Wakazi Kimalamisale wamtaka Rais Samia
Mwenyekiti wa Kijiji cha , KimalamisaleSalum Mtego |
Na Omary Mngindo, Kimalamisale
WAKAZI wa Kijiji cha Kimalamisale Kata ya Dutumi Wilaya ya Kibaha Mkoa wa Pwani, wameelezea kiu yao ya kutaka kumuona Rais Samia Suluhu Hassan kijijini hapo, lengo ni kumshukuru kwa kazi kubwa aliyowafanyia.
Shukrani hizo zinatokana na kufikiwa kwa huduma zote muhimu ambazo kwa takribani zaidi ya miaka 50 kama sio 100 hawajawahi kuziona, huku wakikosa imani kabisa kama zinaweza kuwafikia kutokana na kijiji hicho kuwa mbali na makao makuu ya Kata.
Wakizungumza na waandishi wa habari walisema kuwa awali walikuwa Kisarawe na kwamba, miaka miwili na nusu wamehamishiwa Kibaha Vijijini chini ya rais Samia Suluhu Hassan, Mbunge Mwakamo na baraza zima la Halmashauri huduma hizo zimewafikia.
"Tunamtaka rais Samia Suluhu Hassan afike Kimalamisale tumpatie shukrani zetu, kwa zaidi ya miaka 50 kama sio 100 hatujawahi kupata huduma muhimu kama shule, maji ya bomba, umeme, barabara na zahanati tuliishi kama Kisiwani, sasa mambo safi" alisema Mariamu Zinga.
Naye Grace Tegemeo alisema kuwa kwa sasa huduma zote zipo, "Tunaishukuru serikali kwa kututoa katika hali ngumu, hatukuwahi kuwa na huduma muhimu, tuliishi kama kisiwani, tunaiomba itusogezee mabomba majumbani, kwa sasa tunachota katika vizimba," alisema Tegemeo.
Moshi Hamisi, aligusia kilio cha kukosekana kwa kituo cha Polisi kijijini hapo, hivyo inapotokea tatizo wanalazimika kutembea kilometa zaidi ya 20 kwenda kijiji cha jirani cha Kwala Kata ya Kwala, hali inayosababisha adha kubwa huku akiomba kilio hicho kifanyiwekazi.
Jasmine Mussa aliiomba serikali kuboresha huduma za kulazwa katika zahanati yao, ikiwemo umeme kwani inatumika mabetri kuwashia taa, "Pia kutokana na umbali wa Kituo cha afya na hospitali tunaomba tuongezewe daktari sanjali na uboreshwaji wa huduma," alisema Jasmine.
Merina Thomas alisisitizia huduma za kulazwa katika zahanati ikiwemo ujenzi wa wodi, sanjali na maji kusambazwa kwa mabomba majumbani, ikiwa ni kuwasogezea hufuma karibu zaidi.
Mwenyekiti Salum Mtego, amewashukuru viongozi kwa jitihada kubwa zinazofanyika kijijini hapo, huku shukrani zaidi akizipelekwa kwa rais Samia Suluhu na Mbunge Michael wakiwemo baraza la madiwani kwa ujumla.
"Kimalamisale hii sio ya miaka iliyopita, sasa hivi tuna maji safi, umeme, barabara ambayo bado inaendelea kuboreshwa, zahanati yetu nzuri sanjali na majengo mazuri ya shule ya msingi kama unavyoiona," alisemalizia Mtego.
No comments