COTUL YAOMBA SERIKALI KUSAIDIA MANUNUZI MACHAPISHO YA KIELEKITRONIKI
Na Dotto Mwaibale, Singida
SHIRIKISHO la Maktaba za Vyuo Vikuu na Taasisi zinazofanya Utafiti Tanzania
(COTUL) limeiomba Serikali kupitia ofisi ya Waziri Mkuu kusaidia kununua
machapisho ya kielekitroniki yanayotumika
kufundishia vyuoni kwa kuwa yanauzwa bei ghali ambayo shirikisho hilo haliwezi
kumudu kuyanunua.
Mwenyekiti wa Shirikisho hilo , Dkt. Sydney Msonde alitoa ombi hilo Novemba
9, 2023 wakati wa ufunguzi wa kongamano la kisayansi ambalo limewakutanisha
wanataaluma mbalimbali katika ngazi ya wakutubi, walimu wafundishaji
kutoka vyuo vikuu Tanzania Bara na
Visiwani, watafiti pamoja na watu wanaoshughulika na masuala ya teknolojia (IT)
Alisema pamoja na kwamba lengo la COTUL ni kuhakikisha kwamba machapisho ya kielekitroniki yanapatikana kwa walimu na wanafunzi ili waweze kufanya shughuli zao za msingi za kujifunza, kufundisha na kufanya utafiti hapa nchini lakini kununua machapisho hayo imekuwa changamoto kutokana na kuuzwa bei ghali.
Dkt. Msonde alitoa mfano uchapishaji wa kanzi data inayoitwa 'Sience Direct' ambayo inauzwa dola za Marekani 250,000 hivyo sio rahisi kwa taasisi moja za hapa nchini kuweza kumudu kununua chapisho kama hilo.
“COTUL kazi yetu kubwa ni kuhamasisha na kuzileta pamoja taasisi zote za
umma na za watu binafsi ili ziweze kuchangia kwa sehemu rasilimali fedha
zitakazo wezesha kununua machapisho hayo ya msingi katika kukidhi haja ya
kufanya ufundishaji na utafiti nchini,” alisema Dkt. Msonde.
Dkt. Msonde alisema uhaulishaji na upatikanaji wa machapisho hayo unaweza usiwe na tija kama walimu na wanafunzi watakao kuwa wanayatumia hawatajengewa uwezo bora wa kuyatumia jambo ambalo ndilo la msingi.
Alisema lengo la kongamano hilo ni kujadili mustakabari wa fani ya ukutubi
na namna gani walimu katika taasisi za umma na watu binafsi wanaweza kutumia
machapisho ya kielekitroniki katika kuboresha ufundishaji na ujifunzaji kwa
wanafunzi Tanzania.
Naye Mkurugenzi wa Idara ya Ufuatiliaji na Tathmini Ofisi ya Waziri Mkuu,
Sakina Mwinyimkuu, alipongeza COTUL kwa kupiga hatua kubwa katika kipindi cha
miaka 15 tangu shirikisho hilo lilipoanzishwa mwaka 2008.
Alisema shirikisho hilo limekuwa msaada mkubwa kwa serikali kwa kuisaidia
kupata taarifa na maarifa mbalimbali ambayo kwa njia ya kawaida ingekuwa ni
gharama kubwa kuyapata.
"Uwepo wa COTUL ni fursa hata kwa sisi tunaohusika na kufanya tathmini
mbalimbali zikiwemo za utafiti hakika ni jukwaa muhimu sana," alisema
Mwinyimkuu.
Mwinyimkuu alisema Serikali itaendelea kuunga mkono kazi zinayofanywa na
COTUL na kuliomba shirikisho hilo kukutana na wadau wa elimu ndani ya Serikali
ili waone namna ya kushirikiana nao na kuwa kazi zao zinazihitaji na
hazikwepeki hasa katika kipindi hiki ambacho dunia inahitaji teknolojia kwa
ajili kukuza uchumi.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Bodi ya Huduma za Maktaba Tanzania (TLSB),
Dkt. Mboni Ruzegea alisema Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt.Samia
Suluhu Hassan inafanya maboresho makubwa ya maktaba kutoka katika mfumo wa
kuhifadhi vitabu na machapisho mengine kwa njia ya kizamani ya karatasi na
kwenda kwenye mfumo wa kidijitali.
Mmoja wa wafadhili wa kongamano hilo Mkurugenzi wa Kampuni ya Totoo Ltd
yenye makao yake makuu mkoani Kilimanjaro, Dkt. Elvis Silayo alisema changamoto
kubwa inayowafanya watu wengi washindwe kuitumia maktaba kwanza wanakuwa
hawajui taarifa ambazo wanaweza kuzipata
na imekuwa ikichukuliwa kama sehemu ya taaluma na inatakiwa kuwa
mashuleni.
Alisema watu wengi hawapendi kusoma mambo ya taaluma lakini maktaba kuna
taarifa nyingi ambazo wanaweza kuzipata na kuwasaidia kupata maarifa yanayoweza
kuwasaidia katika maisha yao ya kila siku.
Alisema maktaba za sasa zinavitabu vilivyochapishwa kwenye miaka ya 70 na
80 hivyo taarifa zake haziwezi kuwa na msaada kwa mtu anayehitaji kufanya
chochote kwa kipindi hiki na kueleza kuwa maktaba za sasa zinapaswa kwenda
mbele zaidi kwa kuwa na taarifa ambazo zinakwenda na wakati.
Silayo alisema ile dhana iliyozoeleka kuwa maktaba zipo kwa ajili ya
kumuandaa mwanafunzi afaulu mtihani sasa iachwe badala yake zitumike kuwaandaa
kimaisha.
Naye
Mhadhiri wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Dkt. Valeria Kyumana, alisema
mafunzo hayo yamewajenga kwasababu hivi sasa teknolojia inakuwa na maktaba na
huduma wanazotoa haziwezi kuendelea kwa kutumia mfumo wa zamani waliokuwa
wakiutoa.
“Ni lazima tuangalie teknolojia inavyokwenda tukue nayo na kama sisi wakutubi tuweze kuichukua na kuitoa kwa wateja wetu tunaowahudumia ambao ni wanafunzi na watu wengine,” alisema Kyumana.
Baadhi ya wadhamini wa kongamano hilo ni Totoo Company Ltd, Ebsco, Elsevier, Jove, Buku,Eclat, Bookstore, emerad insight, TCC na LexisNexis.
Mwenyekiti wa Shirikisho la Maktaba za Vyuo Vikuu na Taasisi zinazofanya Utafiti Tanzania (COTUL), Dkt. Sydney Msonde akizungumza wakati wa ufunguzi wa kongamano hilo.
Katibu Mkuu Chama cha Wakutubi Tanzania (TLA), Dkt Rhodes Mwageni akizungumza wakati wa ufunguzi wa kongamano hilo.
Keki ya kutimiza miaka 15 tangu kuzaliwa kwa COTUL mwaka 2008 ikikatwa
Makamu Mwenyekiti COTUL, Profesa Kelefa Mwamtimwa, akitoa neno la shukurani kwa mgeni rasmi na wadau wengine wakati wa ufunguzi wa kongamano hilo.
Picha ya pamoja mgeni rasmi na washiriki wa kongamano hilo.
No comments