Header Ads

ad

Breaking News

JKT QUEENS YANG'OKA LIGI YA MABINGWA AFRIKA WANAWAKE

 


TIMU ya JKT Queens imendoshwa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa wanawake baada ya kuchapwa mabao 4-1 dhidi ya AS Casablanca ya Morocco.

 Mchezo huo wa  mwisho wa Kundi A ulipigwa Uwanja wa Laurent Pokou mjini San-Pedro nchini Ivory Coast.

Mabao ya AS Casablanca yalifungwa na Meryem Hajri kwa penalti dakika ya 30, Chaymaa Mourtaji dakika ya 39, N'Guessan Nadège Koffi dakika ya 42 na bao la nne lilitumbukizwa kambani na Sylviane Kokora Adjoua dakika ya 58.

Kwa upande wa JKT Queens, bao lao lilifungwa na Stumai Athumani dakika ya 56. JKT Queens, mabingwa wa Tanzania na Afrika Mashariki na Kati katika mchezo huo kuanzia dakika ya 39, walicheza pungufu baada ya wachezaji wake wawili Happyness Hezron Mwaipaja na Anastazia Simba kutolewa nje kwa kadi nyekundu.

Queens iliingia kwenye mchezo huo bila nyota wake sita kurejea nyumbani kujiunga na kikosi cha timu ya Taifa chini ya umri wa  miaka 20 kufuzu Kombe la Dunia akiwemo mshauri mkuu wa ufundi, Bakari Shime.

Kwa matokeo hayo, JKT Queens inamaliza nafasi ya tatu kwenye kundi lake ikiwa na pointi tatu, mbele ya wenyeji, Athletico Abidjan, wakati Mamelodi Sundowns ikiongoza kundi lao baada ya kuipasua Athletico Abidjan kwenye Uwanja wa Amadou Gon Coulibaly mjini Korhogo ikijikusanyia alama tisa.

Mamelodi Sundowns na AS Casablanca yenye pointi nne, zimesonga mbele hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo.

Bingwa wa michuano hiyo ataondoka na kitita cha dola za Marekani 400,000, mshindi wa pili 250,000, waliokwenda Nusu Fainali 200,000, wanaomaliza nafasi ya tatu kwenye Kundi 150,000 na wanaoshika mkia dola 100,000.

No comments