Header Ads

ad

Breaking News

NMB YAKABIDHI MADAWATI, MABATI SHULE TANO ZA WILAYA YA RORYA

Mkuu wa Wilaya ya Rorya mkoani Mara, Juma Chikoka (kushoto), akipokea sehemu ya msaada wa madawati 150 kwa ajili ya Shule ya Msingi Minigo kutoka kwa Kaimu Meneja wa NMB Kanda ya Ziwa, Hamadan Silliah, ambapo NMB pia imetoa madawati 100 kwa shule ya Msingi Nyanduru,mabati 168 kwa Shule ya Girango, mabati 100 kwa Shule ya Sekondari Prof Sarungi  na ukarabati wa madarasa 7 ya shule ya msingi Minigo, msaada wote huo unagharimu jumla ya shilingi milioni 84.

 

Na Mwandishi Wetu

 

BENKI ya NMB imetoa msaada wenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 80 ukiwa ni madawati 250 na mabati 368 kwa shule tano za Halmashauri ya Wilaya ya Rorya mkoani Mara. 


Shule zilizonufaika na msaada huo ni Shule ya Msingi Minigo iliyopata madawati 100 na Shule ya Msingi ya Nyanduru madawati 100. 

 

Shule zilizopokea mabati ni Shule ya Msingi Gilango mabati 168, Shule ya Msingi Kiamwani mabati 100, mbao na misumari, wakati Shule ya Sekondari Profesa Philemon Sarungi imejengewa hosteli mbili na kupewa shilingi milioni 15.

 

Mbali na misaada hiyo, benki hiyo imefanya ukarabati wa madarasa saba katika Shule ya Msingi Minigo na kumalizia ujenzi wa darasa moja katika shule hiyo.

 

Akizunguzmza wakati wa hafla fupi ya makabidhiano iliyofanyika jana katika Shule ya Msingi Minigo,  Mkuu wa Wilaya ya Rorya Juma Chikoka ameishukuru Benki ya NMB kwa kusaidia uboreshaji  wa miundombinu ya elimu katika wilayani Rorya. 


Chikoka aliweka wazi kuwa, Wilaya ya Rorya inakabiliwa na changamoto kubwa sana ya uchakavu wa miundombinu ya elimu.

 

"Misaada mbalimbali ya elimu tunayopokea kutoka NMB imetusaidia shule zetu tatu za sekondari kuingia katika kumi bora ya Mkoa wa Mara katika mitihani ya Taifa (NECTA) ya kidato cha nne," amesema.

 

Mkuu wa wilaya hiyo ameiomba Benki ya NMB kufikiria kuwa mdhamini wa tuzo za elimu wilayani Rorya zenye lengo la kusaidia shule kufanya vizuri katika mitihani ya kitaifa.

 

Chikoka ameiomba Benki ya NMB iwasaidie kutoa mikopo kwa wavuvi ili waweze kutumia ufugaji wa vizimba  na mikopo kwa wakulima waweze kutumia kilimo cha umwagiliaji.

 

Naye, Kaimu Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Ziwa, Hamadan Sillia amesema benki yao itaendelea kusaidia jamii kwani, kushiriki katika kutatua changamoto mbalimbali zinazokabili jamii wanazohudumia ni moja ya kipaumbele cha benki hiyo.

 

“Ni faraja kwa Benki ya NMB kuona tunashirikishwa katika masuala muhimu kama utatuzi wa changamoto zinazoikabili jamii yetu, hii inaonesha ni namna gani mnaitambua Benki ya NMB kama sehemu ya jamii yetu, ni heshima na tunashukuru sana,” alisema Hamadan

 

Kaimu Meneja wa Kanda ambaye pia ni Meneja wa Benki hiyo Tawi la Kenyata Road jijini Mwanza, amewaomba walimu na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya kuendelea kutumia huduma mbalimbali za Benki ya NMB ikiwemo ufunguaji wa akaunti za NMB Pesa ambazo hufunguliwa kwa shilingi 1,000 tu.

 

Kwa upande wake Mkuu wa Shule ya Msingi Minigo, Mwalimu Joseph Onyango amesema NMB imewasaidia kuongeza mahudhurio ya wanafunzi kutokana na uboreshaji wa madarasa na wanategemea pia ongezeko la ufaulu.

No comments