Header Ads

ad

Breaking News

WAUMINI WA KIISLAMU MANGA WATOA ONYO WANAOPOTOSHA KUHUSU MGOGORO WA KIWANJA

 

 Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Singida, Shamim Hoza, (kulia) akiongoza upimaji wa  kiwanja kilichopo eneo la Manga Manispaa ya Singida kinachomilikiwa na Jumuiya ya Wanawake wa Kiislamu (JUWAKITA) ambacho mfanyabiashara Philipo Masawe maarufu Medikenya aliuziwa kwa Sh.milioni 50 bila kufuata utaratibu. Kushoto ni Sheikh wa Mkoa wa Singida, Issa Nasoro akiwa na baadhi ya viongozi wa Baraza Kuu la Waislamu (BAKWA)_ Mkoa wa Singida wakati wa upimaji wa eneo hilo.

 ......................................................................................

Dotto Mwaibale na Thobias Mwanakatwe, Singida

 

WAUMINI wa Dini ya Kiislamu Kijiji cha Manga Kata ya Mtipa Manispaa ya Singida wametoa onyo kwa baadhi ya watu wakiwamo waumini wa dini hiyo wanaoendeleza malumbano na upotoshaji kuhusu mgogoro wa kiwanja kilichopo eneo la Manga Manispaa ya Singida kinachomilikiwa na Jumuiya ya Wanawake wa Kiislamu (JUWAKITA), ambacho mfanyabiashara Philipo Masawe maarufu Medikenya aliuziwa kwa sh.milioni 50 bila kufuata utaratibu.

Katibu wa Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA), Kata ya Mtipa, Abdallah Makiya, akizungumza na waandishi wa habari alisema kuna kikundi ambacho kimeendelea kudanganyana kuhusu kiwanja hicho na kumwaminisha mfanyabiashara huyo kuwa, atarejeshewa umiliki licha ya kuwepo kwa maamuzi yaliyotolewa na Waziri wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Jelly Silaa.

Alisema Bakwata inatambua kuwa serikali ipo makini hivyo, kamwe haiwezi kugeuka na kutoa uamuzi mwingine tena tofauti na ule uliotolewa na Waziri wa Ardhi kwenye mkutano wa hadhara wa Rais Samia Suluhu Hassan ya kwamba hati ya kiwanja hicho ambacho kilikuwa kimenunuliwa na mfanyabiashara huyo kwa kutumia nyaraka za kughushi ifutwe.

Makiya alisema Bakwata hivi sasa inasubiria siku 60 zilizotolewa na Waziri wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Singida, Shamimu Hozza kukabidhi hati kwa Bakwata kwa niaba ya Jumuiya ya Wanawake wa Kiislamu Tanzania (JUWAKITA) kwa kuwa ndio wamiliki halali wa kiwanja hicho.

Alisema tatizo kubwa kwa Mkoa wa Singida baadhi ya viongozi wa dini ya kiislamu wameacha kabisa kufuata misingi ya dini na badala yake wanaendekeza majungu,fitina na umbeya jambo ambalo kimsingi halina afya kwa dini na mstakabari wa taifa kwa ujumla.

"Waziri wakati anatolea ufafanuzi wa mgogoro huu wa kiwanja waziri alisema wazi kwamba viongozi wa taasisi ikiwamo ya dini hawaruhusiwi kuuza mali bila idhini ya Baraza la Wadhamini,kwa hiyo hata kiwanja hiki inafahamika waliomuuzia mfanyabiashara huyo kwa njia ya kinyemela ni baadhi ya viongozi wa dini wakati wanatambua kuwa sheria hairuhusu," alisema.

Aidha,taarifa ambazo gazeti hili imezipata ni kwamba waliomuuzia kiwanja hicho mfanyabiashara huyo wanahaha kutaka kwenda kumuona rais wakiamini maamuzi yaliyotolewa na Waziri wa Ardhi Oktoba 16,2023 kwenye mkutano wa hadhara mbele ya rais yatapinduliwa.

Oktoba 16, 2023 Waziri wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Silaa, alimwagiza Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Singida, Shamim Hoza, kufuta hati ya kiwanja alichouziwa mfanyabiashara Philipo Masawe maarufu Medikenya kwa zaidi Sh.milioni 50 kwa kutumia nyaraka za kughushi ambacho kinamilikiwa na Jumuiya ya Wanawake wa Kiislamu Tanzania (JUWAKITA).

Alitoa agizo hilo kwenye mkutano wa hadhara uliokuwa umeandaliwa kwa ajili ya Rais Samia Suluhu Hassan kuhutubia wananchi mjini Singida wakati wa maadhimisho ya kumbukizi (birthday) ya Mkoa wa Singida kutimiza miaka 30 tangu kuanzishwa kwake 1963.

Silaa alifikia maamuzi hayo baada kufanya kikao katika ofisi ya kamishna kusuluhisha mgogoro wa kiwanja hicho namba 2 kitalu  A kilichopo eneo la Manga Manispaa ya Singida  ambacho pia  kilihudhuliwa na mfanyabiashara huyo na kubaini aliyemuuzia aliyefahamika kwa jina moja la Abubakari alitumia nyaraka za kughushi.

 Katika kikao hicho, wanawake wawili Binamu Sagaa na Fatuma Issa waliodaiwa kuweka saini kwenye muhtasari wa mauziano walikana mbele ya waziri kwamba hawakuhusika kabisa na kwamba saini zao zimeghushiwa kuhalalisha uuzwaji wa kiwanja hicho.

"Masawe hapa ndugu yangu unetapeliwa,namwagiza Kamishna wa Ardhi Mkoa Singida kupitia kifungu cha 99 cha sheria ya usajili wa ardhi afute hati ile uliyokuwa umepewa na atoe hati mpya kwa Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Mkoa wa Singida.

Silaa alisema watu wanapaswa kuwa makini wasitapeliwa wanaponunua ardhi kwasababu sheria zipo wazi mali zote za taasisi iwe ya dini au chama haiwezi kuuzwa na mtu binafsi wenye mamlaka ya kuuza mali husika ni Baraza la Wadhamini na si vinginevyo.

Naye mfanyabiashara huyo katika kikao hicho alijitetea kuwa hakatai maamuzi ya serikali ya kufutiwa hati ya kiwanja hicho lakini kwasababu kuna gharama amezitumia kukiendeleza  afikiliwe.

Hata hivyo, Waziri wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi alimwambia mfanyabiashara huyo kwamba gharama zote alizozitumia amdai Abubakari aliyemuuzia kiwanja hicho kwa kutumia nyaraka feki.

Aidha,Silaa alimwagiza Sheik wa Mkoa wa Singida, Issa Nassoro, kuwatangazia viongozi wake kwamba mali zote za taasisi zinamilikuwa Baraza la Wadhamini hivyo hakuna mwenye mamlaka ya kuiuza bila idhini ya baraza hilo.

Upimaji wa kiwanja hicho ukiendelea, baada ya . Oktoba 16, 2023 Waziri wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Jery Silaa, kumwagiza Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Singida, Shamim Hoza, kufuta hati ya kiwanja alichouziwa mfanyabiashara Philipo Masawe maarufu Medikenya
Maafisa Ardhi kutoka Ofisi ya Ardhi Mkoa wa Singida wakiendelea na upimaji wa kiwanja hicho baada ya 
Katibu wa Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA) Kata ya Mtipa, Abdallah Makiya, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kiwanja hicho.

No comments