Shule ya Inovet yatumia milioni 5 kuvuta maji
Mkurugenzi wa shule, George Ndaki |
Na Omary Mngindo, Kibwende
UONGOZI wa Shule ya Inovet iliyopo Kitongoji cha Kibwende Kata ya Mlandizi Kibaha Vijijini Mkoa wa Pwani, imetumia shilingi milioni tano kuvuta maji shuleni hapo.
Mkurugenzi George Ndaki aliyasema hayo shuleni hapo mbele ya waandishi wa habari, Novemba 12,2023 mkoani Pwani, na kwamba hatua hiyo imetokana na shule kutumia maji ya kisima tangu kuanzishwa kwake mwaka mmoja uliopita.
"Kama unavyoiona shule yetu ipo pembezoni kidogo na mji, hatua hii imetuhamasisha kuja kuwekeza elimu eneo hili, kwa kipindi chote tulikuwa tunatumia maji ya kisima lakini tumevuta maji ya bomba," alisema Ndaki.
Aliongeza kuwa, kwa kipindi cha zaidi ya mwaka mmoja walikuwa wanatumia maji ya kisima, huku wakiendelea na ujenzi wa majengo mengine ya vyumba vya madarasa zoezi lililokwenda pamoja na uvutaji wa maji.
"Sasa tunaelekeza nguvu katika kufikisha umeme shuleni kwetu kwani tunatumia umeme wa sola ambao kipindi cha mvua huwa hauna nguvu, tunaendelea na juhudi hizo ili kukamilisha mchakato huo," alisema Ndaki.
Aidha Ndaki alizungumzia changamoto ya barabara, kutoka njiapanda ya barabara ya Mlandizi Bagamoyo, ambapo kuanzia njiapanda kufika shuleni hapo imejaa mchanga hali inayosababisha magari yao kupita kwa shida.
"Hii changamoto ya mchanga katika barabara ya kuja hapa shule ni kubwa, wakati mwingine magari yanapitia Visiga kutokana na mchanga kisai cha magari kunasa, tunaiomba halmashauri kupitia TARURA iiangalie," alisema Ndaki.
No comments