Header Ads

ad

Breaking News

WATANZANIA TUMUENZI HAYATI EDWAED NGOYAI LOWASSA-RAIS DKT.SAMIA

Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan

 Na Sophia Kingimali

RAIS Dkt.Samia Suluhu Hassan amewaasa wananchi kumuenzi hayati Edward Ngoyai Lowassa kwa kufanya kazi kwa bidii na kuyaishi yote mazuri aliyoyafanya katika kipindi chake cha utumishi.

Hayo ameyasema leo Februari 17,2024 wakati akiongoza mazishi ya Lowassa katika Kijiji cha Ngarash wilayani Monduli mkoani Arusha.

Amesema hayati Lowassa amekuwa mtu wa kujituma kwa kufanyakazi kwa bidii na kwa weledi huku akiwa na msimamo katika kuyasimamia aliyoyaanzisha.

Rais Dkt.Samia Amesema atamkumbuka kwa mambo matatu ambayo yamekuwa funzo kwa taifa, ushupavu, ustahimilivu na ulezi.

“Haya mambo matatu yamekuwa funzo kwa taifa kwani aliyafanya bila kuyumba inabidi tuyaenzi kwa kufanyakazi kwa didii bila kusukumwa na wanaotuongoza,”amesema.

Amesema ustahimilivu aliouonesha Lowassa katika nyanja zote hasa katika siasa na hii imewezzesha hata uwepo wa 4R ambazo zinaendelea kufanyakazi ikiwemo maridhiano.

Sambamba na hayo amesema atakumbukwa kwa usimamizi wake wa miradi mikubwa ya maji ambayo imekuwa na manufaa makubwa kwa taifa.

“Kwa haya somo tunalipata tukipewa dhamana za uongozi na kuaminika katika nafasi mbalimbali za serikali lazima tuwe na uthubutu na ubunifu pamoja na kusimamia na kutekeleza kwa weledi bila kuyumbishwa,”amesema.

Akizungumzia suala la ulezi, amesema Lowassa amelea vijana wengi na kuwafundisha katika ngazi mbalimbali na hakuacha ulezi huo hata alipokuwa nje ya utumishi, aliendelea kulea.

Amesema katika suala la elimu alihamasisha ujenzi wa shule za sekondari za kata ambapo serikali ilijenga shule hizo na hadi sasa inaziendeleza, ambapo kutoka shule 828 mwaka 2004 hadi shule 4,578 mwaka 2023.

Sambamba na hayo, ametoa rai kwa wanasiasa nchini kuendelea kufanya siasa za kistaarabu na kustahimiliana kwa kuweka maslahi ya nchi mbele.

Kwa upande wake Waziri Mkuu ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya kitaifa ya kuratibu mazishi, Kassim Majaliwa, amemshukuru Rais kwa usimamizi na ushari wake katika kuhakikisha hayati Edward Lowassa anazikwa kwa taratibu zote za kiserikali.

Kwa upande wake Spika wa Bunge, Dkt. Tulia Akson ametoa rai kwa wananchi kuanza kujitafakari katika safari ya maisha, wanatarajia kuacha alama gani ili pindi watakapoaga dunia waache funzo na alama kama alivyofanya Lowassa.

Wakizungumza kwa niaba ya familia watoto wa marehemu Lowassa ambaye ni Richard Lowassa na Fredrick Lowassa, wamewashukuru wote waliojitokeza kuwafariji na kuwasaidia katika kipindi chote walichokuwa wakimuuguza baba yao hadi umauti unamkuta.

Naye, Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mboye amesema historia ya Lowassa haitasahaulika ndani ya chama kwani ameweza kusaidia kupata ongezeko kubwa la wabunge wa upinzani bungeni na madiwani wengi wakati alipogombea urais katika chama hicho.

                                        (Fullshangwe)

No comments