Header Ads

ad

Breaking News

WAZIRI MKUU ASEMA SERIKALI INATHAMINI MCHANGO WA SEKTA BINAFSI


Na Mwandishi Wetu

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan imeendelea kuthamini na kutambua mchango wa sekta binafsi katika kuimarisha ustawi wa jamii ya watanzania.

Ameyasema hayo leo Jumapili Februari 18, 2024, alipomwakilisha Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kufungua Hospitali ya Saifee Tanzania jijini Dar es Salaam. akiweka wazi kuwa, sekta binafsi zinaunga mkono jitihada za Serikali katika kutoa huduma mbalimbali kwa wananchi.

Waziri Mkuu amesema mchango wa sekta binafsi katika eneo la kutoa huduma kwa wananchi ni mkubwa na unadhihirika kupitia huduma mbalimbali wanazozitoa ambazo ni huduma za afya, elimu, mawasiliano na maji.

Amesema kwa upande wa sekta ya Afya, Serikali inatekeleza kwa vitendo Sera ya Ubia kwa kufanya kazi pamoja na baadhi ya vituo vya kutolea huduma ya afya vinavyomilikiwa na sekta binafsi.

Waziri Mkuu amesema amefarijika na huduma zinazotolewa na hospitali hiyo zikiwemo za upasuaji wa moyo, mgongo, ubongo kwa kutumia teknolojia za kisasa za kitabibu na pia kuweka vipandikizi (implants) kwenye matibabu ya mifupa.

“Ni matumaini yangu kuwa Taasisi ya Saifee itasaidia kupunguza rufaa za wagonjwa kwenda nje ya nchi na kupunguza gharama kwa wananchi na serikali, hivyo uwekezaji huu una manufaa makubwa sana kwa taifa.”

Amesema Hospitali ya Saifee na nyingine kama hizo nchini, ni nyenzo muhimu katika kuiharakisha Tanzania kuelekea kuwa kitovu cha utalii tiba katika ukanda wa Afrika mashariki, kati na kusini na visiwa vya Bahari ya Hindi.

Naye, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema wataendelea kuwa wabunifu na kushirikiana na sekta binafsi katika kuboresha huduma za afya kwa watanzania., na kwamba kuna vituo zaidi ya 12,000 vya kutolea huduma za afya kati yake asilimia 60 ni vya serikali na asilimia 40 vinamilikiwa na sekta binafsi.

Waziri Ummy ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa watanzania kuzingatia ulaji unaofaa pamoja na kufanya mazoezi ili kuepukana na magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo ya moyo na kisukari.

No comments