Header Ads

ad

Breaking News

JKCI YAFANYIKA KLINIKI YA MATIBABU YA MOYO MKOANI GEITA

 

Daktari wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Marsia Tillya  akiandika taarifa mara baada ya kusoma majibu ya mgonjwa aliyefika katika kliniki maalumu ya siku tano ya uchunguzi na matibabu ya moyo iliyofanyika  katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato (CZRH) iliyopo mkoani Geita. Jumla ya wagonjwa 312 wamepata huduma ya uchunguzi na matibabu katika kliniki hiyo iliyomalizika Februari 23,2024.

Na Mwandishi Maalumu - Geita

WATAALAM wa afya wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wameweka kliniki maalumu ya matibabu ya kibingwa ya magonjwa ya moyo kwa wagonjwa wanaohitaji huduma hiyo mkoani Geita.

Kliniki hiyo maalumu ya wiki moja imefanyika katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato (CZRH) na kumalizika leo Februari 23,2024 kwa kufanywa na wataalamu wa afya wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao wa CZRH ambapo wagonjwa 312 wamefanyiwa vipimo vya moyo na kupatiwa matibabu.

Kliniki hiyo inatarajiwa kufanyika mara moja kila mwezi lengo likiwa kuwajengea uwezo wataalamu wa CZRH pamoja na kuiwezesha Hospitali hiyo kutoa huduma za kibingwa za uchunguzi na matibabu ya moyo kwa wagonjwa wa moyo waliopo kanda ya ziwa.

Akizungumzia kliniki hiyo Daktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Williams Ramadhan alisema kati ya watu 312 waliopatiwa huduma watu 13 wamekutwa na matatizo ya kuziba kwa mishipa ya moyo, watu 12 wamekutwa na matundu kwenye moyo, na watu 14 wamekutwa na matatizo ya umeme wa moyo (arrhythmias).

“Watu 55 tumewakuta na tatizo la shinikizo la juu la damu, watu saba wana magonjwa ya kuziba kwa mishipa ya damu ya miguu, watu sita wana vidonda sugu kwasababu ya mishipa ya miguu kutanuka na kuwa na shinikizo la juu la damu, na watu wawili tumewakuta na tatizo la kutanuka kwa mshipa mkubwa wa aorta,” alisema Dkt. Ramadhan

Dkt. Ramadhan alisema wagonjwa 51 wamepewa rufaa kufika JKCI kwaajili ya matibabu zaidi ambapo 13 watahitaji upasuaji wa kuzibua na kupandikiza mishipa ya damu, wagonjwa 14 watahitaji kufungwa vifaa maalumu kurekebisha mfumo wa umeme wa moyo, wagonjwa 11 kufanyiwa upasuaji wa mishipa ya miguu, wagonjwa 12 kufanyiwa upasuaji wa kuziba matundu ya moyo na mgonjwa mmoja kupandikizwa mshipa mwingine wa bandia.

Kwa upande wake Mratibu wa huduma za afya Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato (CZRH) Dkt. Osward Lyaba alisema Hospitali hiyo ilianzisha kliniki ya magonjwa ya moyo miezi sita iliyopita ambayo ilizinduliwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) marehemu Prof. William Mahalu.

“Katika kuendeleza huduma za kliniki hii wataalamu wa afya kutoka JKCI wameshirikiana nasi kwa kuweka kambi ya wiki moja katika Hospitali yetu ikiwa ni sehemu ya kutujengea uwezo na kutoa huduma kwa wagonjwa wa moyo wanaohitaji huduma za kibingwa,” alisema Dkt. Osward

Dkt. Osward alisema kambi hiyo imehusisha wataalamu wa afya mabingwa wa matibabu ya moyo, mabingwa wa upasuaji wa moyo na wataalamu wa vipimo vya magonjwa ya moyo.

"Mwitikio umekuwa mkubwa kwani kwa siku tatu za mwanzo tumeweza kuona takribani watu 230 waliojitokeza kufanyiwa uchunguzi na kupatiwa matibabu ya moyo na wale waliohitaji huduma zaidi wamepewa rufaa kufika JKCI kwaajili ya matibabu zaidi,” alisema Osward.

Fundi sanifu wa moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), Jasmine Keria akimpima kipimo cha kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (Echocardiography – ECHO) mkazi wa Geita aliyefika katika kliniki maalumu ya siku tano ya uchunguzi na matibabu ya moyo iliyofanywa  na wataalamu wa JKCI kwa kushirikiana na wenzao wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato (CZRH) iliyopo mkoani Geita.

wakazi wa Geita wakiwa katika foleni ya kusubiri kupata huduma katika kliniki maalumu ya siku tano ya uchunguzi na matibabu ya moyo iliyofanyika katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato (CZRH) iliyopo mkoani Geita. Jumla ya wagonjwa 312 wamepata huduma ya uchunguzi na matibabu katika kliniki hiyo iliyomalizika Februari 23,2024.




No comments