Header Ads

ad

Breaking News

MKUTANO WA KIMATAIFA WA MAGONJWA YA MOYO KUFANYIKA ZANZIBAR

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Dkt. Peter Kisenge akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kongamano la wataalamu wa afya leo kabla ya mkutano wa magonjwa ya moyo utakaofanyika kesho katika Hoteli ya Golden Tulip iliyopo Zanzibar.

Na Mwandishi Maalumu - Zanzibar

TAASISI ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), itafanya mkutano wa kimataifa wa magonjwa ya moyo kwa wataalamu wa afya nchini kuwapa mbinu mbalimbali za kutambua wagonjwa wa moyo.

Mkutano huo ulioanza leo na kongamano la kutoa huduma mbalimbali za magonjwa ya moyo kwa wataalamu wa afya utafanyika tarehe 9 na 10 katika Hotel ya Golden Tulip iliyopo Zanzibar.

Akizungumza na waandishi wa habari leo katika Hotel ya Verde iliyopo Zanzibar  Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Peter Kisenge alisema lengo la mkutano huo ni kuwawezesha madaktari wazawa wa hospitali zote kuanzia ngazi za chini hadi taifa kubadilishana mawazo na uzoefu kutoka kwa wataalamu wa JKCI na wenzao wa nje ya nchi.

Dkt. Kisenge alisema mkutano huo utawawezesha watu wa nchi za Afrika kuielewa Taasisi hiyo na huduma zinazotolewa jambo ambalo litapelekea kupunguza gharama za kupeleka wagonjwa nje ya nchi.

“Kutokana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia mkutano huu unaenda sambamba na mafunzo maalumu kwa vitendo kwa madaktari wa upasuaji juu ya mambo mbalimbali yakiwemo ya uvunaji wa mishipa ya moyo, jinsi ya kumhudumia mgonjwa mahututi wakati wa kongamano kabla ya mkutano wa magonjwa ya moyo”, alisema Dkt. Kisenge Dkt. Kisenge alisema wawakilishi zaidi ya 500 ambao ni wazawa na 40 kutoka nchi mbalimbali wanatarajiwa kushiriki katika mkutano huo ikiwemo madaktari bingwa wa magonjwa ya moyo na wauguzi wanaotoa huduma kwa wagonjwa hao.

Aidha Dkt. Kisenge alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwekeza vifaa na rasilimali watu katika Taasisi hiyo jambo ambalo limepelekea kuwa kimbilio la wagonjwa wa moyo kutoka nchi mbalimbali.


Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Upasuaji wa moyo kwa watoto Dkt.Godwin Sharau alisema katika mafunzo hayo watahakikisha wanagusa kile eneo linalohusiana na magonjwa ya moyo kutimiza lengo la mkutano.

Dkt. Godwin alisema wataalamu wa afya walioshiriki watapata nafasi ya kujifunza changamoto za matibabu ya moyo, maendeleo mapya juu ya ugonjwa wa moyo, upasuaji kwa kutumia tundu dogo, kuzibua mishipa ya damu iliyoziba pamoja na kurekebisha mishipa ya damu iliyokinzana.

“Kwa wagonjwa wanaofika katika Taasisi yetu hadi sasa tunao uwezo wa kuwahudumia lakini wapo wale ambao wana magonjwa ya moyo na hawafiki katika taasisi yetu kwaajili ya matibabu ndio maana tunatoa mafunzo haya kwa wenzetu kuwasaidia wale ambao hawafiki katika Taasisi kupata matibabu," alisema Dkt. Godwin.

Naye Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya wadhamini ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete, Asha Izina alisema ili kuhakikisha teknolojia zinatumika kwa usahihi ni lazima kuwe na watu wenye uwezo wa kuzitumia ili kuhakikisha huduma bora zinazotolewa kwa walengwa.

“Mkutano wetu utazungumzia huduma za moyo katika nchi za Afrika sambamba na mafunzo mbalimbali yatakayowasilishwa na madaktari bingwa kutoka ndani na nje ya nchi kuwasaidia wataalamu wa afya kutoa huduma bora na kuijengea uelewa jamii kujua viashiria vya magonjwa ya moyo,” alisema Asha.

Mkutano wa kimataifa wa magonjwa ya moyo wenye kauli mbiu 'Maendeleo ya matibabu ya moyo katika nchi za Afrika' utafunguliwa rasmi kesho na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Isdor Mpango na kufungwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi Jumamosi Februari 1, 2024.

Daktari bingwa wa upasuaji wa moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Godwin Sharau akielezea mada zitakazotolewa katika mkutano wa magonjwa ya moyo utakaofanyika kesho katika Hoteli ya Golden Tulip iliyopo Zanzibar.

Wataalamu wa afya kutoka Hospitali mbalimbali nchini wakifanya mazoezi kwa vitendo ya namna ya kuunganisha mishipa ya damu wakati wa kongamano leo kabla ya mkutano wa magonjwa ya moyo utakaofanyika kesho katika Hoteli ya Golden Tulip iliyopo Zanzibar. 

Wataalamu wa afya kutoka Hospitali mbalimbali nchini wakifanya mazoezi kwa vitendo ya namna ya kuunganisha mishipa ya damu wakati wa kongamano leo kabla ya mkutano wa magonjwa ya moyo utakaofanyika kesho katika Hoteli ya Golden Tulip iliyopo Zanzibar. 

Wataalamu wa afya kutoka Hospitali mbalimbali nchini wakifanya mazoezi kwa vitendo ya namna ya kumhudumia mgonjwa wa dharura wakati wa kongamano leo kabla ya mkutano wa magonjwa ya moyo utakaofanyika kesho katika Hoteli ya Golden Tulip iliyopo Zanzibar. PICHA ZOTE NA JKCI

No comments