Header Ads

ad

Breaking News

Usawa wa kijinsia waweka salama shoroba

Na Selemani Msuya

UZINGATIAJI usawa wa kijinsia kwenye usimamizi wa shoroba saba ambazo zipo kwenye Mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili umewezesha shoroba hizo kuwa salama na endelevu.

Hayo yamesemwa na Ofisa Ufuatiliaji na Tathmini wa mradi huo, Doroth Nyoni wakati akitoa mada kwa waandishi wa habari wanachama wa Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira (JET), kuhusu umuhimu wa kuzingatia jinsia kwenye utekelezaji wa miradi ambayo inahusu uhifadhi na mazingira.

Nyoni amesema Mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili unaotekelezwa katika shoroba saba za Kwakuchinja, Amani na Nilo, Udzungwa na Hifadhi ya Nyerere, Ruaha Rungwa na Katavi, Ruaha Rungwa na Inyonga na Kigosi Moyowosi- Burigi Chato umezingatia usawa wa kijinsia kwa kuwezesha makundi yote kushiriki katika shughuli za kiuchumi.

Amesema katika ufuatiliaji na tathmini ambayo wamefanya wameona ushirikishwaji wa makundi yote wakiwemo wanawake, vijana, watoto, walemavu na wengine, inasababisha rasilimali zote zinzopatikana kwenye hifadhi kuwa salama, kwa kila kila mwana jamii ni mnufaika.

“Katika kuhakikisha fursa zinazopatikana kwenye uhifadhi zinakuwa endelevu ni lazima kuwepo uchambuzi wa kijinsia unazingatiwa kwani kufanya hivyo kunasababisha hifadhi kutunzwa na kuwa endelevu,” amesema.

Amesema Mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili umeshirikiana na wananchi waliopo karibu na shoroba kuhakikisha wananufaika na fursa zilizopo, ikiwemo kuanzisha vikoba, ujasiriamali na nyingine.

Aidha, Nyoni amesema katika kusimamia misingi ya usawa wa kijinsia wamehakikisha makundi yote yanashiriki katika uongozi ili wawe sehemu ya maamuzi kuhusu rasilimali zao.

Ofisa huyo amesema taarifa za kitafiti zinaonesha wanawake na vijana hasa wakike ndio wanaathirika na uharibifu wa mazingira, hivyo uamuzi wa kuzingatia usawa wa kijinsia utawanufaisha zaidi.

Amesema iwapo kampeni ya uhifadhi na utunzaji wa mazingira itaachiwa kundi moja ni wazi kuwa hatari itakuwa kubwa, hivyo wao USAID Tuhifadhi Maliasili wamehakikisha jinsia inapewa nafasi.

“Kwenye shoroba ya Amani Nilo wilayani Muheza mkoani Tanga tumefanya kampeni kuanzia mashuleni, hali ambayo imewezesha watoto wa shule kutambua faida za hifadhi na hivyo kulizinda. Lakini pia kule Kwakuchinja mkoani Manyara kuna Program ya Twende Porini nayo imefanikiwa kwa kuwa imejikita kwenye muktadha wa kijinsia,” amesema.

Ofisa huyo anasema awali wakati mradi ukiwa haujashirikisha makundi yote, kulikuwa na hali ya baadhi kuona kutengwa, ila kwa utaratibu huu wa kijinsia hali imekuwa nzuri.

Aidha, Nyoni amesema katika baadhi ya shoroba wananchi wamepata elimu kuhusu matuzi bora ya ardhi, hivyo kuanza kunufaika na ardhi yao.

“Tumezingatia misingi ya kuwezesha uhifadhi ambao wananchi wananufaika na rasilimali hiyo ya shoroba. Mfano GFP amewezesha wakulima wa viungo wilayani Muheza kunufaika,” amesema.

Amesema kutokana na matokeo chanya ambayo GFP na wakulima wamefanya, umuhimu wa sekta binafsi kwenye uhifadhi umeweza kuonekana.

Pia amesemaa mradi huo umwezesha uanzishwaji wa vikoba na ujasiriamali wa aina mbalimbali kama ufugaji nyuki na nyingine.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa JET, Dkt. Ellen Otaru amesema uamuzi wa Mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili kuzingatia misngi ya kijinsia unapaswa kuungwa mkono kwa kuwa ndio mwelekeo wa dunia.

Dkt. Utaru amesema dunia kwa sasa inapigania usawa wa kijinsia, hivyo ni muhimu waandishi wa habari kueleza kwa kina kuhusu miradi ambayo inazingatia hayo.

“Kusema kweli mimi ni mdau wa usawa wa kijinsia, hivyo uamuzi wa mradi kuzingatia hili umenigusa mimi, lakini na dunia nzima,” amesema.




No comments