Header Ads

ad

Breaking News

DKT.BITEKO ASHUHUDIA UTIAJI SAINI MKATABA WA UMEME KIGOMA

                                   

NAIBU  Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko akishuhudia utiaji saini mkataba wa ujenzi wa mradi wa uzalishaji umeme wa megawati 49.5 kwa nguvu ya maji katika Mto Malagarasi mkoani Kigoma. Wanaosaini ni Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Mhandisi Gissima Nyamo-Hanga (kulia) na Meneja Mradi kutoka Kampuni ya Dongfang Electric International ya nchini China, Ni Zhihong, hafla hiyo imefanyika leo Februari 8,2024 jijini Dodoma.


Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amesema Serikali imeamua kutekeleza miradi mipya uzalishaji wa umeme, badala ya kutegemea vyanzo vya zamani ili kuendana na ongezeko kubwa la mahitaji ya umeme nchini.

Dkt. Biteko amesema hayo leo Februari 8,2024 jijini Dodoma baada ya kushuhudia utiaji saini mkataba wa ujenzi wa mradi wa uzalishaji umeme wa megawati 49.5 wa nguvu ya maji katika Mto Malagarasi mkoani Kigoma. 

Mkataba huo umesainiwa na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Kampuni ya Dongfang Electric International kutoka Jamhuri ya Watu wa China.

“Lazima tuwe na vyanzo vingi na vipya vya umeme, kiu na njaa ya umeme tuliyonayo inatufanya tufikirie namna ya kupata umeme kwa haraka, mahitaji ya umeme yameongezeka sana, lakini vyanzo ni vilevile vya miaka mingi, mfano Bwawa la Mtera lilijengwa  mwaka 1980, Kidatu mwaka 1975, Kihansi mwaka 2000, Pangani 1995, Hale 1968, Nyumba ya Mungu 1964 na mwaka 2019, baada ya gesi kuanza uzalishaji umeme, mahitaji yalikuwa pungufu kuliko uzalishaji lakini sasa mahitaji ni makubwa kuliko vyanzo,” amesema Dkt. Biteko

Amesema  kutokana na mahitaji ya umeme kuwa makubwa kuliko vyanzo vyake, Serikali inaendelea kuongeza vyanzo vipya ikiwemo mradi wa Malagarasi ambao utekelezaji wake utachukuwa miezi 42 na utekelezaji wa mradi wa Julius Nyerere (JNHPP), ambao kwa sasa umekamilika kwa asilimia 96 na unatarajia kuingiza umeme kwenye gridi ya Taifa mwezi huu.

Ameeleza kuwa, utekelezaji wa miradi hiyo mipya ni maagizo ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa, vyanzo vyote vilivyopo vianze kujengwa sasa ikiwemo miradi ya umeme ya Kakono, Kikonge, Luhudji, Rumakali na miradi ya gesi mkoani Mtwara ili kuwa na umeme wa kutosha kwa mahitaji ya nchi.

Ili kuwa na umeme kutoka vyanzo mchanganyiko, Dkt, Biteko amesema kuwa, ametoa maagizo kwa watendaji wa wizara na TANESCO kuhakikisha wanabadilika na kuboresha huduma zao kwa wananchi na kuwezesha uwekezaji katika miradi ya kuzalisha umeme kwa nguvu ya jua na upepo.

Dkt. Biteko amesema pamoja na mradi wa Mto Malagarasi, kuna miradi mingine mitatu ikiwemo usafirishaji wa umeme kutoka Nyakanazi hadi Kigoma (kV 400), Tabora hadi Kigoma (kV 132), kuongezwa uwezo wa kituo cha umeme wa jua cha Kigoma kutoka megawati tano hadi megawati 10

Dkt. Biteko amesema kuwa, uboreshaji wa miundombinu nchi nzima unaendelea na inajumuisha ujenzi wa vituo vya kupoza umeme katika maeneo mbalimbali nchini na kwa kuanzia vinajengwa vituo 24 katika maeneo ya kimkakati ili kutengemaza gridi
ya Taifa.

Ameishukuru Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) kwa kutoa mkopo wa masharti nafuu wa kiasi cha dola za Marekani milioni 140 ili kutekeleza mradi wa Malagarasi, ambapo Serikali ya Tanzania imetoa dola za Marekani milioni 4.14. 


Ameongeza kwamba, benki hiyo imeendelea kuiunga mkono Serikali katika miradi mbalimbali nchini.

Amewaagiza wakandarasi kutekeleza mradi huo kwa haraka na ufanisi kama ilivyo kwa mradi wa umeme wa JNHPP ili wananchi wa Kigoma na nchi nzima wapate umeme wa uhakika.

Mradi  wa Malagarasi unahusisha ujenzi wa eneo la kufua umeme wa maji, njia za kupitisha maji, jumba la mitambo ya umeme, kituo cha kupokea na kusafirisha umeme, ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa kV 132 ambayo itaunganishwa kwenye Gridi ya Taifa kupitia kituo cha Kidahwe- Kigoma na  kuunganisha umeme kwenye vijiji saba vitakavyopitiwa na mradi.

Naye, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Wenye Ulemavu, Profesa Joyce Ndalichako amesema mbali na uzalishaji wa megawati 49.5 kuongeza kiwango cha umeme katika gridi ya Taifa, hatua hiyo itachochea uanzishaji na ukuaji wa viwanda katika Mkoa wa Kigoma.

Amesema kuwa, kupitia hali hiyo, ajira zitaongezeka na kuwezesha wananchi kushiriki katika kukuza uchumi wa Mkoa wa Kigoma na Taifa.

Kwa upande wa Mkurugenzi Mtendaji Mkuu Shirika la Umeme  Tanzania (TANESCO), Mhandisi Gissima Nyamohanga amesema ujenzi wa mradi huo utagharimu dola  za Marekani milioni 144.14 na utachukua miezi 42 hadi kumalizika .
Pia ameishukuru Benki ya Maendeleo ya Afrika  kwa  mkopo nafuu kwa kutoa dola za Marekani milioni 140 huku Serikali ya Tanzania kutia dola  million 4.4.
Amesema mradi wa kufua umeme kwa nguvu ya maji wa Mto Malagalasi upo kilometa 100 kusini mwa Mji wa Kigoma kilometa 27 kusini mwa Barabara Kuu ya Uvinza  – Kigoma katika Kata ya Kazuramimba  Kijiji cha Igamba kwenye Mto Malagalasi wenye lengo kuu la kuboresha  usambazaji wa umeme magharibi mwa Tanzania ili kuchochea shughuli za kijamii na kiuchumi  katika mikoa ya magharibi mwa nchi ikiwemo Kigoma.
Mradi huo utawezesha ongezeko la umeme katika Gridi ya Taifa na kuwezesha biashara ya umeme wa kanda na mradi wa Malagalasi unatarajiwa kuzalisha umeme wa wastani wa gigawati 181 kwa mwaka .

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Thobias Andengenye amesema maono na maelekezo ya Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhusu uzalishaji wa nishati mkoani humo yameuheshimisha Mkoa wa Kigoma na Taifa.

Amesema uzalishaji wa megawati 49.5 za umeme utapunguza gharama za uendeshaji ambapo kwa sasa zinatumika lita 28,000 za mafuta kwa siku kwa ajili ya kuzalisha umeme.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Wenye Ulemavu, Profesa Joyce Ndalichako, akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini Mkataba wa Ujenzi wa Mradi wa uzalishaji umeme wa megawati 49.5 kwa nguvu ya maji katika Mto Malagarasi mkoani Kigoma. Hafla hiyo imefanyika leo Februari 8,2024 jijini Dodoma.

Mkurugenzi Mtendaji Mkuu shirika la Umeme  nchini (TANESCO), Mhandisi Gissima Nyamohanga,akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini mkataba wa ujenzi wa mradi wa uzalishaji umeme wa negawati 49.5 kwa nguvu ya maji k atika Mto Malagarasi mkoani Kigoma. Hafla hiyo imefanyika leo Februari 8,2024 jijini Dodoma.Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Thobias Andengenye, akitoa neno la shukrani baada ya kumalizika kwa hafla ya utiaji saini mkataba wa ujenzi wa mradi wa uzalishaji umeme wa megawati 49.5 kwa nguvu ya maji katika Mto Malagarasi mkoani Kigoma. Hafla hiyo imefanyika leo Februari 8,2024 jijini Dodoma.Washiriki wakisikiliza hotuba ya Naibu   Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko (hayupo pichani), akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini mkataba wa ujenzi wa mradi wa uzalishaji umeme wa megawati 49.5 kwa nguvu ya maji katika Mto Malagarasi mkoani Kigoma. hafla iliyofanyika leo Februari 8,2024  jijini Dodoma.

No comments