amir Mhando

Katibu Mkuu wa Chama cha Waandishi wa Habari Tanzania (TASWA), Alfred Lucas Mapunda

Mwenyekiti Kamati ya Tuzo, Jemedari Said Kazumari
Mwenyekiti Kamati ya Katiba, Boniface Wambura

Mwenyekiti Kamati ya Mafunzo na Maadili, Dkt.Egbert Mkoko
Mwenyekiti wa Kamati ya Wanawake na Michezo, Timzoo Kalugira
Mwenyekiti Kamati ya Fedha na Mipango, CPA Shija Richard

No comments