Header Ads

ad

Breaking News

TANZANIA YATHIBITISHWA KUWA MJUMBE WA BARAZA TENDAJI LA SHIRIKA LA UTALII DUNIANI (UNWTO)

Waziri wa Maliasili na Utalii, Angellah Jasmine Kairuki (Mb)

Na Mwandishi Wetu

TANZANIA imethibitishwa na Mkutano Mkuu wa 25 wa Shirika la Utalii Duniani (UNWTO), kuwa Mjumbe wa Baraza Tendaji la Shirika hilo kwa kuchaguliwa bila kupingwa na nchi wanachama wa Shirika la UNWTO. 

Uchaguzi huo ulifanyika Oktoba 19,2023 jijini Samarkand, Uzbekistan ambako Mkutano Mkuu wa 25 wa UNWTO unaendelea. 

Kupitia nafasi hiyo, Waziri wa Maliasili na Utalii, Angellah Jasmine Kairuki (Mb), ataiwakilisha Afrika kwa kipindi cha miaka minne cha 2023–2027, katika mikutano muhimu ya Baraza hilo itayokuwa ikifanyika mara mbili kwa mwaka. 

Akizungumza baada ya Tanzania kuthibitishwa katika nafasi hiyo, Waziri Kairuki ameeleza kuwa, nafasi hiyo ni muhimu katika kukuza na kutangaza utalii wa Tanzania na Afrika kwa ujumla kwa kuwa, Baraza hilo ni chombo muhimu kinachosimamia mipango na bajeti ya shirika pamoja na utekelezaji wake. 

Waziri Kairuki ameongeza kuwa, kupitia nafasi hiyo, Tanzania itashiriki kupeleka agenda muhimu zenye maslahi mapana ya maendeleo ya utalii wa Bara la Afrika na duniani kwa ujumla.

Tanzania na Morocco zilishinda nafasi hiyo ya kuliwakilisha bara la Afrika katika uchaguzi uliofanyika Mauritius wakati wa mkutano wa Kanda ya Afrika, katika mkutano huo duniani zilihitajika kura za wanachama kutoka mabara mengine ili kuthibitishwa katika nafasi hizo.



No comments