Header Ads

ad

Breaking News

TAWA WAJIPANGA KUONGEZA MAPATO


NA BEATUS MAGANJA, ARUSHA

MAMLAKA ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), inaandaa mkakati mpya wa ukusanyaji mapato utakaolenga kuongeza mapato ya taasisi hiyo mara dufu ya makisio yake ya mwaka wa fedha 2023/2024.

Hayo yameelezwa leo Oktoba 1, 2023 na Kamishna wa Uhifadhi wa TAWA, Mabula Nyanda, katika kikao kazi na wakuu wa Kanda na wakuu wa mapori wa TAWA chenye lengo la kuboresha utendaji kazi katika nyanja za kuongeza mapato na uhifadhi, kilichofanyika katika ukumbi wa NCAA jijini Arusha.

Kamishna Mabula amesema suala la kuongeza Kasi ya ukusanyaji mapato ni maelekezo kutoka kwa Waziri wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Angellah Kairuki hivyo, utekelezaji wake unapaswa kuanza haraka.

"Suala la ukusanyaji mapato lisisubiri mkakati unaoandaliwa, lianze Kuanzia Sasa hivi, Kila kitu unachokiona kwenye eneo lako ni rasilimali, hakikisha unaitumia kuingiza mapato," amesema Kamishna Mabula.

Kamishna huyo amesisitiza suala la udhibiti wa Wanyamapori wakali na waharibifu na kuwataka maofisa hao kutafuta mbinu mbadala za kuhakikisha Wanyamapori hao hawaendelei kuleta madhara kwa maisha na mali za binadamu.

Amewataka maofisa hao kuzingatia maelekezo aliyotoa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili, Kamishna Benedict Wakulyamba, wakati wa semina elekezi kuhusu Wanyama Wakali na Waharibifu.

Kaimu Naibu Kamishna wa Uhifadhi, Mlage Kabange, amesema mtaji namba moja wa TAWA ni ulinzi wa maeneo yote waliyopewa kuyasimamia kwani, yanapokuwa salama na uzalishaji mapato huongezeka ikizingatiwa kuwa, asilimia 70 ya mapato ya TAWA yanatokana na shughuli za uwindaji wa kitalii.

Kabange amesisitiza kuongeza Kasi ya utekelezaji wa kazi ya kuweka alama za mipaka katika maeneo yote yaliyo chini ya usimamizi wa taasisi hiyo, huku wakifuata miongozo na maelekezo yote yaliyotolewa na Serikali.













No comments