TEUWENI WARATIBU WAADILIFU DAWATI LA JINSIA-MPANJU
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Wakili Amon Mpanju
Na WMJJWM Iringa
NAIBU Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Wakili Amon Mpanju amewataka wakuu wa vyuo vya Elimu ya Juu na Kati kuteua waratibu wa dawati la jinsia waadilifu, katika kutatua changamoto za ukatili wa kijinsia vyuoni.
Mpanju amesema hayo wakati akifungua mafunzo ya namna bora ya uanzishaji wa madawati ya jinsia kwa Wakuu wa Vyuo na Waratibu Madawati ya Jinsia katika taasisi ya elimu ya juu na elimu ya kati Mkoani Iringa Oktoba 31, 2023.
“Nasisitiza uwezeshwaji wa Madawati hayo ya Jinsia kwa kutumia Rasilimali za Serikali au kupitia wadau kuhakikisha madawati haya yanafikika kiurahisi kwa kuweka mfumo mzuri wa mawasiliano ya utoaji wa taarifa za ukatili wa kijinsia," amesema Mpanju.
Mpanju ameelekeza wajumbe wa Madawati ya Jinsia kuendesha Elimu ya kutokomeza matendo ya ukatili wa kijinsia kwa wanafunzi na wanajamii ndani ya Vyuo husika kwani kutokomeza matendo ya ukatili na unyanyasaji kwa wakati kwenye taasisi za Elimu ya juu na ya kati ndio lengo mahsusi la kuundwa kwa madawati hayo.
"Nitoe rai kwa vyuo vya elimu ya juu na kati kuhakikisha wanaanzisha ‘Madawati ya Jinsia’ katika vyuo vyao kwa kutumia Mwongozo wa Uanzishaji, Uendeshaji na Ufuatiliaji wa Dawati la Jinsia wa mwaka 2021 ambao ulishatolewa na unapatikana pia katika tovuti ya Wizara.
Kwa upande wake, mwezeshaji wa mafunzo hayo Dkt. Cyril Komba akifafanua mwongozo wa Dawati la Jinsia kwenye Taasisi za Elimu ya Juu na Elimu ya Kati amesema majukumu yake ya msingi ni kuona ukatili unakomeshwa.
Naye Afisa Maendeleo ya Jamii Mwandamizi kutoka Ofisi ya Rais - utumishi Staricko Meshack akitoa mafunzo kuhusu Daftari la Usajili wa matukio ya ukatili wa kijinsia katika Taasisi za Elimu ya Juu na kati amesisitiza kutumika kwa madaftari hayo.
No comments