Header Ads

ad

Breaking News

Wakazi Mziha waipongeza TANROADS Pwani

Meneja wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS), Mkoa wa Pwani, Baraka Mwambage

Na Omary Mngindi, Kibindu

WAKAZI wa Kijiji cha Mziha Mkoa wa Morogoro na kwa Msanja Kata ya Kibindu Bagamoy mkoani  Pwani, wameishukuru Serikali kupitia Wakala wa Ujenzi wa Barabara (TANROADS), mkoani hapa kwa ujenzi wa barabara.

Wakijitambulisha kwa majina ya Swaumu Idd na Ramadhani Said wakazi wa Mziha Morogoro na Juma Ramadhani wa Kwakonje Bagamoyo Pwani, walisema kuwa kwa miaka mingi barabara hiyo ilikiwa inapitika kwa shida.

Walieleza kuwa miaka yote hiyo kipindi cha mvua ilikuwa inapitika kwa shida sana kutokana na kutokuwa ya kiwango cha changarawe, na kwamba kwa sasa maeneo mengi yamewekwa madaraja makubwa na makalvat hivyo inapitika kipindi chote.

"Hili daraja kubwa mnaloliona, hapa palikuwa mpaka kati ya Mziha Morogoro na Kibindu Bagamoyo Pwani, kipindi cha mvua hapapitiki lakini leo pamejengwa daraja kubwa watu na magari yanapita," alisema Swaumu.

Kwa upande wake Ramadhani alisema kuwa barabara hiyo muhimu inayounganisha mikoa ya Morogoro na Pwani imezidi kuwa maarufu kwani magari mengi yanapita baada ya kuboreshwa na TANROAD'S Pwani, huku akiishukuru serikali kupitia wakala hao.

"Hii barabara inaanzia hapa Mziha inapita Kibindu inakwenda kutokea Mbwewe njiapanda ya barabara kuu ya Chalinze Segera, kukamilika kwake kwa kiwango cha changarawe kumeongeza idadi kubwa ya magari kutumia hii wakiingilia Mtibwa kuja kutokea Mbwewe, tunawapongeza TANROAD'S," alisema Said.

Nae Ramadhan mkazi wa Kata ya Kibindu alisema kuwa kukamilika kwa barabara hiyo kumeipatia fursa vijiji vilivyopo kandokando, kwa mabasi kusimama na kununua bidhaa mbalimbali hali inayowaongezea kipato wananchi.

"Tunaishukuru serikali kwa kazi hii kubwa ambayo wameifanya, hatukutaraji kupata barabara yenye kiwango bora kama hiki, pia kwa kazi hii TANROAD'S wametutendea haki," alisema Ramadhani.


No comments